TANZANIA,BORA KUISHANGILIA-8: Katavi naingia,Chakula wamejazia

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Katavi una ukubwa wa kilomita za mraba 47,527 na ulitangazwa rasmi Marchi Mosi, 2012 kwa uamuzi wa Serikali wa kuanzisha mikoa minne mipya ambayo ni Katavi yenyewe, Njombe, Simiyu na Geita.

Lengo la kufanya hivyo ni kusogeza huduma za kiutawala na kiuchumi kwa wananchi wake na ulizinduliwa rasmi Novemba 25,2012 na Mheshimiwa Gharib Bilal, Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkoa upo Magharibi mwa Tanzania kati ya Latitude 40 na 80 Kusini mwa msitari wa Ikweta na Longitude 300 hadi 330 Mashariki mwa msitari wa Greenwich.

Aidha,Kaskazini unapakana na Wilaya za Urambo na Kaliua (Tabora), Mashariki unapakana na Wilaya ya Sikonge (Tabora),Kaskazini Mashariki unapakana na Wilaya ya Chunya (Mbeya) na Kusini unapakana na Wilaya ya Nkansi (Rukwa).

Pia,Kusini Mashariki unapakana na Wilaya ya Sumbawanga (Rukwa),Magharibi unapakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo huku Kaskazini Magharibi ukipakana na Mkoa wa Kigoma.

Mkoa upo kati ya wastani wa mita 1000 hadi 2500 kutoka usawa wa bahari. Hali ya joto ni kati ya nyuzi 130c na 160c miezi ya Juni na Julai na nyuzi 260c hadi 300c miezi ya Septemba hadi Novemba.

Kwa wastani, Katavi hupata mvua kati ya mm 700 hadi mm 1300 zinazonyesha kati ya Novemba na Aprili. Mkoa umegawanyika katika kanda nne za hali ya hewa ambazo ni ukanda wa bonde la Ziwa Rukwa, Nyanda za uoto wa miombo ya Katumba-Inyonga, Miinuko ya Mwese na Mwambao wa Ziwa Tanganyika. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema Mkoa wa Katavi una mengi ya kujifunza na muhimu kwa Taifa letu. Endelea;


1.Katavi ninaingia,
Mkoa kukutajia,
Watuwe wametulia,
Kwa majembe mashambani.

2.Njaa wanaisikia,
Chakula wamejazia,
Na kilichowazidia,
Wanapeleka Handeni.

3.Mahindi kitaka pia,
Mchele wajilimia,
Samaki wanajilia,
Kwa kuwa wako ziwani.

4.Hapa nakusimulia,
Maajabu ya dunia,
Wanyama wamejazia,
Huko Katavi mbugani.

5.Mbuga ya taifa pia,
Hapa kwetu Tanzania,
Wachache wanafikia,
Watalii nje ndani.

6.Kitu utafurahia,
Ni ule uasilia,
Mandhari ya kuvutia,
Unapokuwa mbugani.

7.Vile wanatuambia,
Nyati walivyojazia,
Ni ya kwanza kwa dunia,
Kwa jinsi walivyo ndani.

8.Kama umeisikia,
Hiyo mbuga nakwambia,
Bora ukaifikia,
Uingie hadi ndani.

9.Waziri Mkuu pia,
Yule tulimsikia,
Huko ndiko lianzia,
Kuingia duniani.

10.Pinda ninakutajia,
Liongoza Tanzania,
Yake tunakumbukia,
Juzijuzi si zamani.

11.Mpole kimsikia,
Nondo akikushushia,
Makini kufwatilia,
Alipokuwa kazini.

12.Vema alisimamia,
Kazi zilizomjia,
TAMISEMI kumbukia,
Livuma sana nchini.

13.Vile aliwazukia,
Wale waliovilia,
Waweza kusimulia,
Jinsi aliwabaini.

14.Waziri Mkuu pia,
Kazi kuzisimamia,
Mengi alitufanyia,
Yakukumbukwa nchini.

15.Kweli limsaidia,
Kikwete ninakwambia,
Vile alimjibia,
Maswali kule Bungeni.

16.Kuna siku alilia,
Akiwasikitikia,
Walioaga dunia,
Matendo ya kishetani.

17.Walivyotuchafulia,
Sifa njema Tanzania,
Ndugu zetu kuvamia,
Sababu ni albini.

18.Vita alisimamia,
Kusaka maharamia,
Sote tukafurahia,
Walivyotiwa mbaroni.

19.Ila twasikitikia,
Wauaji kutimia,
Hatua zinasalia,
Kuwatia hatiani.

20.Haki zingine sikia,
Kutetea nakwambia,
Unaweza kuumia,
Kufika hadi moyoni.

21.Mtu unajiulia,
Tena kwa kukusudia,
Kunyongwa wanatwambia,
Ni adhabu yenye soni.

22.Ndivyo ninavyosikia,
Ndugu walotuulia,
Adhabu liwapatia,
Bado wadunda hewani.

23.Baba Pinda alilia,
Albino kulilia,
Wauaji kusalia,
Haingii akilini.

24.Mizengo Pinda sikia,
Sisi tunakusifia,
Kazi ulitufanyia,
Kula raha uzeeni.

25.Mnyenyekevu sawia,
Na upendo kuzidia,
Busara yako sikia,
Inatufaa nchini.

26.Dodoma ametulia,
Mashamba ajilimia,
Ukitaka jifunzia,
Mtembelee shambani.

27.Miembe mingi sikia,
Na nyuki ajifugia,
Asali atuuzia,
Afya njema twasheheni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news