SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-18

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...Hakuna mchawi yeyote kambini hapo aliyekuwa akifikiria mtego huo, hata hivyo kila mmoja alipiga saluti akimpongeza mtoto huyo ambaye alikuwa nabii kwa jamii yao.

Endelea

Gari aina prado nyeusi macho ya panzi iliyotengenezwa na makaburu wa Afrika Kusini, gari hilo lilikuwa likipaki kanisani hapo. Ndani yake kulikuwa na Padri Samson Mcjohn, wazungu watatu na watumikiaji wawili.

Walishuka ndani ya gari wakalakiwa chini na waumini wenye tabia ya kujipendekeza. Katika makanisa na misikiti huwa kuna watu vimbelembele sana kwa wageni.

Hasa wanapogundua mgeni mwenyewe ni mzungu au mwarabu, akili zao huwa zinadumaa na kuwaona wageni hao ni wa maana.

Kumbe wageni wengine huwa ni washenzi wakubwa, kwa mfano Padri na wageni wake hao walikuwa washenzi wakubwa.

Endapo jamii ingelitambua mambo ya hovyo ambayo hufanywa na wengi wao wa wageni hao, wasingelijaribu kuwashobokea.

Kanisani hapo kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamekuja kushuhudia ndoa ya kijana huyo. Shamrashamra zilikuwa nyingi kanisani hapo, kanisa lilijaa idadi ya waamini na washuhudiaji wa ndoa hiyo. Padri na wageni wake waliingia kanisani kisha wakapitiliza kwenye chumba cha kuvalia.

Wale wazungu watatu walioambatana na yule padri walikuwa pia ni mapadri waliokuwa wamekuja eneo hilo kwa kazi maalumu.

Waliletwa na taasisi mbalimbali kuja kumsaidia Padri Samson Mcjohn kumteketeza mtoto THE BOMBOM. Lengo lao ilikuwa ni kuzima ndoto ya Waafrika kuwa na nabii ambaye alitabiriwa miaka mingi iliyopita.

Mapadri hao waliungana na Padri Samson Mcjohn kuendesha misa ya ndoa hiyo. Bwana harusi alikuwa mzima kabisa akiwa kakaa eneo maalum kwa ajili yake, alikuwa katinga suti moja ya kijivu iliyomfanya aonekane mwemwele mwemwele. Kengele iligongwa ya kuanza ibada, waumini walisimama huku kwaya ikihanikiza kwa nyimbo.

Mapadri waliingia wakiwa wameambatana na watumikiaji wakiwa wamevalia majoho ya ibada. Chetezo iliyokuwa na ubani ilizungushwa altarini huku moshi ukizagaa ndani ya kanisa hilo.

Padri Samson alikuwa mtu wa kwanza kusogea altari na kuibusu, wale Mapadri wengine walifanya hivyo hivyo kama alivyofanya mtangulizi wao. Waumini wote walikuwa wamesimama huku wakiimba wimbo uliokuwa ukiendelea.

Bibi harusi alionekana kuwa na furaha sana, ilikuwa siku yake maalumu katika maisha yake. Alikuwa haamini kilichokuwa kikiendelea kanisani hapo, zilikuwa zimesalia dakika chache tu pingu za maisha baina yake na mumewe ifungwe.

Padri aliwataka maharusi kupita mbele ili shughuli ya ndoa ianze, maharusi walitii kwa kupita mbele wakiambatana na wasaidizi wao.

Ghafla bwana harusi alidondoka chini na kubamiza kichwa chake sakafuni, mayowe yalisikika pande zote kanisani humo.

Macho yalimtoka bwana harusi huyo huku damu zikimtiririka masikioni, puani na mdomoni mwake. Padri Samson alishituka kuona tukio hilo, alimsogelea bwana harusi huyo, lakini hakumgusa mwili wake.

Tayari alikuwa na wasiwasi juu ya tukio hilo lililokuwa likiendelea mbele yake, hakubaini kuwa bwana harusi huyo alikuwa alishauawa toka jana usiku.

Padri aliagiza watu kumbeba bwana harusi huyo ili kumtoa nje, walijitokeza wanaume kadha wakambeba na kumtoa nje ya kanisa hilo.

Walipomfikisha nje walimlaza kwenye kivuli chini ya mti mkubwa huku wakimpepea kwa nguo, hakuwa na uwezo wa kuongea kitu chochote. Baada ya muda mfupi bwana harusi huyo alikata roho, huku wakimshuhudia ndugu zake.

Ulikuwa ni msiba wa kusikitisha, ndoa ilibadilika kuwa shubiri. Badala ya furaha ilikuwa karaha, hakuna aliyekuwa akiamini alichokuwa akikiona. Bwana harusi alikuwa kaaga dunia kabla ya kufunga ndoa kanisani hapo.

Bibi harusi alikuwa hajitambui kwani tayari alikuwa kazimia, wazazi wake na wazazi wa bwana harusi nao walizima. Hali haikuwa rafiki tena kanisani hapo, majonzi yalitawala eneo hilo huku kila mmoja akitoa machozi.

Kwa upande wa Padri Samson na wale Mapadri wageni walijadili kwa kina tukio hilo wakiwa altarini. Lilikuwa ni tukio la kwanza katika utumishi wao, bwana harusi kufariki mbele yao kabla ya kufunga ndoa!

