Leo hatujaja kikazi, tumekuja kutoa elimu kuhusu dawa za kulevya ila tutarudi timu kubwa...

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Aretas Lyimo amewapa elimu wanavijiji wa Kisimiri Juu kuhusu umuhimu wa kuachana na kilimo cha bangi na kujihusisha na mazao mbadala kwa ustawi bora wa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Elimu hiyo ameitoa Juni 21, 2023 baada ya kufika kijijini huko zikiwa ni siku chache zimepita ambazo Watanzania walishuhudia mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiteketeza maelfu ya tani za bangi na mashamba ya baadhi ya wanavijiji ambao wamekuwa wakijihusisha na kilimo hicho haramu wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.

"Nimekuja kuwapa neno la heri, neno la busara ili sisi sote sasa tuweze kwenda na mwenendo wa Serikali wa kutii sheria bila shuruti kuhakikisha kwamba katika maeneo yetu yote hakuna zao la bangi linalolimwa tena katika maeneo yetu, mwanzoni tulipokuja kwenye operesheni, zile siku nane tulikuja kikazi, tulikuja kioperesheni si ndiyo na watu mkahama kwenye nyumba zenu.

"Lakini, ninafurahi leo tupo wote hapa, hakuna aliyehama kwenye nyumba kwa sababu tumekuja kwa amani, tumekuja kuwapa elimu ili sote tuweze kujua tatizo la dawa za kulevya, madhara ya dawa za kulevya, madhara ya kulima bangi, madhara ya kuvuta bangi.

"Ili tuhakikishe tunajenga kizazi cha kesho, kizazi cha wachapakazi, kizazi cha wazalishaji, kizazi ambacho kitajenga uchumi wa nchi, kwa sababu kwenye maeneo yetu haya athari ya bangi inaharibu zaidi vijana.

"Athari kubwa inapoingia kwa vijana, wanashindwa kuzalisha wanaposhindwa kuzalisha, nchi haiwezi kuendelea kiuchumi kwa sababu, vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi ndiyo inayoharibiwa na bangi,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Juni 19, 2023 jijini Dar es Salaam Kamishna Jenerali Aretas Lyimo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imeendelea kufanya jitihada kubwa za kudhibiti dawa za kulevya nchini.

Alisema, kupitia operesheni walizofanya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha walifanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 200.5, bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5,465, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5.

Nyingine ni methamphetamine gramu 531.43,heroin kete 3,878, cocaine kete 138, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza ekari 1,093 za mashamba ya bangi.

Aidha, kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB), mamlaka imezuia kuingia nchini jumla ya kilogramu 1,507.46 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya.

Mbali na hayo, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo ameendelea kuwaeleza wanajiji hao wa Kisimiri Juu kuwa, "Kwa hiyo tumekuja, wazazi wangu, ndugu zangu, vijana wenzagu tuhakikishe sasa tunapiga vita zao la bangi na tulime mazao mengine mbadala ambayo yatatusaidia kukuza uchumi wa nchi yetu.

"Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inataka kila mwananchi ahakikishe kwamba anapiga vita dawa za kulevya ili nchi iweze kupata maendeleo.

"Kwa hiyo, leo mtapata elimu na tutawagawia pia vipeperushi hivi ambavyo vinaonesha madhara ya bangi na haya madhara najua kina mama mumeona pia kwenye clip wamesema pia watoto wao wamepata madhara ya bangi, ndiyo maana hawawasikilizi wazazi wao, wanazurura hawazalishi, lakini pia wamekuwa na viburi vilivyopitiliza, lakini wengine pia wamejiingiza kwenye uhalifu kutokana na athari wanazozitumia kutoka bangi wanazozitumia.

"Kwa hiyo, tutawapa vipeperushi hivi na vitawasaidia ili msome muweze kuona yale ambayo mnayapata mkidhani labda mtoto ni tabia yake kumbe imesababishwa na bangi ili sasa sisi sote, wazazi, vijana na jamii kwa ujumla, lakini pia na viongozi wa Serikali waliopo kwenye maeneo yenu wahakikishe sasa tunaendelea kuhakikisha tunafyeka bangi yote iliyopo.

"Baada ya muda kama wazee wa kimilia walivyotuambia, baada ya mwezi mmoja tutarudi ili kuhakikisha tunakagua mashamba yote ili kuhakikisha kwamba hakuna shamba ambalo litakuwa na bangi kwa lile shamba ambalo litakuwa na bangi, kwa hiyo wale wahusika ambao watakuwa na yale mashamba tutaendelea kuwakamata ili sheria iendelee kuchukua mkondo wake.

"Lakini, kwa wale wote ambao watafyeka bangi yao na shamba halitakuwa na bangi kama mlivyoahidi tunahakikisha kwamba tunawapa mbegu mbadala, Wizara ya Kilimo itakuja kuwapa elimu, lakini mtalima mazao ambayo yatawasaidia kukuza uchumi.

"Lakini pia kukuza uchumi wa nchi, kwa hiyo tuwaombe wote tuweze kuwa marafiki wa Serikali kwa kutii maelekezo ya Serikali, ili maeneo yetu sasa yasiwe na kilimo cha bangi si ndiyo (ndiyoooo...ooo), kwa hiyo tukija mwezi mmoja hatutakuta hata zao moja la bangi, si ndiyo (ndiyoooo...ooo).

"Kwa hiyo tutakuja timu kubwa, ambayo tutaenda vijiji vyote, Lesinoni, Kisimiri Juu, Kisimiri Chini, Monduli yote, kote maeneo yote tutakagua mashamba yote ili kuhakikisha sasa bangi imeisha na elimu itaendelea kutolewa kwenu ili kuhakikisha kwamba sisi tunakuza kizazi cha kuisaidia Serikali, lakini kizazi cha kesho cha kuijenga nchi yetu,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo wakati akitoa elimu kwa wanavijiji wa Kisimiri wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha kuhusiana na madhara ya kilimo cha bangi na matumizi yake kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Amebainisha kuwa, Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani.

Maadhimisho

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amewaalika wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kushiriki katika maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya ambayo yataanza Juni 23 na kilele chake ni Juni 25, 2023.

Amesema, katika maadhimisho hayo ambayo yatafanyika jijini Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mgeni rasmi siku ya kilele atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Tuzingatie Utu na Kuboresha Huduma za Kinga na Tiba.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news