Ni bajeti ya maendeleo 2023/24

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imependekeza mapato na matumizi ya shilingi trilioni 44.39 kama bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.38 sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.

Aidha, kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 26.73 na mapato yasiyo ya kodi kutoka wizara,idara,taasisi na mamlaka za serikali za mitaa yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.66.

Mbali na hayo Dkt.Mwigulu wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni jijini Dodoma Juni 15, 2023 amewataka watendaji wa Serikali kutosita kuwachukulia hatua wanaofuja fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.

Amewataka pia wafuatilie na wasimamie kikamilifu fedha na miradi inayotokana na fedha hizo badala ya kusubiri mambo hayo yafanywe na mbio za Mwenge wa Uhuru, ziara za viongozi wa kitaifa na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Waziri Dkt.Mwigulu amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia inapeleka fedha nyingi wizarani, mikoani na wilayani kuliko kipindi chochote katika historia ya Tanzania

“Kwa mujibu wa muundo wa utawala katika nchi yetu, kila ngazi ina uongozi kamili wa Serikali, tunao wa kupanga, wa kufanya malipo, wa kukagua, wa kutathmini, wa kuchunguza, wa kukamata, wa kupeleleza, tunayo magereza ya kuwaweka wahalifu na tunao wa kuhukumu.

“Kwa nini tunasubiri mbio za mwenge, ziara za viongozi wa kitaifa au taarifa ya CAG na kila siku tunaishi huko inakotekelezwa miradi. Viongozi wa Serikali tusijidogoshe, tumepewa mamlaka,”amesema Waziri Mwigulu.

Ardhi

Pia, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amewataka watendaji wa Serikali kutoa fursa kwa wamiliki wa ardhi kunufaika na maeneo wanayomiliki pale wawekezaji wanapohitaji ardhi kwa ajili ya kuwekeza nchini.

Waziri Dkt.Mwigulu amesema, maono ya Rais Dkt.Samia ni kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, hivyo ni lazima watendaji wote serikalini wawe na nidhamu ya kuilea na kuiwezesha sekta binafsi kukua na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi badala ya kufanya urasimu na kuwadhibiti.

“Tunatumia nguvu kubwa kwenye kudhibiti kuliko nguvu tunayoitumia kuwezesha. Lazima tuheshimu sekta binafsi na kutambua mchango wake katika kutoa ajira, kuondoa umaskini na kukuza uchumi. Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu tuwe na nidhamu katika kuiwezesha sekta binafsi kukua.

“Hali ilivyo sasa, wawekezaji wa ndani wakijaribu kupiga hatua wanapigwa vita na kukatishwa tamaa. Hata wamiliki wa ardhi hawapati fidia stahiki pale wawekezaji wanapohitaji kumilikishwa ardhi hizo.

"Kana kwamba watanzania hawatakiwi kutajirika. Nitoe rai kwa watendaji wa Serikali, acheni Watanzania walipwe pesa nyingi, acheni Watanzania watajirike,"amesisitiza Waziri Dkt.Mwigulu.

Pia amesema,licha ya wawekezaji kuleta mtaji, teknolojia, ajira, kuongeza mapato kwa Serikali na kukuza uchumi, uzoefu unaonesha kuwa, wawekezaji hao wanakumbana na vikwazo kuliko uwezeshaji ndani ya Serikali na hata kwa wananchi.

“Jawabu la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuondoa umaskini kwa Watanzania ni kukuza uwekezaji, hususani katika sekta za uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi.

“Kwa upande wa Serikali, kila ofisi anayoingia mwekezaji, wanatafuta kipengele kinachoweza kumkwamisha ili wazo lake likwame badala ya kutafuta namna nzuri ya kufanikisha uwekezaji.”Amesema Mwigulu na kuongeza

“Kwa upande wa wananchi, atakutana na mtazamo wa uraiani mathalani mwekezaji anapofika na mtaji wa kuwekeza kwenye meli na bandari ya uvuvi wa samaki kwenye kina kirefu ambao hata wasipovuliwa watahama na kuvuliwa sehemu nyingine, mosi utasikia ana fedha kweli, huyu sio tapeli kweli?.

