SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-29

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...akachomoka mbio kuelekea nyumbani kwake, lengo lake ilikuwa kujinusuru na dhahama iliyokuwa mbele yake. Alipofika kwa mbele kidogo alipigwa mtama akajibwaga chini mithili ya furushi la magimbi.

Endelea

Alinyanyuka na kuanza kukimbia akiifuata barabara iendayo kwenye ubao wa shule hiyo. Alipofika kwenye ubao huo alishika barabara iendayo machinjioni kupitia kwa Bhukebhuke, kipigo alichokipata hakukitarajia maishani mwake.
Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji mara nyingi waganga huhudhuria sherehe za kichawi kama alivyohudhuria mganga huyu.

Kinachowafanya kuhudhuria sherehe hizo ni kupima kiwango cha dawa walizo nazo. Endapo mganga atafanikiwa kuhudhuria sherehe hizo, kiwango chake cha kujiamini huongezeka mara dufu.

Siku zote sherehe za kichawi zimegawanyika katika makundi mbalimbali, zipo zinazohusu vikao vyao wenyewe ambazo huwa za kawaida kwa kuwa huwa hazina watu wengi.

Aina nyingine ni sherehe za kuwatawaza viongozi wao wakuu, sherehe hizo ndizo huwa kubwa kuliko sherehe zozote. Katika sherehe za namna hiyo, hualikwa wachawi wa sehemu mbalimbali wenye mahusiano meme na kundi la wachawi husika.

Ni sherehe ambazo huchinjwa binadamu wengi kwa ajili ya kula nyama zao, ng'ombe, mbuzi, kondoo mamia kwa mamia huchinjwa pia.

Katika sherehe hizo chakula kikuu ni nyama za binadamu, wachawi kwa asili hupendelea sana nyama hasa za binadamu.

Nyama ya binadamu iko tofauti kidogo na ile ya wanyama wengine, rangi yake ni nyekundu ina vinyuzinyuzi vinavyoshuka na kupanda. Ni nyama iliyopoa lakini ni tamu kuliko maelezo, ndiyo maana wachawi huipendelea sana.

Aina nyingine ya sherehe ya kichawi ni ile ya kubadilishana madawa. Kuna muda wachawi wa eneo fulani hukutana na wachawi wa eneo jingine kubadilishana uchawi wao.

Hapa pia huwa kunafanyika sherehe kubwa ambayo huambatana na uchinjwaji wa binadamu na wanyama wengine. Aina nyingine ya sherehe ya kichawi ni hiyo iliyokuwa imefanyika siku hiyo, sherehe hii ilikuwa ya kukaribisha wachawi wageni.

Sherehe hii ilionekana kuwa kubwa kwa kuwa miongoni mwa wachawi wapya waliokuwa wamekaribishwa alikuwemo mke wa Mganga Hoja.

Huyo mganga kwa kiasi kikubwa alikuwa akiwasumbua sana wachawi wa maeneo hayo. Kuna muda alikuwa akimwaga madawa hata kwenye njia za kupita wachawi.

Siyo kila njia mchawi anapokwenda kuwanga hupita, zipo njia maalumu ambazo hupita wakati wa kutoka au kuingia. Wachawi wakawa wanamuonya lakini alionekana kuwa jeuri kulingana na nguvu ya madawa aliyokuwa nayo.

Huyu Mganga Hoja amewahi kuwazuia wachawi kumuua kijana mmoja mwenyeji wa mtaa wa Kilimo. Wachawi walifanikiwa kumuua na kumficha nyuma ya mlango wa nyumbani kwao, kipindi cha kwenda kumzika kilipofika walipokwenda kumchukua nyuma ya mlango hawakumuona.

Suala hili liliwasumbua sana wachawi hao, baada ya kuchunguza walibaini Mganga huyo ndiye aliyefanya mambo hayo. Hata walipomfuata kufanya suluhu aliwafukuza na kuwatolea maneno ya shombo.

Mganga huyu alionekana kuwa jeuri na mwenye kujiamini kuliko kawaida, hakuogopa shirika kubwa la kichawi yeye eliendelea kuwasumbua.

Kuna muda aliwahi kuunguza nyumba waliyokuwa wakihifadhiwa misukule, wachawi walibaini na kumfuata lakini majibu yake yalikuwa ya kejeli. Eti alikuwa akijaribu uwezo wa dawa zake alizokuwa ameoteshwa kipindi hicho.

Mganga Hoja ni miongoni mwa Waganga waliokuwa wakijiamini sana kupitia dawa zake. Kuna muda alikuwa akiwatega fisi wa wachawi hao na kuwaua pasipo hata sababu.

Wachawi wa mtaa huo walipojaribu kumsaka kwa namna yeyote ile walishindwa, inasemekana wakati wa usiku alikuwa halali nyumbani kwake.

