Tanzania yaungana na Afrika Kusini kuadhimisha siku ya Taifa hilo

NA ELEUTERI MANGI
Afrika Kusini

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeungana na Afrika Kusini kuadhimisha Siku ya Afrika Mei 25, 2023 manispaa ya Mogala nchini Afrika Kusini kusherehekea miaka 60 ya Umoja wa Afrika tangu kuanzishwa kwake Mei 25, 1963 Addis Ababa Ethiopia.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema Siku ya Afrika ni siku muhimu ya kuwakumbuka viongozi walitoa mchango mkubwa wa kuzikomboa nchi za Afrika na jinsi walivyojitolea kuhakikisha Afrika inasonga mbele na kufika hapo ilipo na zaidi.

“Kwa wenzetu Afrika Kusini wanaipa umuhimu mkubwa sana siku hii, Rais mwenyewe wa nchi Rais Cyril Ramaphosa alikuwepo hapa na kuwaongoza watu wote kwenye maadhimisho haya,” amesema Balozi Milanzi.
Kwa kuonesha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini, Balozi Milanzi amesema Tanzania imeshiriki katika sherehe hizo kwa kutuma ujumbe kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu pamoja na kikundi cha Sanaa cha Safi ambacho kimetia fora kwa kutumbuiza hatua ambayo imepelekea kupewa nafasi kwenda kutumbuiza wakati wa sherehe ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Afrika Kusini Mei 27, 2023.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema siku hiyo ni adhimu kwa Afrika nzima, Watanzania wanawajibu wa kujivuania kuwa nchi yao ni miongoni mwa nchi waasisi wa umoja huo ambapo Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ni miongoni mwa Viongozi waanzilishi wa Umoja huo na kuongeza kuwa ujumbe anaouongoza yupo pia Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Fatma Hamad Rajab.
Akihutubia mamia ya wananchi wa Afrika Kusini pamoja na mabalozi wanawakilisha nchi zao nchini humo, Rais Cyril Ramaphosa amesema waafrika wanajivuvia historia yao na kujipanga kutengeneza kesho ya Waafrika wenyewe licha ya changamoto mbalimbali zinazokumba nchi za Afrika ambazo nyingi zinatatuliwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizo kwa njia ya kutoa wataalamu, ujuzi na kusisitiza kuwa Afrika ina wataalamu bora duniani wenye ujuzi katika fani mbalimbali.
Siku ya Afrika imesherehekewa Afrika Kusini kwa kupambwa na bendera zote za nchi 54 za Afrika na kuhudhuriwa na mabalozi wa nchi 14 pamoja na viongozi mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news