"Pili wakijiridhisha ana fedha, utasikia huyu hatatuibia kweli? tatu akitokea anayeshauri kwamba nadhani uwekezaji huu ni muhimu kwa ajili ya nchi utasikia huyu lazima ameshapewa fedha, amelambishwa asali huyu. Ni lazima tukubali uwekezaji ikiwemo kuwapa majina mazuri wanaobeba hatima za wengine,”amesema Waziri Dkt.Mwigulu.

Marufuku

Wakati huo huo, Serrikali imepiga marufuku utaratibu wa taasisi mbalimbali za Serikali na halmashauri kufunga biashara, ofisi na maeneo mengine ya uzalishaji.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, kumekuwa na tabia baada ya kufanya kaguzi na kuthibitisha ukiukwaji wa sheria mbalimbali zinazosimamia biashara ukimbilia kuzifunga.

“Ufungaji wa biashara, kwa sababu zozote zile, una athari kubwa kwa ustawi wa uchumi wetu kwa kuathiri ajira za wananchi, ustawi wa biashara, mapato ya kampuni na mapato ya Serikali,”amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Pia, amesema utaratibu huo unakwenda kinyume na juhudi kubwa za Rais Dkt.Samia katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Waziri amesema ili kuondokana na athari hizo, anapendekeza kuanzia Julai Mosi, mwaka huu iwe ni marufuku kwa taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu mbalimbali.

Aidha, anapendekeza sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zirekebishwe ili kumchukulia hatua mwenye biashara kwa makosa ya biashara na siyo kuifunga biashara yenyewe.

“Hatua hii inalenga kulinda ajira za watanzania, mapato ya biashara, kukuza uchumi na kuongeza mapato ya Serikali,”amesema.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu ameendelea kufafanua kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wanasema kodi zinatozwa nchini ni za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, za Waziri Mwigulu au za TRA ambapo amesema hiyo sio kweli kwakuwa kodi ni jambo la nchi.

“Kumezuka dhana ya kuona kuwa kodi zinazotozwa ni kubwa bila kujali mzigo mkubwa wa Serikali kwa nchi yetu katika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za jamii, kuna baadhi ya wanasiasa wanasema kodi hizi ni za Samia, kodi hizi za Mwigulu, kodi hizi za TRA.

“Kodi zote zinazokusanywa huwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali uliopo Benki Kuu ya Tanzania, na baadae kupelekwa kwenye wizara za kisekta, fedha hizo ndizo zinazotumika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo mijini na vijijini ikiwemo miradi ya umeme,

"Maji, barabara, madaraja, vivuko, reli, usafiri wa anga, madarasa, zahanati, ununuzi na usambazaji wa dawa na malipo ya mishahara ya watumishi kama walimu, wauguzi na madaktari.

“Kila mmoja wetu ajue kuwa, kodi sio jambo la Rais, kodi sio jambo la Waziri wa Fedha, kodi sio jambo la TRA, kodi ni jambo la nchi.

"Kodi ndio maendeleo ya nchi yetu, kila Mtanzania mwenye sifa za kulipa kodi ana wajibu wa kulipa kodi stahiki na halali kwa mujibu wa sheria, ni lazima kulipa kodi, ni lazima tutumie mashine za EFD bila udhuru wowote, ni lazima kila anayeuza atoe risiti na anayenunua adai risiti,”amesema.

Kicheko wanafunzi

Wakati huo huo, Serikali imependekeza kuanzishwa kwa programu ya mikopo ya wanafunzi waliochaguliwa katika vyuo vya kati katika fani za kipaumbele ambazo ni uchumi, elimu sayansi na afya.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wataalamu na ujuzi unaohitajika katika azima ya mapinduzi ya viwanda nchini.

Pia amesema wanapendekeza kuondolewa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na Vyuo vya Ufundi vya Dar es Salaam Institute of Technology (DIT), Mbeya University of Science and Technology (MUST) na Arusha Technical College (ATC).

Amesema, hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi na elimu inayohitajika katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda ndani na nje ya nchi.

“Nilisema hotuba hii imebeba hotuba ya Mama namna anavyotaka kuwasaidia watoto wa maskini. Pochi ya Mama imefunguka. Mama yuko kazini.

