Rais amfuta kazi Waziri wa Viwanda, Nishati na Madini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Tunisia, Mheshimiwa Kais Said amemfukuza kazi Waziri wa Viwanda, Nishati na Madini,Naila Nouira Al-Kenji bila kutaja sababu yoyote.

Uamuzi huo umechukuliwa Mei 4, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, hayo yanajiri ikiwa ni mara ya pili kufutwa kazi kwa afisa wa serikali ya Tunisia ndani ya mwezi mmoja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Tawfiq Charafeddine pia kufutwa kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Kamal Feki.

Aidha, taarifa hiyo haikutaja sababu ya kufutwa kazi, na serikali ya Tunisia pia haikuzungumzia suala hilo. Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vinadai kuwa, huenda kufukuzwa kazi kwa maafisa hao kunaweza kuhusishwa na mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaoendelea nchini humo.

Tunisia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na machafuko ya kijamii tangu mapinduzi ya 2011, na janga la UVIKO-19 limezidisha changamoto za kiuchumi.

Changamoto za kiuchumi za nchi hiyo zimechangiwa zaidi na mvutano wa kisiasa kati ya Rais Kais Said na Bunge. Uamuzi wa rais wa kusimamisha Bunge, kumfukuza kazi Waziri Mkuu na kuchukua mamlaka ya utendaji, ulisababisha maandamano makubwa ya Watunisia na ukosoaji kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Marekebisho ya Serikali ya Tunisia yamezua hisia tofauti kutoka kwa wananchi na viongozi wa kisiasa, huku baadhi wakipongeza kuwa ni hatua muhimu ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa za nchi hiyo, huku wengine wakiikosoa kuwa ni ukiukaji wa taasisi za kidemokrasia nchini humo.

Kufukuzwa kazi kwa Waziri wa Viwanda, Nishati na Madini huenda kukaleta athari katika sekta ya nishati nchini ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi.

Sekta hiyo imekuwa ikijitahidi kuvutia wawekezaji kutoka nje, huku serikali ikizingatia nishati mbadala na kujaribu kuongeza uwazi na ushindani. Uamuzi huo unaacha maswali mengi juu ya kipi ambacho kitajiri na madhara gani ambayo yanatarajiwa kwenye sekta ya nishati na uchumi wa nchi kwa ujumla.(Mashirika)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news