Kamishna Kafulila azimegea wizara siri

NA MWANDISHI WETU

KAMISHNA wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ,Wizara ya Fedha na Mipango David Kafulila amesema kuna kila sababu wizara zote kukaa kuona wanavyoweza kutumia uwepo wa fursa ya sekta binafsi kupunguza mzigo wa deni la Serikali, kupunguza ulazima wa kodi kutumika kutekeleza miradi inayoweza kutekelezwa na sekta binafsi ikiwemo miundombinu ya barabara.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 2,2023 jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi cha siku tano ambacho kimewakutanisha wadau kutoka Serikalini na Wataalam kutoka Taasisi ya Benki ya Dunia inayojihusisha na utoaji wa mikopo na misaada ya kiufundi kwa Sekta Binafsi kwa ajili ya kupitia na kujadili miradi ya kimkakati ambayo Serikali inataka itekelezwe kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi.

Pamoja na mambo mengine Kafulila amesema wananchi lazima wawe tayari kulipia sehemu ya huduma kupitia miradi inayotekelezwa kwa ubia na kutumia mabilioni ya fedha, akitoa mfano ukitengeneza barabara kwa utaratibu wa sekta ya Ubia tafsiri yake watu watapita kwenye barabara ile kwa kulipia.

"Ni kweli kwamba ukipita kwenye barabara ya kawaida kwa foleni tulizonazo inawezekana unaingia gharama kubwa kuliko kama ungelipia , huo ni uzoefu wa duniani kote kwa hiyo tunajenga miundombinu hii ya barabara kama ya kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa utaratibu wa Ubia ...

"Lakini utakuwa na wajibu wa kulipia huduma ili kusudi upunguze hasara ambayo ungeipata kwa kutotumia hiyo huduma kwa kukaa barabarani kuliko ungepita kwenye barabara ambayo ungelipia ya mwendo kasi ,huko ndiko Dunia iliko, tunapotekeleza miradi mikubwa ya kimkakati tunaiwezesha Serikali kutokopa fedha ili kuitekeleza au kuongeza kodi,"amesema.

Amefafanua kwamba hadi kufikia Februari mwaka huu 2023 deni la Serikali zote duniani ilikuwa zaidi ya dola trilioni 226 lakini ndio mfumo wa Dunia kwa maana ya uzalishaji duniani kuwa takribani dola trilioni 105, kwa tafsiri nyingine ni ukubwa wa mikopo Dunia ilikuwa na mkopo mkubwa kuliko kiasi inachozalisha.

"Tafsiri yake uchumi wa Dunia unaendeshwa kwa mkopo, sisi Tanzania tuna nafuu kidogo deni letu la Taifa liko kwenye asilimia 40 ya uchumi kwa maana ya uzalishaji lakini hatuwezi kubweteka tukasema tutaendelea kuwa hivi kama hatuchukui njia mbadala, kwasababu mahitaji ya miundombinu ni makubwa.

"Wananchi wanahitaji huduma bora ambazo zinahitaji miundombinu zaidi,tafiti zinaonesha kati ya sasa na mwaka 2050, mahitaji ya miundombinu ya mwaka 2050, miundombinu iliyopo sasa inatosha theluthi moja tu ya mahitaji ya mwaka 2050.maana yake kati ya sasa na 2050 tunahitaji kujenga miundombinu mara mbili tuliyojenga katika karne nzima.

"Nasema karne nzima kwasababu kuna miundombinu ambayo ina miaka zaidi ya 100 kama reli ya kati na tunaitumia mpaka leo,kwa hiyo ukiwa na jicho la mbali kama tunavyoangalia kwenye miundombinu kwa mwaka 2050 ,unaona haitakuwa vema kutegemea kodi na mikopo ya kufikia malengo ya miundombinu ambayo unahitajika kwa ajili ya ujenzi wa uchumi kufika mwaka 2050.

"Kwa hiyo ndio sababu tunakuja na hii PPP ambao ni Ubia kati ya sekta ya umma na Serikali ili sekta binafsi ifanye baadhi ya mambo ambayo Serikali ingefanya na Serikali ifanye ambayo sekta binafsi hawezi kabisa kufanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news