"Serikali inapendekeza kuanzisha programu ya mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa na Serikali kusoma kwenye vyuo vinavyotoa elimu katika fani za kipaumbele.

"Hatua hii itaanza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo wa 2023/24, pia Mama aliamua kuongeza kiwango cha posho ya kujikimu maarufu kama boom kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi 8,500 hadi shilingi 10,000 kwa siku,”amefafanua Waziri Dkt.Mwigulu.

Muungano

Aidha, Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, Serikali imezipatia ufumbuzi hoja nne za Muungano ikiwemo ya malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.

Mheshimiwa Waziri amezitaja kodi hizo ni pamoja na kodi ya mapato kadri unavyopata na kodi ya zuio mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume (Terminal III).

"Pia ongezeko la gharama za umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).

"Hivyo ni jukumu letu sote kuulinda, kuudumisha na kuuenzi Muungano. Katika kuendelea kudumisha Muungano, Serikali imekuwa ikifanya vikao mbalimbali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa hoja za Muungano,"amesema.

Dkt.Mwigulu ameongeza kuwa, katika mwaka 2022/23, Serikali ilijadili hoja nane za Muungano ambapo nne zilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya hoja za Muungano.

MSD

Amesema,Serikali inakusudia kuipatia Bohari ya Dawa (MSD) mtaji ili iweze kufanya kazi kwa kujitegemea na si kutegemea fedha serikalini katika kujiendesha.

“Serikali imeendelea kuboresha ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba ambapo mpaka sasa kiasi cha Sh485 bilioni zimetolewa kupitia Bohari ya Dawa MSD, hii ni njia ya kuona huduma za afya zinaendelea kuimarishwa hivyo kufikia mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kutenga fedha zaidi.

“Serikali itaendelea kutenga fedha kwa kuipatia mtaji MSD ili ifanye kazi kama bohari ya dawa na si kitengo cha ununuzi wa dawa Serikali,”amesema Waziri Dkt.Mwigulu.

Pia, amesema Serikali imepanga kulipa madeni ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuiwezesha kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi.

Vyanzo vya mapato

Mbali na hayo, Serikali imependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 kwa kuongeza ushuru wa barabara na mafuta kwa kiasi cha shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta ya Petroli na Dizeli.

Waziri Dkt.Mwigulu amesema, pia anapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 4A cha Sheria ya Ushuru wa Barabara Sura, 220 kwa kuongeza kipengele ‘c’ kitakachoelekeza fedha zitakazokusanywa kutokana na ongezeko hilo la ushuru wa barabara na mafuta la shilingi 100 kwa mafuta ya petroli na dizeli.

Amesema, fedha hizo zitakazokatwa zitatumika kwenye utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ili kupata vyanzo vya uhakika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.“Hatua hii inatarajia kuongeza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 381,826.8,”amesema.

Wakati huo huo,Mheshimiwa Waziri Mwigulu amesema marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa hasa kwa zile za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla.

“Kwa muktadha huo, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru kwa kiwango cha asilimia 10 ya bei kwenye bidhaa zisizo za petroli, na asilimia 20 ya bei kwenye bidhaa za bia na tumbaku,” amesema.

Amesema, lengo la hatua hiyo ni kuakisi mabadiliko ya thamani ya mapato ya Serikali kwa kuwa utozaji wa ushuru wa bidhaa kwa kutumia viwango maalum usiporekebishwa hupoteza thamani ya fedha na hivyo kupunguza mapato.

“Njia bora inayotumika kuondoa mapungufu hayo ni kurekebisha viwango maalum vya ushuru ili kuendana na thamani ya fedha kulingana na mfumuko wa bei,”amesema Waziri Dkt.Mwigulu.

Dhahabu

Pia, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, Serikali imekamilisha taratibu za kununua dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kuanzisha akiba ya dhahabu hapa nchini.

“Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa viwanda vya kusafishia dhahabu, Serikali itaendelea kuweka vivutio kwa viwanda hivyo ili vipate malighafi ya kutosha na ili kukamilisha hilo Serikali imepunguza mrahaba wa madini yanayouzwa kwenye viwanda hivyo kutoka asilimia sita hadi asilimia nne.

