Serikali yatoa onyo kwa wafugaji Namtumbo

NA YEREMIAS NGERANGERA

MKUU wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Ngollo Ng’waniduhu Malenya amewaonya wafugaji wa wilaya hiyo na kuwataka kuacha kupuuza maagizo ya viongozi ya kuwataka kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi ili kupisha maeneo ya hifadhi na maeneo ya kilimo.

Akizungumza na wafugaji na wananchi wa Kijiji cha Mtelamwahi,Njomlole ,Ligera na Namahoka mkuu wa wilaya ya Namtumbo alisema maagizo ya viongozi yanapaswa kuheshimiwa ya kuwataka kuondoka katika maeneo yasiyorasmi.

Malenya aliwaambia wafugaji kuwa wanapaswa kuondoka Namtumbo kwa kuwa hakuna maeneo yaliyotengwa kisheria kwa ajili ya mifugo na kuendelea kubaki katika maeneo yasiyorasmi ni kukaidi maamuzi ya serikali.

Aliwataka kuondoa mifugo yao na kuipeleka katika wilaya ya Tunduru ndiko ambako serikali imetenga vitalu kwa ajili ya wafugaji kufanya shughuli zao za ufugaji katika maeneo hayo bila kuingiliana na wakulima.

Hata hivyo Malenya aliwahakikishia wafugaji hao kuendelea kuwa na imani ya kutotaka kuondoka katika maeneo yasiyorasmi ni kujidanganya kwani serikali wilayani Namtumbo haiwezi kuvumilia kuona uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji,ukataji miti hovyo kwa wafugaji ukiendelea,kulisha mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na kuchunga na kulisha mifugo mazao ya wakulima na kuharibu ardhi kwa ajili ya kilimo.

Pamoja na hayo mkuu wa wilaya huyo alidai wilaya imeanza kuwaondoa wafugaji katika maeneo yasiyorasmi lakini baadhi ya viongozi wa vijiji hushirikiana na wafugaji hao kwa manufaa yao kuvuruga zoezi hilo na waliotuhumiwa na wananchi kuhujumu zoezi hilo walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Namahoka Herman Kapinga alisema kijiji chake kina wafugaji wanne lakini wafugaji hao wanasababisha shughuli za kilimo zisifanyike na zikifanyika hugeuka malisho ya mifugo yao.

Kapinga alidai kuwa serikali yake iliwaandikia barua wafugaji hao ya kuwataka kuondoka katika maeneo ya kijiji hicho kwa kuwa hawana vibali vya kuingiza mifugo katika maeneo ya kijiji, lakini mpaka sasa hawajaondoka kijijini hapo alisema mwenyekiti huyo.

Hamis Ng’amba mkazi wa kijiji cha Namahoka pamoja na kumpongeza mkuu wa wilaya kwa kitendo chake cha kusikiliza kero kutoka kwa wananchi na kuzipatia ufumbuzi ,alimwomba mkuu wa wilaya huyo swala la kuwaondoa wafugaji wanaokaidi kuondoka kijijini hapo lifanywe na ngazi ya wilaya kwa kuwa wanavyombo vya ulinzi na sio serikali ya kijiji .

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo anafanya ziara ya kutembelea vijiji vya wilaya ya Namtumbo kuzungumza na wananchi kwa kusikiliza kero na kuzipatia ufummbuzi huku akiwaonya wafugaji ambao wanaendelea kusalia katika maeneo yasiyorasmi licha ya kuwataka kuondoka katika maeneo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news