Dkt.Jafo aweka wazi mipango ya Serikali kuhusu mazingira

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania imeendelea kuweka mikakati na sera endelevu za uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ikiwemo kuhamasisha zoezi la upandaji miti ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira mabadiliko ya tabianchi. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akifanya usafi wa mazingira katika eneo la Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege iliyopo Manispaa ya Dodoma wakati wa uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani leo Juni Mosi, 2023.

Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo (Juni Mosi, 2023) Jijini Dodoma, Dkt. Jafo amesema katika kipindi cha mitatu ajenda ya mazingira ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vinavyoendelea kupewa msukumo na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo uhamasishaji wa kampeni za usafi wa mazingira na upandaji miti. 

Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema katika siku za hivi karibuni,Tanzania imeshuhudia athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ambazo ziliathiri sekta mbalimbali za uchumi na uzalishaji mali na kushuhudiwa kuongezeka kwa bei za bidhaa za mazao ya chakula hali iliyotokana na na ongezeko kubwa la ukame katika maeneo mbalimbali ya nchi. 

Sote ni mashahidi kuwa hivi karibuni tumeshuhudia mvua zisizo na wastani mzuri zikinyesha katika baadhi ya maeneo ambazo zilileta athari ikiwemo vifo. Pia tumeshuhudia ukame mkali katika Wilaya za Simanjiro, Longido na Kiteto hali iliyosababisha vifo vingi vya wanyama na kusababisha hali ya umaskini wa kipato kwa wafugaji,” amesema Dkt. Jafo. 
Akifafanua zaidi Waziri Jafo amebainisha kuwa pia baadhi ya maeneo yaliyopo katika visiwa vya Nungwi pamoja na baadhi ya sehemu za kisiwa cha Pemba, Zanzibar pia zimeanza kushuhudia ongezeko kubwa la wingi wa maji ya bahari katika makazi ya wananchi hatua inayotokana na kuyeyuka kwa barafu na kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari. 

Waziri Jafo kutokana na hali hiyo, Serikali imeanisha mikakati, sera na vipaumbele mbalimbali vinavyolenga katika kuhamasisha uhifadhi na utunzanji wa mazingira ikiwemo kuanzia kampeni za upandaji miti, kutokana na ukweli kuwa hakuna mbadala wa mazingira katika mustakabali wa maisha ya binadamu na viumbe hai. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo akipanda mti katika Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege iliyopo Manispaa ya Dodoma wakati wa uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani leo Juni Mosi, 2023. Anayeshuhudia katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

Waziri Jafo amesema kila mwanadamu anahitaji mazingira safi na salama, hivyo kutokana na umuhimu huo katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani mwaka 2023, Serikali imekuja na ajenda mahsusi kwa wananchi kwa kupanda miti na usafi wa mazingira katika maeneo nchini. 

Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Serikali pia imetoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha vibali vya ujenzi vinavyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya wananchi vinaelekeza wajibu wa mwananchi kupanda idadi ya miti katika eneo husika ili kulinda mazingira. 

“Takribani miti Milioni 276 itapandwa kila mwaka, na hili ni lengo la kila Halmashauri kupanda miti Milioni 1.5 kila mwaka, kwa hapa Dodoma lengo ni kupanda Miti Milioni 40 ambalo ni lengo la kipekee ukilinganisha na Mikoa na Wilaya nyingine nchini. Tunazishukuru Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kusimamia vyema kampeni hizi,” amesema Dkt. Jafo. 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kuipatia ushirikiano ofisi yake kwa kuendelea kutoa msukumo na hamasa ya uhifadhi wa utunzaji wa mazingira kupitia Mpango Mkakati wa Mazingira ambapo Mkoa wa Dodoma umetajwa kama Mkoa pekee uliowekewa shahada ya uhifadhi wa mazingira. 

Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mchakato maalum wa kampeni ya Dodoma ya kijani, miti yote mikubwa iliyopo sasa ilitokana na juhudi zake wakati akiwa Makamu wa Rais. Tutahakikisha maelekezo yote yatakayotolewa tupo tayari kuyatekeleza” amesema Mhe. Senyamule. 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule wakifanya usafi wa mazingira katika eneo la Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege iliyopo Manispaa ya Dodoma wakati wa uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani leo Juni Mosi, 2023. Anayeshuhudia katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo.

Aidha Senyamule amesema Ofisi yake pia imeweka mikakati madhubuti ya kulinda vyanzo vya maji ikiwemo Bonde la Mzakwe ambapo eneo hilo kwa sasa limepandwa miti ya kutosha iliyostawi kutokana na hamasa kubwa iliyopo katika kutunza mazingira ya eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news