“Nafurahi kulijulisha Bunge kuwa Serikali imekamilisha taratibu za kununua dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kuanzisha akiba ya dhahabu hapa nchini.

“Tunataka tunapotaja akiba ta fedha za kigeni tutaje na akiba ya dhahabu tuliyonayo, hatua hii itawapatia wachimbaji bei nzuri na kuimarisha sarafu ya nchi yetu, hii ni baada ya kupokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia na michango ya waheshimiwa wabunge,”amesema.

Matangazo

Waziri Dkt.Mwigulu ameendelea kufafanua kuwa, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatarajia kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia na kuhakikisha kodi husika za Serikali kupitia matangazo yanayowekwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama blogs, Instagram, Facebook na Twitter zinalipwa kwa wakati.

Amesema, uamuzi huo unatokana na ukuaji wa teknolojia ambao umeleta mabadiliko pia katika tasnia ya matangazo ya kibiashara.

“Kutokana na ukuaji wa teknolojia, Dunia inashuhudia mabadiliko makubwa katika tasnia ya matangazo ya kibiashara (Advertisment) ambapo sasa matangazo mengi yamekua yakifanyika kupitia mitandao (online advertisement) hasa mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Facebook,Twitter na blogs mbalimbali.

“Kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali inatarajia kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia na kuhakikisha kodi husika za Serikali zinalipwa kwa wakati, hii itajumuisha matangazo ya biashara ambayo huwekwa na watu maarufu (digital influencers) na biashara za mtandaoni zinazofanyika nchini,”amesema.

Ajira

Wakati huo huo, Serikali imesema licha ya hatua kubwa ilizochukua za kujenga uchumi, tatizo la ajira kwa vijana bado ni kubwa nchini.

Mheshimiwa Dkt.Mwigulu amesema, utafiti wa Nguvukazi wa mwaka 2020/21 ulibaini kuwa ukosefu wa ajira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 35 nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka kutoka asilimia 12.1 kwa mwaka 2014 hadi aslimia 12.6 kwa mwaka 2020/21. 7

“Tatizo hili la ajira ni kubwa zaidi hasa kwa vijana wa kike ambao ni asilimia 16.7 ikiwa ni mara mbili ya kiwango kwa vijana wa kiume ambao ni asilimia 8.3,”amesema.

Amesema, Serikali imechukua hatua mbalimbali kupunguza tatizo hilo la ajira na kwamba katika Utafiti wa Nguvukazi wa mwaka 2020/21 ulibaini kuwa ukosefu wa ajira kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 au zaidi ulipungua hadi asilimia 9.3 kutoka asilimia 10.5 mwaka 2014.

“Kupungua kwa kiwango hiki ni matokeo ya juhudi mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali, ingawa viwango vya ukosefu wa ajira bado ni vya juu na vinahitaji juhudi zaidi kuvipunguza,”amesema.

Licha ya changamoto hiyo ya ajira, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema,Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini uliokithiri kutoka asilimia 9.7 kwa mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.

“Pamoja na utajiri tulionao na hatua kubwa iliyopigwa,nchi yetu bado ina wananchi maskini, kiwango cha umasikini cha mahitaji ya msingi kitaifa kinapimwa kwa kuangalia wanakaya wanaoishi kwa kutumia chini ya shilingi 49,320 kwa mwezi kwa mtu mzima kwa ajili ya kupata mahitaji ya msingi.

"Vilevile, kiwango cha umasikini uliokithiri (umasikini wa chakula) unapimwa kwa kuangalia wanakaya wanaoishi kwa kutumia chini ya shilingi 33,748 kwa mwezi kwa mtu mzima hivyo kushindwa kumudu kupata chakula chenye kalori 2,200 zinazotakiwa kwa mtu mzima kwa siku.

“Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya wa mwaka 2017/18 ulionesha kuwa asilimia 26.4 ya Watanzania walikuwa wanaishi chini ya mstari wa umasikini wa mahitaji ya msingi, hali hii imepungua kutoka asimilia 28.2 kwa mwaka 2012, Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini uliokithiri kutoka asilimia 9.7 kwa mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.

“Hata hivyo, kiwango cha umasikini kimeendelea kupungua, lakini siyo kwa kasi ya kuridhisha hivyo bado kuna Watanzania masikini,”amesema.

