TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-10: Karibu Kilimanjaro...Kilimanjaro ni njia

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Kilimanjaro ulianzishwa rasmi mwaka 1963 kwa Tangazo la Serikali Na.450 la mwaka huo ukiwa na wilaya za Kilimanjaro na Pare.

Kabla ya Uhuru Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa ni sehemu ya Jimbo la Kaskazini (Nothern Province) lililokuwa linaundwa na wilaya za Arusha na Mbulu, wakati Wilaya ya Pare ilikuwa sehemu ya Jimbo la Tanga (Tanga Province).

Wakati nchi yetu inapata Uhuru tarehe 9 Desemba, 1961 Mkuu wa Jimbo la Kaskazini (Provincial Commissioner ) alikuwa Mheshimiwa PC Edward Barongo ambaye aliongoza hadi 1963 na kufuatiwa na Mheshimiwa Peter Kisumo, Mkuu wa mkoa wa kwanza wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Picha na Kori Safaris.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande ana jambo la kukushirikisha kuhusiana na mkoa huu wenye mema mengi ukiwemo mlima mkubwa zaidi Afrika na duniani. Endelea:

1.Kilimanjaro ni njia,
Si mkoa nakwambia,
Wachaga wametulia,
Wakilima migombani.

2.Wapare nao sikia,
Huko kwao watambia,
Maisha wayapania,
Kipambana maishani.

3.Mlima tunatambia,
Afrika na dunia,
Wengi wanajipandia,
Twala pesa za kigeni.

4.Uwanja wetu wa KIA,
Muhimu kwa Tanzania,
Ndege huko zaingia,
Hata toka Marekani.

5.Watalii kisikia,
Wengi hapa Tanzania,
KIA ndipo washukia,
Kuja vinjari mbugani.

6.Kutoka na kuingia,
Twaitegemea KIA,
Ni karibu kufikia,
Mbuga zetu za thamani

7.Na Kilimanjaro pia,
Mlima unavutia,
Ruksa kujipandia,
Fedha leta kibindoni.

8.Milima waisikia,
Afrika na dunia,
Barafu kujipatia,
Ni ajabu duniani.

9.Ikweta ya Tanzania,
Ni ajabu kusikia,
Barafu twajivunia,
Pale juu mlimani.

10.Kile cha kuangalia,
Mazingira jitunzia,
Mvuto sijeishia,
Kutuweka msambweni.

11.Moto tunaosikia,
Huko unaibukia,
Bora kutafuta njia,
Usitokee angani.

12.Miti tukijitunzia,
Na uoto asilia,
Mlima utasalia,
Kivutio duniani.

13.Hapo twajitangazia,
Kwamba upo Tanzania,
Wale wanatuibia,
Aibu zao usoni.

14.Wachaga wanavutia,
Mengi wanatufanyia,
Kwa biashara huria,
Kweli hawawezekani.

15.Kwa Mangi utasikia,
Kote kote Tanzania,
Ni vile wanapania,
Mkono wende kinywani.

16.Unaweza wafanyia,
Chochote watasikia,
Pesa ukiwaibia,
Timbwili hutoamini.

17.Kwa wasomi Tanzania,
Hawa nao watambia,
Wengi lichangamkia
Elimu toka zamani.

18.Wapi utakopitia,
Siweze wasalimia,
Taifa watumikia,
Hata huko duniani.

19.Sekta kiangalia,
Zile unazijulia,
Hao utajipatia,
Wakiwa bize kazini.

20.Kutegea wasikia,
Kwao huwezi sikia,
Kazi kuchangamkia,
Imewakaa moyoni.

21.Hawa ninakuambia,
Tamaduni meingia,
Bora na wa kuvutia,
Waigwaigwa nchini.

22.Mwaka unapoishia,
Kwao wanakutania,
Yao kuzungumzia,
Na mipango ya mwakani.

23.Jambo zuri nakwambia,
Bora kuigilizia,
Mila wanashikilia,
Siseme hawajuani.

24.Ajenda kuzisikia,
Zile wanajadilia,
Vigumu ninakwambia,
Ila tunazo za ndani.

25.Sote tukifwatilia,
Mazuri kuwaibia,
Pazuri tutafikia,
Hata kwetu vijijini.

26.Ila tukipuuzia,
Tulipo tutasalia,
Tukijisikitikia,
Tugotavyo ukingoni.

27.Nyumba ya Mungu tangia,
Zamani twalitumia,
Samaki kujipatia,
Na umeme gridini.

28.Vema kusisitizia,
Mazingira jilindia,
Tuweze jifaidia,
Mito maziwa nchini.

29.Makabila yasalia,
Kote nakowatajia,
Hao wawakilishia,
Sendi hadi Upareni.

30.Mkoa litupatia,
Cleopa Msuya pia,
Kama hujamsikia,
Kamsome vitabuni.

31.Huyu alishikilia,
Ukuu kwa kurudia,
Nyerere alianzia,
Kwa Mwinyi akashaini.

32.Sokoine naye pia,
Vipindi viwili pia,
Waziri Mkuu pia,
Waliongoza nchini.

33.Sawa Malecela pia,
Makamu Rais pia,
Nchi alitumikia,
Tumshukuru jamani.

34.Hekima inasalia,
Msuya atupatia,
Kwa kweli inaingia,
Kufika hadi moyoni.

35.Sifa yake yasalia,
Ukweli sijasikia,
Uongo kunitajia,
Alikujenga nyumbani.

36.Mwanga waliopitia,
Kwapendeza nasikia,
Ubunge aliutumia,
Kutengeneza nyumbani.

37.Barabara twasikia,
Huko kweli zavutia,
Na hata umeme pia,
Uko tangia zamani.