Kila ulipofika muda wa usiku, yeye aliuhamishia mji wake hewani, kwa hiyo wachawi walipojaribu kumfuata nyumbani kwake hawakumuona.

Ni miongoni mwa Waganga waliodiriki kuzindika uwanja wa shule ya Msingi Mhandu na madarasa yake. Akazuia kwa muda mrefu wachawi kwenda kucheza au kufanya shughuli zao maeneo hayo.

Kwa kifupi Mganga Hoja alijiamini kupitiliza, jambo hilo liliwatia hasira wachawi hao. Walipojaribu kuwaua watoto wake ilishindikana, kila njia waliyoijaribu ilishindikana.

Alikuwa kajiganga kuanzia mate, nyayo, mkojo, sauti, mwili, kinyesi, damu, kucha na nywele. Pia alikuwa kajiganga, nguo, jasho na uchafu wa mwili jambo lililosababisha wasimtie mikononi mwao. Wagonjwa waliopelekwa kwake aliwatibu bila kuogopa, hata wagonjwa ambao walikuwa na chapa aliwatibu pasi na kuogopa.

Wachawi wa kundi hilo walikaa na kubuni njia za kumnasa Mganga Hoja, maana kila njia waliyobuni mwisho wake ilikuwa ni chungu kwa upande wao.

Hatimaye wakaja na wazo la kumrubuni mke wake ili iwarahisishie kazi. Mipango kabambe iliandaliwa kwa mkewe kupitia shoga yake ambaye alikuwa mchawi, ulikuwa ni mpango makini uliochukua mwaka mzima.

Hatimaye mama huyo siku hiyo alikuwa kahudhuria kwenye sherehe ya kichawi hiyo, huu ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa kambi hiyo ya kichawi.

Mama huyo alikuwa akiandaliwa kuwasaidia wachawi hao, kumuua mmewe kipenzi. Mbaya zaidi mmewe alikuwa hajui mpango mzima uliokuwa umewekwa dhidi yake.

Kwa kuwa alikuwa na taarifa juu ya kufanyika kwa sherehe hizo siku hiyo, alijiandaa mapema Mganga huyo kuhudhuria.

Cha ajabu alipofika eneo hili ndipo alikutana na maajabu, alimkuta mke wake kwenye sherehe hizo za kichawi. Kwa kuwa wachawi wote walikuwa hawamuoni aliendelea na shughuli zake, huku akisubiria kuona kilichokuwa kimemleta mke wake kwenye sherehe hizo.

Katika harakati zake Mganga huyo maeneo hayo ya sherehe akakutana na kibao na mtama, aliyempiga hakumuona hata kidogo ndiyo maana alikimbia.

Wakati hayo yanatokea wachawi wa eneo hilo hawakujua, hata Mganga Hoja hakujua aliyempiga kofi na mtama. Alichokuwa na uhakika nacho ni kumuona mkewe kwenye sherehe hizo pamoja na kupigwa kofi na mtama.

Mtoto THE BOMBOM na kundi lake ndiyo waliharibu shughuli nzima ya Mganga Hoja, kama wasingelimpiga kofi na mtama angefuatilia mwanzo mwisho tukio hilo.

Mtoto huyo na kundi lake waliondoka eneo hilo huku wakishika barabara inayokwenda kwenye ubao wa shule ya Msingi Igoma.

Walipofika eneo hilo walikamata barabara inayoelekea mtaa wa Ndama, waliifuata kwa mguu barabara hiyo mpaka Kwa Mang'ombe.

Pale kuna mwamba mrefu kwenda juu na mpana kwa ukubwa. Barabara inapita karibu sana na mwamba huo, walifika eneo fulani lililokuwa na ngazi za kupanda mlima huo unaojulikana kwa jina la Pasua.

Wakaamua kupanda mlima huo mpaka juu, walipofika kileleni kulikuwa tambarare kunakomuwezesha mtu kuuona vizuri mji wote wa Igoma.

Kwa usiku mji huo ulionekana kung'aa zaidi ya mji wa Yerusalemu, usingeliufananisha na mji wa Galilaya uliopo Israel hata kidogo.

Mji wa Igoma ulikuwa umepambwa kwa majengo ya kifahari kila kona, yalikuwa majengo ya kuvutia yaliyong'ara kwa rangi mbalimbali.

Mandhari ya milima iliongezea uzuri wa mji huo, ni miji michache sana duniani unayoweza kuifananisha na mji huo wa Igoma.

Ulikuwa umejengwa kwenye milima ya mawe yaani miamba, hii ndiyo sababu mji wa Mwanza kwa ujumla huitwa THE ROCK CITY.

Kule kileleni kwenye mwamba huo kuna kisima kilichopasua katikati ya mwamba. Watu wa Igoma hukiita Pasua kwa kuwa kimepasua katikati ya mwamba, ndiyo maana hata mlima wenyewe huitwa Pasua.