Betting

Mheshimiwa Waziri amependekeza kuongeza tozo ya michezo ya kubahatisha kutoka shilingi 10,000 hadi shilingi 30,000 kwa kila mashine ya sloti kwenye maeneo ya baa.

“Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha kwa kuanzisha michezo ya meza isiyozidi miwili katika maeneo yenye Mashine za Sloti Arobaini (Forty Machine Site).

"Lengo la hatua hii ni kuongeza ukusanyaji wa mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha kutoka kwenye uendeshaji wa Mashine Arobaini za Sloti.

“Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 4,223 kwa mwaka wa fedha 2023/24, pia napendekeza kuongeza tozo ya michezo ya kubahatisha kutoka shilingi 10,000 hadi shilingi 30,000 kwa kila mashine ya sloti kwenye maeneo ya baa (sehemu za kuuzia pombe), hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 4,738 mwaka 2023/24.

“Kuanzisha ada ya maombi ya shilingi 500,000 na ada ya leseni kuu ya dola za Kimarekani 10,000 kwa mwaka kwenye mashine za sloti kwenye maduka, ada ya maombi ya shilingi 500,000 na ada ya leseni kuu ya dola za Kimarekani 10,000 kwa mwaka kwenye mashine za sloti katika maeneo ya baa (sehemu za kuuzia pombe).

"Ada ya maombi ya shilingi 500,000 na ada ya leseni kuu dola za Kimarekani 5,000 kwa mwaka kwenye mashine arobaini za sloti.

“Lengo la hatua hii ni kuweka utofauti kati ya shughuli za mashine za sloti katika maeneo ya baa (sehemu za kuuza pombe), maduka na shughuli za mashine arobaini za sloti pamoja na kuwezesha ufanisi na udhibiti bora wa michezo ya kubahatisha,”amesema.

Pia amependekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 20 kwenye mashine za kamari zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na zinazozalishwa nchini.

“Mashine hizo zinatambulika kwa Hs Code 9504.30.00, lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali, hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,365.4,”amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Msamaha

Mheshimiwa Waziri kupitia hotuba yake amependekeza kusamehe ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa mujibu wa uwezo wa injini (engine capacity) kwenye magari yanayotumia nishati ya umeme pekee yanayotambulika kwa HS Code 8702.40.11; 8702.40.19; 8703.80.10 na 8703.80.90 na magari yanayotumia Nishati ya Gesi Asilia (CNG) pekee.

“Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya nishati ya umeme na gesi asilia nchini na hivyo kuokoa matumizi ya fedha za kigeni inayotumika kuagiza nishati ya mafuta kutoka nje ya nchi,"amesema.

Pia amependekeza kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye uuzaji na ukodishaji wa ndege, injini za ndege na vifaa vyake vinavyouzwa nchini.

“Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa waendeshaji wa shughuli za usafiri wa anga kwa kuwawezesha kununua bidhaa husika nchini au kuagiza kutoka nje ya nchi bila kulipa kodi ya ongezeko la thamani.

“Hatua hii itafuta uamuzi uliochukuliwa mwaka 2022/23 ili kuendana na dhamira ya kukuza sekta ya utalii sambamba na hatua ya Mheshimiwa Rais ya kuhamasisha sekta hii kupitia filamu yake ya “Royal Tour,”amesema Mheshimiwa Dkt.Mwigulu.

Himilivu

Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, deni la Serikali hadi Aprili 2023, lilikuwa shilingi trilioni 79.10, sawa na ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 69.44 mwezi Aprili 2022.

Amesema, kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni shilingi trilioni 27.94, sawa na asilimia 35.3 na deni la nje ni shilingi trilioni 51.16, sawa na asilimia 64.7.

“Kati ya deni la nje, deni lenye masharti nafuu ni shilingi trilioni 37.69, sawa na asilimia 73.6, hivyo, sehemu kubwa ya deni la nje ni mikopo yenye masharti nafuu,”amesema.

Amesema, tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba 2022 ilionesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu.

Waziri Dkt.Mwigulu amesema kuwa, matokeo ya tathmini yanaonesha uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 32.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 18.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40.