Baada ya hapo walikubaliana kumrudisha marehemu kanisani humo ili ibada hiyo waimalizie kwa kutoa sadaka. Sherehe ya furaha ilibadilika kuwa shubiri, vilio viliendelea kutamalaki eneo hilo, muda wa kutoa sadaka ulifika.

Pembeni mwa kanisa hilo upande wa nyuma kulikuwa na bibi mmoja kikongwe, aliyekuwa amefika kanisani hapo kwa ajili kushuhudia ndoa hiyo.

Alijikongoja kuelekea sehemu ya sadaka huku akiwa kashikilia vyema mkongojo wake, alipofika eneo la sadaka alitumbukiza noti mbili za elfu tano na elfu mbili kisha akaondoka.

Bibi huyo alikuwa kaandaliwa na wachawi kukamilisha mpango wao. Hakuna aliyekuwa akijua nini kilichokuwa kikiendelea, watu wakiendelea kutoa sadaka zao.

Miongoni mwa watoa sadaka alikuwepo pia mzee mmoja aliyekuwa amekaa upande mwingine tofauti na yule bibi kikongwe. Naye alisogea kwenye sanduku la sadaka na kutoa noti mbili, noti ya elfu tano na elfu mbili kisha akarudi kukaa.

Misa ilipokamilika walimchukua maiti wao na kuondoka, msafara wa magari ulibeba waombolezaji badala ya washangiliaji.

Yule bibi na babu walifanikiwa kutimiza malengo waliyokuwa wametumwa. Waliondoka na kurudi kambini kwao, bahati nzuri hawakuwa wenyeji wa kijiji hicho, hivyo hawakuwa wakitambulika na mtu yeyote.

Walipofika kambini waliwakuta wachawi wachache, wengi wao walikuwa wemekwenda eneo la tukio. Kwa kuwa walikuwa katika maumbo ya kichawi, bibi na babu huyo waliambatana kuelekea kwenye eneo la tukio.

Walipofika eneo lenyewe waliwakuta wachawi wengi wakiwa wanasubiria, baada ya kufika hawakuchelewa kuelezea namna ndoa ilivyobadilika kuwa shubiri.

Baada ya hapo waliungana kuwasubiria Mapadri hao na watumikiaji, walengwa wa ajali hiyo walikuwa ni wale wazungu. Tayari mtoto THE BOMBOM alikuwa ameshawaelezea wachawi wenzake lengo la uwepo wa wazungu hao nchini mwetu.

Mmoja wa wazungu hao alikuwa ni raia wa Uingereza, mwingine alikuwa raia wa Marekani na yule wa mwisho alitoka Ufaransa.

Watu hawa walikuwa wameletwa maalumu na taasisi zao kwa shughuli moja ya kumuua nabii wa Kiafrika mtoto THE BOMBOM. Mambo yalikuwa yamebadilika, muwinda huwindwa, wakati huo wao walikuwa wakiwindea pasipo kujua.

Baada ya misa Padri huyo alizichukua sadaka na kuziweka ndani ya gari lake, kisha aliambatana na wale wazungu kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo. Kule walijadili mambo kadhaa huku akiwahakikishia kuwa eneo hilo ndilo wanaweza kumpata mtoto huyo kirahisi.

Aliwaelezea kwa kifupi kambi ya kichawi iliyomo kijijini humo, hakusita kuwaeleza kila jambo alilokuwa akilijua juu ya kambi hiyo. Aliwafafanulia uimara wa kambi hiyo na udhaifu wake.

Mazungumzo baina yao yalikuwa marefu, kila mmoja alitoa mbinu ambazo zingerahisisha kuiteka kambi hiyo na hatimaye kumchinjilia mbali mtoto huyo.

Katika kikao chao wote walikubaliana kuwa hata msiba wa bwana harusi aliyefariki umesababishwa na kambi hiyo, hivyo walipanga kurudi jioni kuwashikisha adabu. Walipanga mipango yao kwa utulivu mkubwa huku wakiwa na uhakika kurudi usiku wa siku hiyo.

Walipanda ndani ya gari na kwenda msibani, kule msibani walipanga mipango mbalimbali ya namna ya kumhifadhi marehemu wakishirikiana na wazazi wa marehemu.

Walipokamilisha kazi hiyo waliamua kurudi parokiani wakisisitiza kurudi kesho yake, moyoni walikuwa walikuwa na ajenda ya siri ya kurudi usiku kwa ajili ya kuishughulikia kambi ya kichawi iliyopo kijijini hapo. Baada ya hapo waliingia kwenye gari lao na kuondoka, njiani walikuwa wakiendelea kupanga mipango ya jioni hiyo.

Nyuma ya usukani Padri Samson Mcjohn alikuwa akiliendesha gari hilo kwa kasi ya ajabu akielekea Parokiani kwake. Ndugu msomaji unadhani Padri Samson Mcjohn atawakwepa tena wachawi kama alivyofanya awali? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua kinachohusiana na KANISA LA KICHAWI chini ya mtunzi mahiri WILLIAM DAUD BOMBOM.

TINGITINGI MMBOGA?

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news