Waziri Lela aguswa na programu za kimkakati Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)

NA MWANDISHI WETU 

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe.Lela Mohamed Mussa amekipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kufanikiwa kuwa na programu kadhaa za kimkakati.
Mheshimiwa Lela ametoa pongezi hizo leo Mei 20, 2023 alipotembelea banda la maonesho la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) katika maonesho ya pili ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
“Mipango ya serikali ni kwenda kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, tukipata walimu wenye sifa stahiki katika nyanja hizo maana yake tutafikia malengo kwa wepesi zaidi, niwapongeze kwa uamuzi wenu wa kuziweka hizi programu kuwa za kimkakati ili ziweze kuwafikia wahitaji wengi zaidi,”amesema Mheshimiwa Lela.
Aidha, amepongeza uwepo wa mfumo wa kutoa elimu kwa njia ya mtandao kwani umeonekana kuwa unaweza kuhudumia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja bila kuathiri shughuli zao za utafutaji maisha. 
Mheshimiwa Lela ametoa rai kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kushirikiana na taasisi nyingine za kielimu ili kozi za taaluma mbalimbali zipatikane katika mfumo wa kimtandao wa chuo hiki.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Huduma za Kitaalam, Prof. Deus Ngaruko, ametembelea maonesho haya na kusema kuwa chuo kinafanya marekebisho makubwa ya mitaala yote na kuanzisha mingine mipya ili kuendana na uhitaji wa elimu wa sasa.
“Tunafanya mapitio ya mitaala yote iliyokuwa imekwisha muda pamoja na ile ambayo ilikuwa bado ili kuifanya iendane na sera ya taifa ya elimu kwa sasa, tunapokwenda kuanzisha kituo kikubwa cha utafiti, gunduzi, ubunifu na ukarimu tunataka kuifanya sayansi na ubunifu kuwa vivutio vya utalii nchini,”amesema Prof. Ngaruko.
Aliendelea kusema kuwa kituo cha utafiti, ugunduzi, ubunifu na ukarimu kitajegwa mjini Kibaha katika eneo la Bungo ambapo kitakuwa na mambo mengi ya kuvutia ikiwamo mashamba darasa, kiwanda cha uchapaji, mabwawa ya kusafisha majitaka, kufuga samaki na mifumo ya umwagiliaji, ufugaji wanyama na nyuki lakini pia viwanja vya michezo na nyumba za kitalii za kupumzika.
Ili kuendana na sera ya elimu nchini, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kimeweka progamu za stashahada ya Ualimu wa shule za msingi (DPTE), kozi ya maendeleo kwa vijana (CYP), programu ya ujasiriamali na stashada ya juu ya ualimu wa ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (PGD-TVTE) kuwa ni program za kimkakati kufanikisha sera inayojikita katika mitaala ya ujuzi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news