Aidha, uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 120 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.

Amesema, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa 60 mauzo ya bidhaa na huduma nje ni asilimia 13.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 15.

“Matokeo haya yanawiana na matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanywa na Shirika la Fedha la Kimataifa na kuchapishwa Aprili 2023,”amesema.

Amesema, katika kuhakikisha kuwa Deni la Serikali linaendelea kuwa himilivu, Serikali inatekeleza hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha mikopo inayopewa kipaumbele ni ile yenye masharti nafuu kadri inavyopatikana.

Hali hiyo inajidhihirisha katika bajeti inayopendekezwa ambapo mikopo nafuu imeongezeka kwa asilimia 22.8 na yenye masharti ya kibiashara imepungua kwa asilimia 14.4.

“Kuelekeza mikopo yenye masharti ya kibiashara katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na mauzo nje ya nchi, kuboresha mikakati ya kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuhakikisha sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa na mapato ya ndani pamoja na kupunguza matumizi yanayoweza kuepukika bila kuathiri uendeshaji wa shughuli za Serikali,”amesema Waziri Dkt.Mwigulu.

Mapendekezo mengine

Kupitia hotuba yake, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amependekeza kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotumbulika kwa HS code 9619.00.90.

Amesema, lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyp hapa nchini, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali.

Pia, amependekeza kupunguza Ushuru wa Bidhaa kutoka shilingi 4,386 kwa lita hadi shilingi 2,466.45 kwa lita kwenye vinywaji vikali (ready to drink) vinavyozalishwa nchini. Vinywaji hivyo vinatambulika kwa Hs Code 2208.60.00.

Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani na kuvifanya viwe shindani. Hatua hii inatarajia kupunguza 107 mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 779.1.

Nyingine ni kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye magari ya abiria yanayoingizwa nchini yanayozidi umri wa miaka mitano (magari chakavu) yaliyotokana na ukuaji wa teknolojia ili kuwianisha na magari mengine yanayofanana yanayotozwa ushuru huo.

Magari hayo ni yale yanayotambuliwa kwa H.S Codes 8702.20.22, 8702.20.29, 8702.20.99, 8702.30.22, 8702.30.29, 8702.30.99, 8702.40.22, 8702.40.29 na 8702.40.99.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu pia amependekeza kupunguza ada ya hati miliki kutoka shilingi 50,000 kwa hati hadi shilingi 25,000 kwa hati.

Aidha, amependekeza kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mabasi ya abiria yanayotambulika kwa HS Codes 8702.10.99 na 8702.20.99 yanayoingizwa nchini kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri, hatua hii inalenga kupunguza gharama za uingizaji wa mabasi hayo ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi.

Jambo lingine ni kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Cash registers, Electronic Fiscal Device (EFD) Machines and Point of Sale (POS) machines) zinazotambulika kwa HS Codes 8470.50.00 na 8470.90.00.

Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya vifaa hivi katika kuhasibu mapato ya Serikali.Huku akipendekeza kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye Gypsum Powder inayotambulika kwa HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja.

Lengo la hatua hii ni kulinda wazalishaji wa Gypsum Powder nchini.Aidha, amependekeza kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwa waunganishaji wa pikipiki za matairi matatu.

Pendekezo hilo ni bila kujumuisha fremu ili ziweze kutengenezwa na kuunganishwa hapa nchini (CKD for three-wheel motorcycles excluding chassis and its components) zinazotambulika kwa HS Code 8704.21.90.

Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa waunganishaji wa 152 pikipiki hizo nchini ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo. Kutoza ushuru wa Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye 149 matairi mapya ya pikipiki (new pneumatic tyres of rubber) yanayotambulika kwa HS Code 4011.40.00.
Amesema, lengo la hatua ni kuhamasisha uzalishaji wa matairi hayo nchini kwa kuwa kuna malighafi za kutosha.Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza sabuni (toilet soap) zinazotambulika kwa HS Code 3401.20.10.

Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa sabuni nchini, kuongeza ajira na mapato ya Serikali. Pia, kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Marekani 500 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa 158 kikubwa badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (refined) yanayotambulika kwa HS codes 1507.90.00; 1508.90.00; 1509; 1510.10.00; 1510.90.00; 1511.90.30; 1511.90.90; 1512.19.00; 1512.29.00; 1513.19.00; 1513.29.00; 1514.19.00; 1514.99.00; 1515.19.00; 1515.29.00; 1515.50.00; na 1515.90.00.

Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda na kuhamasisha uchakataji wa mbegu na mafuta ghafi yaliyoingizwa nchini ili kuongeza thamani ya bidhaa (value addition), kukuza ajira, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.Kuongeza ada ya usajili wa mkufunzi mpya wa shule ya udereva kutoka Shilingi 10,000.00 hadi Shilingi 20,000.00 na kuongeza tozo ya ada ya upotevu wa mali kutoka shilingi 500.00 hadi shilingi 1,000.00.

Mheshimiwa Waziri amependekeza kufuta tozo kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji ili kuchochea matumizi ya kielektroniki katika miamala mbalimbali.

Kuongeza ushuru wa bidhaa kutoka shilingi 589.05 kwa lita hadi shilingi 600 kwa lita kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu (Energy Drink) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Vinywaji hivyo vinatambulika kwa Hs Code 2202.99.00.

Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani na kuvifanya viwe shindani. Hatua hii inatarajia 110 kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 36.9.

Nyingine ni kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 30 kwenye sigara na bidhaa za aina hiyo zinazotumia mbadala wa tumbaku zinazotambulika kwa Hs code 2402.90.00; tumbaku inayovutwa kwa kutumia bomba la 109 maji inayotambulika kwa Hs code 2403.11.00; na sigara za kielektroniki, shisha na bidhaa za aina hiyo zinazotambulika kwa Hs codes 8543.40.10, 8543.40.90 na 9614.00.00.

Lengo la hatua hii ni kujumuisha bidhaa mpya zinazotumika kama mbadala wa tumbaku ambazo pia zina athari sawa na tumbaku. Kuongeza kima cha usajili kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani kinachotakiwa kwa mfanyabiashara kusajiliwa kutoka shilingi milioni 100 hadi shilingi milioni 200.

Amesema, Serikali itaendelea kuongeza kima husika hadi kufikia shilingi milioni 500 ili kuepusha athari za kimapato zinazoweza kujitokeza. Lengo la hatua hii ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa Kodi ya Ongezeko la Thamani na kuchochea ulipaji kodi wa hiari.

Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyumba zinazouzwa na wajenzi wa nyumba za kibiashara zenye gharama nafuu isiyozidi shilingi milioni 50.

Lengo ni kutoa 97 unafuu kwa wanunuaji wa nyumba hizo na kuboresha maisha ya watanzania.Kutoza Ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye magari yenye uwezo wa injini (Engine Capacity) wa kati ya 1000cc hadi 2000cc yaliyotokana na ukuaji wa teknolojia ili kuwianisha na magari mengine yenye ukubwa unaofanana yanayotozwa ushuru huo.

Magari hayo ni yale yanayotambuliwa kwenye H.S Codes 8703.40.00, 8703.50.00, 8703.60.00 na 8703.70.00. Kutoza Ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye magari yenye uwezo wa 108 injini (Engine Capacity) wa zaidi ya 2000cc yaliyotokana na ukuaji wa teknolojia ili kuwianisha na magari mengine yenye ukubwa unaofanana yanayotozwa ushuru huo.

Magari hayo ni yale yanayotambuliwa kwa H.S Codes 8702.10.11, 8702.10.19, 8702.20.11, 8702.20.19, 8702.30.11, 8702.30.19, 8702.90.11, 8702.90.19, 8703.40.00, 8703.50.00, 8703.60.00, 8703.70.00, na 8703.90.90.

Kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye magari ya abiria yanayoingizwa nchini yanayozidi umri wa miaka mitano (magari chakavu) yaliyotokana na ukuaji wa teknolojia ili kuwianisha na magari mengine yanayofanana yanayotozwa ushuru huo.

Magari hayo ni yale yanayotambuliwa kwa H.S Codes 8702.20.22, 8702.20.29, 8702.20.99, 8702.30.22, 8702.30.29, 8702.30.99, 8702.40.22, 8702.40.29 na 8702.40.99;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news