Mtoto ashambuliwa na chui

NA YEREMIAS NGERANGERA

MTOTO Bashiru Issa Matola (10) wa Kijiji cha Nambecha wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma ameshambuliwa na chui usiku wa kuamkia Juni 13, mwaka huu akiwa shambani kwao Mtimbira.

Mtendaji wa Kijiji cha Nambecha, Petro Nyoni amekiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa baadhi ya familia kijijini hapo zinaishi mashambani nyakati hizi za mavuno,hivyo mtoto huyo alitoka nje ya kibanda kwa lengo la kujisaidia na kukutana na chui ambaye naye alikuwa akipita eneo hilo na kumrukia mtoto huyo.

Nyoni amesema, mtoto Bashiru huyo alipiga kelele na watu kujitokeza kwa wingi usiku huo na kumfanya chui akimbie kuingia msituni huku akimwachia mtoto huyo majeraha makubwa kwenye kichwa chake.

Afisa huyo amedai kuwa,ofisi yake ilipata taarifa juu ya tukio hilo na kutoa taarifa ofisi ya maliasili wilaya ya Namtumbo pamoja na kumkimbiza mtoto huyo Hospitali ya Wilaya Namtumbo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mtendaji wa kijiji huyo, mtoto Bashiru alipatiwa matibabu ya majeraha yake na hali yake kwa sasa inaendelea vizuri huku akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo.

Ofisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Prisca Msuha pamoja na kukiri kuwepo kwa tukio hilo amesema walipata taarifa hiyo na kisha kwenda kumuona kijana Bashiru hospitali kwa kutoa kiasi cha fedha ya pole,lakini pia kumjazia fomu ili aweze kupata fedha ya kifuta jasho.

Msuha ameongeza kuwa, askari wa wanyamapori kutoka katika ofisi yake wapo tayari katika eneo la Mtimbila na silaha kwa ajili ya kumsaka chui huyo ili asilete madhara mengine kwa wananchi.

Diwani wa Kata ya Mgombasi, Mrisho Mbawala amedai kata yake imepakana na msitu wa hifadhi wa wanyamapori wa Mwalimu Nyerere, hivyo matukio ya wanyama kuja katika makazi ya watu ni ya mara kwa mara hasa tembo, lakini akaishukuru serikali kwa kuongeza nguvu ya ulinzi kwa wanyama hao kuingia kwenye makazi ya watu kwa kuongeza askari wa wanyamapori wa vijiji na kusaidiwa na askari wa TANAPA.

Aidha, mtoto Bashiru anaendelea kubaki katika uangalizi wa madaktari Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo mpaka hapo hali ya majeraha aliyonayo yatakapodhihirika kupona na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news