Musoma Vijijini waguswa na mchango wa Prof.Muhongo kuhusu uwekezaji uvuvi wa vizimba

NA DIRAMAKINI

WANANCHI wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamempongeza Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo kwa mchango wake alioutoa kwa Serikali wa kuwekeza katika uvuvi wa vizimba katika kuifanya sekta ya uvuvi izidi kuwa na mchango katika maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa nchi.
Wakizungumza na DIRAMAKINI kwa nyakati tofauti leo Mei 4, 2023 wananchi hao wameunga mkono ushauri huo alioutoa Prof. Muhongo Bungeni jijini Dodoma Mei 3, 2023 wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Prof. Muhongo wakati akichangia alisema, "Uvuvi uwezeshwe kutoa chakula cha kutosha (food security), ajira na uchangie kwa kiasi kikubwa uchumi wa Taifa letu. Pia suluhisho la ukosefu wa samaki ndani ya maziwa yetu makuu, ni kuwekeza kwenye uvuvi wa vizimba (aquaculture)."alisema na kuongeza kuwa.

"Utafiti ufanywe kwenye aina mbalimbali za samaki (species of fish) walioko kwenye maziwa makuu yetu."

Mathias Bwire ni mkazi wa Nyakatende katika Jimbo la Musoma Vijijini akizungumza na DIRAMAKINI kwa njia ya simu amesema, ushauri wa Profesa Muhongo una tija kubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuchangia uchumi wa taifa kukua endapo Serikali itaufanyia kazi kikamilifu.

"Kama alivyoshauri Prof.Muhongo ni vyema Serikali yetu ikajikita kutoa mikopo kwa wavuvi kusudi sasa waingie kwenye uvuvi wa vizimba ambao utakuwa na tija na huu uvuvi muda mwingi Prof. Muhongo amekuwa akiulilia na kutoa msisitizo kwa wana Musoma Vijijini hasa vijana tutumie vizimba kutokana na umuhimu wake kwani samaki wanapungua katika ziwa letu Victoria," alisema Bwire.

Kwa upande wake Joseph Omory mkazi wa Nyegina alisema, vijana wengi hivi sasa wanakabiliwa na tatizo la ajira, lakini endepo Serikali itawapa mikopo vijana wakajiingiza kuwekeza katika uvuvi wa vizimba vijana wataondokana na tatizo la ajira watajikwamua kiuchumi kwa kuuza samaki wao.

"Prof. Muhongo dhamira yake ni kuona wana-Musoma Vijijini na Watanzania wananufaika na uwepo na maziwa ikiwemo Tangayika, Nyasa na Victoria wakati akichangia alitoa ushauri Serikali kuwakopesha Watanzania waanzishe viwanda vya samaki ushauri wake nauunga mkono kwa dhati kwamba viwanda vya samaki vikiwa vingi vijana watapata ajira na serikali itapata mapato. Lakini ili tuwe na samaki wengi lazima uwekezaji kwenye uvuvi wa vizimba ufanywe kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyo sasa."

"Niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ina mpango wa kuwakopesha wavuvi wafanye uvuvi wenye tija jambo hili ni jambo la faraja kwa wavuvi na pia limelenga kuifanya sekta ya uvuvi ilete manufaa,"alisema Winfrida Mafuru na kuongeza kuwa.

"Lakini niungane na ushauri wa Prof. Muhongo kumuomba Waziri mwenye dhamana kufanya utafiti kujua kama aina nyingine za samaki kama bado zipo ndani ya maziwa yetu hii itasaidia Kama samaki aina nyingi wapo tujue na masoko yao yapo wapi ili tuuze tupate fedha Kama taifa hili linawezesha chini ya uongozi tulionao ambao uko makini kabisa chini ya Rais Samia Hassan."alisema Winfrida Mafuru.

Naye Gidion Juma Mkazi wa Tegeruka Jimbo la Musoma Vijijini alisema kuwa."ili sekta ya uvuvi iendelee kuleta nageuzi ya kiuchumi Serikali haina budi kuzingatia ushauri uliotolewa, wakati Prof. Muhongo akichangia alisema China wamefanikiwa sana kutokana na uvuvi wa Vizimba kuzalisha tani nyingi. Akasema pia Egypt ambao ni wa- Africa wenzetu wako juu nasisi Tanzania twende tuwekeze katika uvuvi huo naamini Serikali yetu iko Makini itafanikiwa kuwawezesha wavuvi," alisema Gidion.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news