TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-14:Karibu mkoani Mbeya, Karibu The Scotland of Africa

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Mbeya ni moja kati ya mikoa minne iliyopo katika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania.

Mikoa mingine ni Rukwa, Iringa na Ruvuma. Mkoa wa Mbeya ulianzishwa mwaka 1961 na ulikuwa ukijulikana kwa jina la Southern Highland Province kwa kujumuisha baadhi ya maeneo ya mikoa ya Iringa na Rukwa.

Jina la Mbeya limetokana na neno la kisafwa Ibheya ambalo maana yake ni chumvi, kutokana na wafanyabiashara kufika na kubadilishana mazao yao kwa chumvi.

Mji wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927. Wakati huo dhahabu ilianza kupatikana katika milima iliyopo karibu na Mbeya hadi Chunya hivyo Mbeya ulikuwa ni mji wa mapumziko kwa Wazungu kutokana na hali yake nzuri ya hewa.

Picha na Visit Tanzania.

Hali iliyosababisha mji wa Mbeya kupewa jina la utani kama "The Scotland of Africa" baada ya kutambua kama uoto, hali yake ya hewa na muonekano wa milima inayouzunguka mji wa Mbeya kufanana na Scotland mfano uoto unaopatikana katika mlima Loleza.

Mkoa huu ni moja kati ya mikoa mikongwe iliyokuwepo mpaka wa kati wa uhuru mwaka 1961. Katika kipindi hicho, makabila makuu katika Mkoa wa Mbeya yalikuwa ni Wasafwa, Wanyakyusa, Wandali, Wasangu, Wamalila, Wanyiha, Wakimbu na Wanyamwanga. Ambapo jamii hizo ni maarufu kwa kujishughulisha na kilimo na ufugaji mdogomdogo.

Aidha, mkoa huo ambao ni kati ya mikoa 26 ya Tanzania na 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania una eneo la kilomita za mraba 63,617 kati ya hizo kilomita za mraba 61,783 ni za nchi kavu na kilomita za mraba 1,834 ni eneo la maji.

Mkoa wa Mbeya upo Kusini Magharibi mwa eneo la Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Mkoa upo katika Latitudi kati ya 7º na 9º 31’ Kusini ya Ikweta na Longitudo kati ya 32º na 35º Mashariki ya Greenwich.

Pia, mkoa huo unapakana na nchi za Zambia na Malawi upande wa Kusini, Mkoa wa Rukwa upande wa Magharibi, mikoa ya Tabora na Singida kwa upande wa Kaskazini ambapo kwa upande wa Mashariki unapakana na Mkoa wa Iringa.

Mji wa Tunduma katika Wilaya ya Mbozi na Kasumulu katika Wilaya ya Kyela, hufanya milango ya kuingilia na kutokea nchi za Zambia na Malawi.Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, fursa zilizopo mkoani Mbeya ukifanya uamuzi wa kuziendea hautajuta kamwe kuwekeza fedha zako. Endelea;

