Rais Dkt.Mwinyi:Tunategemea uwekezaji mkubwa kutoka Qatar

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, siku chache baada ya kushiriki mkutano wa Kimataifa wa Kibiashara mjini Doha nchini Qatar ambapo alifanya mazungumzo na wadau mbalimbali nchini humo anatarajia ugeni mkubwa nchini, kwani walionesha utayari wa kuwekeza na kufanya biashara nchini.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 30, 2023 katika vikao vya kawaida vya kila mwezi na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu nchi.

"Nilipata fursa ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa Kibiashara unaoitwa Qatar Economic Forum uliofanyika katika mji wa Doha, niseme tu kwamba mkutano ule ulikwenda vizuri, masuala mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji katika mkutano ule yalizungumzwa. Na sisi kama Zanzibar na Tanzania kwa ujumla tulipata fursa ya kueleza fursa mbalimbali zilizopo katika nchi yetu.

"Nilikuwa nimeambatana na wakurugenzi watendaji kwa upande wetu huku ni ZIPA na kwa upande wa Jamhuri ni TIC ambao walipata nafasi ya kutoa maelekezo ya kina ni maeneo gani ambayo tungependa kupata uwekezaji na biashara kwa ujumla.

"Kwa upande wetu (Zanzibar) tulisisitiza sera yetu ya Uchumi wa Buluu katika maeneo ya vipaumbele vile vitano, tulizungumza juu ya suala zima la utalii, na kwa kweli wengi wamehamasika sana kule kwamba wangependa sana kuja kuwekeza katika maeneo ya utalii, iwe utalii wa fukwe, iwe utalii wa mambo ya kale au utalii wa kisasa wa mikutano.

"Lakini kwa upande wa mafuta na gesi, Qatar ndiyo kwao,gesi wanazalisha nyingi na wana uzoefu wa miaka mingi na utajiri wao mkubwa umetokana na gesi, kwa hiyo wapo tayati kuja kusaidia na kuangalia fursa zilizopo huku katika suala zima la mafuta na gesi.

"Tulizungumza vile vile kuhusu suala la uvuvi, na usindikaji wa bidhaa za bahari nao wana uzoefu na wana makampuni makubwa,ndani ya nchi yao na nje ya nchi yao ambao wamewekeza huko, kwa maana hiyo fursa ambayo tumewaonesha na fursa nyingine kubwa ni ya bandari, nao wapo tayari kuja kuwekeza.

"Lakini wamesisitiza kwamba wao ni watu wa fedha na mara nyingi huwa wanafanya kazi na wataalamu kwa maana ya makampuni makubwa ya Kimataifa, ndiyo huwa wanafanya nao kazi. Kwa hiyo yakiwa tayari yale makampuni wapo tayari kuja kushirikiana nayo kwa kutoa fedha zinazohitajika.

"Kwa hiyo kwa ujumla ilikuwa ni ziara nzuri sana, nimepata fursa ya kuonana na watu wengi sana, mawaziri kadhaa, Mfalme mwenyewe wa nchi ile pamoja na Waziri Mkuu,wote tumebadilishana mawazo na kwa kweli tuna mategemeo makubwa,kwamba sasa tutaanza kuona uwekezaji kutoka nchi ya Qatar ukija Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara vile vile katika maeneo kadhaa ambayo tuliyajadili.

"Ni mategemeo yetu, ndani ya muda mchache ujao tutaanza kupokea timu za wataalamu watakaokuja kwa ajili ya kuja kujionea wenyewe zile fursa ambazo tuliwaeleza zinapatikana hapa,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news