TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-19: Karibu mkoani Pwani, Una mengi yenye shani

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, kabla ya Uhuru Mkoa wa Pwani ulikuwa sehemu ya Jimbo la Mashariki ambako makao makuu yake yalikuwa Morogoro.

Aidha, baada ya Uhuru mwaka 1961 Serikali ilianzisha mfumo wa mikoa. Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa mikoa, mkoa wa sasa wa Dar es Salaam ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Pwani na makao yake makuu yalikuwa Dar es Salaam.

Mwaka 1972 serikali ya Tanzania ilifanya mabadiliko ya kiutawala ambayo yalisababisha kuanzishwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mkoa wa Pwani ulizinduliwa rasmi mwaka 1972 na kubaki na wilaya nne ambazo ni Kisarawe, Rufiji, Bagamoyo na Mafia na makao makuu yake yalikuwa Kibaha.

Pamoja na mabadiliko hayo, robo ya makao makuu ya mkoa wa Pwani ilibaki Dar es Salaam hadi 1979. Mkoa ulibaki na wilaya nne hadi 1979 ilipoundwa Wilaya ya Kibaha kutoka Kaskazini mwa Wilaya ya Kisarawe na Kusini mwa Wilaya ya Bagamoyo.

Julai 1995, Wilaya ya Mkuranga iliundwa kutoka Pwani ya Mashariki ya Wilaya ya Kisarawe ikaongoza Mkoa wa Pwani kuwa na wilaya sita hadi sasa. Pwani ni kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara na kati ya mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema ukifika mkoani Pwani kuna mambo mengi ya kuvutia, kujifunza na kuwekeza kwa ustawi bora wa uchumi. Endelea;

1. Pwani yetu naingia,
Ni kando ya baharini.
Huu tunajivunia,
Mkoa wetu wa Pwani.

2. Ni kama unafifia,
Dasalamu yatishia,
Lakini nausifia,
Una mengi yenye shani.

3. Kiti ningekikalia,
Hili kulijadilia,
Jina ningewafutia,
Lingine nije wapeni.

4. Pwani hiyo nakwambia,
Tanga, Lindi pwani pia,
Dar ya mabaharia,
Hata Mtwara ni pwani.

5. Jina ningeupatia,
Mkoa ungevutia,
Sote tungeangalia,
Liingie akilini.

6. Bagamoyo twasifia,
Ruvu tunajivunia,
Rufiji nakutajia,
Majina yana thamani.

7. Kibaha, Chalinze pia,
Majina yanavutia,
Mlandizi na Mafia,
Mojawapo ngeshaini.

8. Bagamoyo kisikia,
Ni Pwani ninakwambia,
Hapo tunajivunia,
Ya kale Mlingotini.

9. Huko utajipatia,
Mambo ya historia,
Dini na magofu pia,
Yapatikana nchini.

10. Utalii yachangia,
Hapa kwetu Tanzania,
Jaribu kupafikia,
Hutojuta asilani.

11. Ukanda bahari pia,
Samaki twajipatia,
Bagamoyo twasifia,
Samaki wa baharini.

12. Maji Dar twatumia,
Pwani ndiko yaanzia,
Mto Ruvu natajia,
Wakata kiu mwilini.

13. Kibaha yajichimbia,
Mji mkuu sikia,
Pwani tukikutajia,
Hapo ndio ofisini.

14. Viwanda vya Tanzania,
Pwani ndiko vyatulia,
Ni vingi kukutajia,
Vimejaa kama nini.

15. Kote ukiangalia,
Majengo yanavutia,
Bidhaa vyazalishia,
Twauza nje na ndani.

16. Umeme twasubiria,
Mkoa Pwani sikia,
Maji yatiririkia,
Umeme uko njiani.

17. Mbuga ya ajabu pia,
Kando Bahari India,
Maajabu ya dunia,
Hiyo mbuga Saadani.

18. Wanyama wa kuvutia,
Bahari wachungulia,
Kama ukiifikia,
Tawaona ufukweni.

19. Kuna kisiwa Mafia,
Kuzuri kunavutia,
Unaweza kufikia,
Boti na ndege angani.

20. Samaki hujasikia,
Hata kuwafahamia,
Waweza ona Mafia,
Huko Mkoani Pwani.

21. Korosho na nazi pia,
Watu wanajilimia,
Kipato wajipatia,
Watoto wenda shuleni.

22. Mwishoni namalizia,
Pwani ichotuzalia,
Kwa kweli twajivunia,
Kikwete mwana wa Pwani.

23. Rais wa Tanzania,
Aliyetutumikia,
Muda ulipotimia,
Yu Msoga kijijini.

24. Jakaya nikianzia,
Mtu wa watu sikia,
Hata ukimsikia,
Bashasha tele usoni.

25. Kule alikoanzia,
Siasa nitakwambia,
Mke alijipatia,
Anomfaa mekoni.

26. Ukada alizidia,
Chuo akimalizia,
Muda mwingi katumia,
Siasa ziwe kichwani.

27. Bagamoyo wakwambia,
Mkwere wamjulia,
Maafa yakiwajia,
Mwepesi kwenda kuhani.

28. Hiyo kwake ni tabia,
Toka alikoanzia,
Wengi wanashuhudia,
Tangu enzi za zamani.

29. Msiba ulitukia,
Wa Bagamoyo sikia,
Yeye hakuhudhuria,
Kwa sababu za kikazi.

30. Kile aliwafanyia,
Ujumbe liwatumia,
Nami nilishuhudia,
Mjumbe yu kikaoni.

31. Rais wa Tanzania,
Ambaye twajivunia,
Alivyotutumikia,
Kama mwenzetu nyumbani.

32. Wengine kufanania,
Siwezi thibitishia,
Rahisi kumfikia,
Tajiri na maskini.

33. Kwake tunajivunia,
Mengi alitufanyia,
Mkapa lipoishia,
Kaendeleza makini.

34. Miundombinu sawia,
Ambayo twajivunia,
Yeye alisimamia,
Usafiri burudani.

35. Temino ya tatu pia,
Hapa tunajivunia,
Mradi ulianzia,
Pale twapaa angani.

36. Barabara nyingi pia,
Daraja Nyerere pia,
Alituidhinishia,
Twapita kiulaini.

37. Uhuru kujisifia,
Hata mambo ya udhia,
Kwake ilituzidia,
Ukweli naubaini.

38. Redio za Tanzania,
Na televisheni pia,
Ni nyingi zilianzia,
Akiwa yu Magogoni.

39. Sasa hivi twasifia,
Vyombo vingi Tanzania,
Pia tunazisikia,
Redio za mikoani.

40. Mengi tunayotambia,
Yeye ametupatia,
Mishemishe kumbukia,
Zilishamiri mijini.

41. Wote waliotulia,
Yao walijifanyia,
Pesa kujikusanyia,
Wanalia kivulini,

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news