1. Mbeya nauangazia,
Neema kwa Tanzania,
Baridi ukiingia,
Ni kama vile mtoni.

2. Kyela joto laanzia,
Kama Bongo Tanzania,
Wali wake nasikia,
Mtamu kuliko koni.

3. Nazi utajipatia,
Kokoa tajilimia,
Hawa nawafagilia,
Korosho ziko shambani.

4. Michikichi kisikia,
Mawese wayatumia,
Uchumi wanachangia,
Maendeleo nchini.

5. Wanyakyusa kisikia,
Urembo wanatambia,
Wengi unawakutia,
Mjini na vijijini.

6. Sifa wanajivunia,
Kyela ninakuambia,
Jambo wakishikilia,
Hawayumbi asilani.

7. Wanavyojiaminia,
Kwa kweli wanavutia,
Uamuzi kifikia,
Hawachenji asilani

8. Sifa nyingine tulia,
Nipate kukuambia,
Wenyewe waaminia,
Ndio Wanyaki makini.

9. Wengine ukisikia,
Ni wa kuja nakwambia,
Lugha wanajivunia,
Ni wa mfano nchini.

10. Ziwa Nyasa kisikia,
Kyela ndiko latulia,
Samaki wajipatia,
Na usafiri majini.

11. Mwambao ukipitia,
Utalii nakwambia,
Elimu tajipatia,
Ya hapa hapa nyumbani.

12. Rungwe unapoingia,
Ni baridi ya dunia,
Blanketi zingatia
Hasa Julai na Juni.

13. Kazi wanajifanyia,
Uzalishaji kwa nia,
Njaa wanaisikia,
Vyakula tele shambani.

14. Kutalii takimbia,
Jinsi kunavyovutia,
Maziwa mengi si mia,
Ni maajabu nchini.

15. Ziwa Nyasa wasikia,
Samaki wamejazia,
Wale ukiangalia,
Rangi zavuta machoni.

16. Ziwa ni la Tanzania,
Wenyewe twajivunia,
Wenye ile mbaya nia,
Hawapati asilani.

17. Kisiba, Ngozi tambia,
Maziwa twajivunia,
Jinsi yalivyotulia,
Utadhani uko pwani.

18. Ni vema ukapitia,
Elimu kujipatia,
Na tena kushuhudia,
Ni utalii wa ndani.

19. Ziwa Ngozi watwambia,
Maajabu yazidia,
Maji yalikoanzia,
Hata hayajulikani.

20. Maji chumvi yatulia,
Hujawahi kusikia,
Usije kujaribia,
Kuogelea majini.

21. Mlima Rungwe tabia,
Kama Meru nakwambia,
Mrefu unavutia,
Unao mbega mitini.

22. Waweza kuupandia,
Hata ukafurahia,
Uwanda ukifikia,
Ni baridi kileleni.

23. Miti hujaisikia,
Ile hasa asilia,
Huko ndiko yatulia,
Kwa wanyama maskani.

24. Mbeya wanajisifia,
Vile wajiaminia,
Kama nia wakitia,
Hawaachi asilani.

25. Ndizi mbivu mia mia,
Wauzaji wakwambia,
Waweza kujipatia,
Bei ni ya wastani.

26. Mto Kiwira sikia,
Rungwe ndiko waanzia,
Ziwa Nyasa waishia,
Maporomoko oneni.

27. Daraja melisikia,
La Mungu nasimulia,
KeiKei kipitia,
Utalitia machoni.

28. Mbuga ya Kitulo pia,
Mbeya ndiko yaanzia,
Bustani ya dunia,
Ni burudani moyoni.

29. Tembelea angalia,
Utajiri shangilia,
Sifanye kuwaachia,
Watoka ughaibuni.

30. Kwa kilimo shangilia,
Mahindi mpunga pia,
Usangu bonde sikia,
Rutuba limesheheni.

31. Mikoa twaisifia,
Iringa na Mbeya pia,
Mingine ntawatajia,
Yote tunayo nchini.

32. Chakula wazalishia,
Taifa linatumia,
Wenyewe wajipatia,
Pesa zao mfukoni.

33. Ukarimu nakwambia,
Mbeya vulia kofia,
Kwao ukikaribia,
Tajishibia tumboni.

34. Ila ukiwatania,
Hawana kuvumilia,
Waweza kushambulia,
Kukawa na tafrani.

35. Watu wengi mesikia,
Mbeya walikoanzia,
Mmoja nawatajia,
Ni maarufu nchini.

36. Ni huyu Dada Tulia,
Mzamivu nakwambia,
Cheo anashikilia,
Kikubwa hapa nchini.

37. Kazi amsaidia,
Spika ninakwambia,
Kiti amekijulia,
Hekima nyingi kichwani.

38. Chipsi mnatambia,
Kote ninakopitia,
Wanaowazalishia,
Mbeya hasa ni nyumbani.

39. Uporoto kisikia,
Kilimo kimezidia,
Nchi waisambazia,
Nyumbani na hotelini.

40. Kahawa na chai pia,
Nayo wajizalishia,
Parachichi sasa pia,
Ni zao liko shambani.

41. Mboga sijakutajia,
Nyanya vitunguu pia,
Mazao mengi sikia,
Mbeya huko ni nyumbani.

42. Makaa ya mawe pia,
Mbeya utajichimbia,
Kyejo gesi asilia,
Rasilimali nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news