38.Mfano wake sikia,
Mzuri kufwatilia,
Wabunge wakiingia,
Wajali kule nyumbani.

39.Mambo ya kujikalia,
Mijini twayasikia,
Kwao utawasikia,
Waenda uchaguzini.

40.Msuya watuambia,
Watu liwatumikia,
Hata sasa asalia,
kwao akiwa enzini.

41.Mageuzi Tanzania,
Huyu baba lichangia,
Uchumi changamkia,
Nchi ipae angani.

42.Themanini liingia,
Kiti akakikalia,
Nchi akasimamia,
Tulipotoka vitani.

43.Na tena alichangia,
Wizara kitumikia,
Kipindi kilofwatia,
Nchi kutoka vitani.

44.Na alimsaidia,
Mwinyi kututumikia,
Wakati kimalizia,
Miaka yake mwishoni.

45.Mzee ametulia,
Busara amejazia,
Kama ukimsikia,
Utafaidi amini.

46.Kule Mwanga nakwambia,
Huyu wamfurahia,
Alivyowatumikia,
Alipokuwa bungeni.

47.Bado tunamtumia,
Mengi anatufanyia,
Hekima atumwagia,
Nchi yende kileleni.

48.Huyu anafuatia,
Kofia namvulia,
Sifa ametupatia,
Dunia inabaini.

49.Nafasi kashikilia,
Kubwa sana ya dunia,
Mwanamke nasifia,
Kilimanjaro nyumbani.

50.Kikwete limpatia,
Uwaziri nakwambia,
Ki Moon kumsikia,
Kamtaka ofisini.

51.Asha-Rose katimia,
Aliongoza dunia,
Liipamba Tanzania
Sifa kote duniani.

52.Mnyenyekevu sikia,
Kwa kazi ametimia,
Yake diplomasia,
Dunia likaa chini.

53.New York akakalia,
Ki Moon kusaidia,
Ukatibu wa dunia,
Kwa uongozi makini.

54.Sifa ametupatia,
Migiro nakuambia,
Vile alivyotulia,
Akihimiza amani.

55.Balozi atumikia,
Toka enzi Malkia,
Heri tunamtakia,
Uwakilishi makini.

56.Pakubwa hakufikia,
Wale utawasikia,
Lakini nakuambia,
Lifanya mengi nchini.

57.Jumuiya kumbukia,
Ile lituvunjikia,
Aliwahi shikilia,
Utendaji kileleni.

58.Edwin Mtei njia,
Ile aliipitia,
Soma utafurahia,
Ni maarufu nchini.

59.Huyu alitumikia,
Serikali Tanzania,
Yale aliaminia,
Alishika kama dini.

60.Miaka twakumbukia,
Ile yetu Tanzania,
Wakati kishikilia,
Waziri fedha nchini.

61.Rais kumbishia,
Yale alifikiria,
Uchumi kuinulia,
Mwenyewe lijipiga chini.

62.Wachache ninakwambia,
Kuweza jiamulia,
Kujiuzuru sikia,
Ili watoke kitini.

63.Gia wabadilishia,
Angani ninakwambia,
Wazidi kuzikalia,
Nafasi serikalini.

64.Leo ukimsikia,
Usije kumwaminia,
Kesho tabadilikia,
Kaskazi na kusini.

65.Mtei ninakwambia,
Alifaa Tanzania,
Yale walimbishia,
Kwa sasa yako enzini.

66.Uchumi kusikizia,
Wakubwa kituambia,
Ndiko twasikizia,
Mwendo huo duniani.

67.Vile nimekutajia,
Vema pia kujulia,
Huyu lituanzishia,
Benki Kuu ya nchini.

68.Gavana lishikilia.
Miaka nane sikia,
Hapa ilipofikia,
Kazi yake i kichwani.

69.Kazi lipomalizia,
Siasa hakuachia,
Mwanzilishi nakwambia,
CHADEMA nayosikia.

70.Chama kilivyotishia,
Miaka zama sikia,
Kwa kweli alichangia,
Demokrasia nchini.

71.Sasa kwake atulia,
Hekima kitugawia,
Heri tunamtakia,
Aishipo duniani.

72.Mrema memsikia,
Lyatonga nakutajia,
Maarufu Tanzania,
Wizara ile ya Ndani.

73.Nchi alitumikia,
Yake tukafurahia,
Mapya alitupatia,
Bado yadumu nchini.

74.Yeye alileta njia,
Amani sisitizia,
Polisi kisimamia,
Twamkumbuka nchini.

75.Vituo vidogo pia,
Ndiye aliasisia,
Bado tunavitumia,
Sehemu zote nchini.

76.Juzijuzi kaishia,
Kwao tumemzikia,
Yake twayakumbukia,
Aliyofanya nchini.

77.Reginald Mengi pia,
Moshi ndiko likulia,
Tajiri Mtanzania,
Ni maarufu nchini.

78.Mengi alitufanyia,
Hapa kwetu Tanzania,
Japo ametangulia,
Yanasalia nchini.

79.Vyombo kujimilikia,
Vya habari Tanzania,
Ambavyo tunatambia,
Kwenye kanda na nchini.

80.Viwanda ni vingi pia,
Ajira vyatupatia,
Mengi lijianzishia,
Faida hapa nchini.

81.Mazingira nakwambia,
Sana alifikiria,
Hata mali kutumia,
Kote kuwe na amani.

82.Miti alijipandia,
Kilimanjaro sikia,
NEMC lishikilia.
Kwa muda hapa nchini.

83.Amekwishatangulia,
Maarufu Tanzania,
Bado twamkumbukia,
Livyotufaa nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news