Kisima hicho kimepoteza roho za watu wengi, wapo wanafunzi waliofia kisimani humo lakini pia watu wa kawaida. Inasemekana eneo hilo ni makazi ya majini ambayo hunyonya damu za watu, mtoto THE BOMBOM na kundi lake walikisogelea kisima hicho.

Ghafla maji ya kisima hicho yalianza kucheza mithili ya samaki anayecheza mtoni, mara kiumbe wa ajabu alijitokeza nje ya maji akitokea kisimani humo.

Alikuwa ni kiumbe mfano wa binadamu, lakini alikuwa mrefu zaidi ya binadamu. Kichwa chake kilifanana na kile cha binadamu japo chenyewe kilikuwa kikubwa kama cha tikiti maji, alikuwa na jicho moja lililokuwa katikati ya paji la uso wake.

Juu ya kichwa chake alikuwa na pembe mbili zilizokuwa zimejipinda kwa nyuma mithili ya kondoo dume. Masikio yake yalikuwa mapana mithili ya sahani za kulia msibani.

Pua yake kubwa iliyokuwa imechukua eneo lote la uso wake ilimfanya aonekane kuwa mnyama wa kutisha. Kila alipokuwa akipumua cheche za moto zilitoka puami mwake, mdomo wake ulikuwa mpana uliokuwa umepangiliwa meno marefu mithili ya yale ya Simba.

Jitu hilo lilikuwa na ulimi mpana mfano wa upanga, lilikuwa na mikono miwili huku mguu ukiwa mmoja tu. Makalioni lilikuwa na mkia mrefu zaidi ya ule wa ng'ombe, hakika jitu hilo lilitisha. Mguu wake ulikuwa na vidole vinne mithili ya vile vya kuku.

Jitu hilo lilikuwa ni mnyama la kuogofya maana lilikuwa jini si jini, zimwi si zimwi hakika lilitisha. Ghafla lilimsogelea mtoto THE BOMBOM, lilipomkaribia lilipiga magoti mbele yake na kubusu miguu ya mtoto huyo.
Lilikuwa likitokwa machozi ya rangi ya njano mithili ya jezi ya timu ya Wananchi, sauti yake ya kutisha iliyokuwa haieleweki haikumsumbua mtoto huyo.

Mara likaanza kuzungumza Kiswahili fasaha, lilianza kwa salamu ambayo mtoto huyo alikuwa akiifahamu. "Aslamu alekom ya Nabii THE BOMBOM?" Kumbe hata jini huyo alikuwa akimfahamu vyema mtoto huyo.

Mtoto huyo naye aliitikia "Alekoslam ya ustadhi Jini Alfurukum" Jini hilo linatoka kwenye ukoo wa majini yaitwayo Sharif.

Majini hayo ndiyo viongozi wa koo zote za majini unaowafahamu kuanzia, makata, subiani, kisimba na mengineyo yote yapo chini ya koo hiyo.

Liliendelea kuzungumza huku likitoa machozi hayo ya rangi ya njano, lilizungumza Kiswahili fasaha cha lahaja ya Kiunguja. " Ewe Nabii wa bwana, lipi nililokukosea hadi uje uniadhibu kwenye makazi yangu? Tafadhali naomba usinidhuru mimi na ukoo wangu, ikikupendeza turuhusu tukaishi hata mapangoni."Namna lilivyokuwa likijitetea usingeliamini, ama kweli mtoto huyo alikuwa ni nabii aliyeheshimika hata kwa viumbe hao.

Hakusema chochote zaidi ya kuwaomba wale wachawi wenzake kuondoka eneo hilo, wale wachawi wenzake walibaki wanashangaa nguvu alizokuwa nazo mtoto huyo.

Waliachana na jini huyo kisha wakashuka mlima huo, walipofika barabarani hawakupanda bali walitelemuka hadi mtaa wa Ushashini.

Mpa hapo ilikuwa ni saa nane na dakika arobani za usiku, wachawi wa kawaida walikuwa wameanza kurudi majumbani mwao.

Mtaa huo ulikuwa na kundi kubwa la wachawi, ambao walikuwa wamechukua umbo la mbwa. Walikuwa wanabweka mithili ya mbwa, hawakuwa na uwezo wa kuwaona wachawi wa kundi la mtoto THE BOMBOM.

Wachawi hao walikuwa zindiko la mwisho ili kumchukua mtu mmoja mtaa huo. Ndugu msomaji unaposikia mbwa wengi wakilia kwa sauti ya kupokezana, kama sauti zao zitakuwa ziki...

Ndugu msomaji, mambo yanaendelea kupamba moto. Mtoto THE BOMBOM na wachawi wenzake bado wanaendelea na shughuli zao usiku huo ndani ya mji wa Igoma mtaa wa Ushashini. Unadhani nini kitaendelea kwenye simulizi hii ya kutisha? Ungana nami sehemu inayofuata.

WABEJA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news