Rais Dkt.Mwinyi:Walioshindwa kutoa majibu kwa CAG watawajibishwa

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itawachukulia hatua za kisheria watumishi kutoka taasisi na mashirika ya umma walioshindwa kutoa majibu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya mwaka wa Fedha 2022- 2023 iliyowasilishwa na kusomwa Ikulu jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akielekea katika eneo lililoandaliwa katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya uwasilishwaji wa Taarifa za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliyowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Dkt. Othman Abbas Ali, iliyowasilishwa leo Juni 3,2023 katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza kwenye viwanja vya Ikulu, Zanzibar baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Kuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, (CAG).

“Nitatataka kupata majibu kwa wote waliotajwa kwenye ripoti ya CAG ambao hawakutoa majibu, watoe ambao watashindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa,”amesisitiza Rais Dkt.Mwinyi.
Rais Dkt.Mwinyi amesema, ripoti imeonesha mafanikio, changamoto na mapungufu ambayo Ofisi ya CAG iliyabainisha wakati wa uwasilishwaji wake na kueleza kwamba Serikali itachukua hatua mbalimbali zikiwemo za kiutawala na kijinai kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.

“Kwa wale wote watakaothibitika kufanya ubadhirifu, wizi au uzembe ulioisababishia Serikali kupata hasara, utaratibu wa kuchukua hatua uko wazi,"amebainisha Rais Dkt.Mwinyi.

Amesema, kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kuchukuliwa hatua za kiutawala na baadhi ya kuchukuliwa hatua za sheria za makosa ya jinai.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kwamba, ataikabidhi ripoti hiyo kwa mamlaka zinazohusika kwa hatua zaidi, ikiwemo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili nao waipitie kwa kina mapungufu yote hasa yaliyoashiria wizi kwa ajili ya hatua zaidi kwa mujibu wa sheria.
Dkt.Mwinyi amesema, ripoti za CAG ni kipimo tosha cha utendaji kwa wale wote waliopewa majukumu na Serikali kwa kufanikiwa ama kushindwa kuyasimamia katika kuitumikia Serikali.

“Utaratibu huu tuliouazisha wa kuwasilisha ripoti za CAG hadharani utakuwa wa kudumu, nafahamu kuwa haukuzoeleka na unawapa mashaka baadhi ya watu, nataka niwahakikishie kwa wale wenye mashaka, hili litakua zoezi la kila mwaka, na ni moja wapo ya kigezo cha uwazi na utawala bora katika uendeshaji wa Serikali yetu,” amebainisha Rais Dkt.Mwinyi.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Zanzibar, Dkt. Othman Abbas Ali akielekea katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kuwasilisha Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika leo katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.

Hata hivyo, amewataka watendaji na watumishi wa taasisi na mashirika ya Serikali kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar panapokuwa na wajibu wa kufanya hiyo. Amesema, kutofanya hivyo ni kosa kisheria na Serikali haitosita kutimiza wajibu wake.
Akizungumzia mapungufu yaliyojitokeza kwenye ripoti hiyo, Rais Dkt.Mwinyi alieleza baadhi ya mapungufu hayo ni ya kiutaratibu, mengi yalisababishwa na wizi na mengine uzembe kwa baadhi ya watu.

Hivyo alieleza, kazi ya CAG kutoa taarifa na mapendekezo kwa Serikali na jukumu la kufanyia kazi ripoti hiyo ni la Serikali.

Mapema akiwasilisha ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dkt.Othman Abass Ali, aliishauri Serikali kuunganisha pamoja mifumo yote ya fedha ya Serikali, kwa miamala ya fedha zikiwemo fedha zilizoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia mifumo ya Wizara ya Fedha kwa lengo la kuiwezesha mifumo hiyo, kufanya usuluhishi wa upatikanaji wa taarifa za ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa wakati sahihi.

Sambamba na kuziunganisha pamoja sekta zote za Serikali zinazofanyakazi zinazofanana katika mfumo mmoja zikiwemo, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Kampuni ya Usafirishaji bandarini na nyenginezo ili kupata idadi kamili ya wageni na abiria wanaoondoka Zanzibar kwa lengo la kuwepo kigezo sahihi cha ukokotoaji wa ukusanywaji wa mapato yanayotakiwa kupatikana kutoka kwenye vyanzo hivyo.
Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (kutoka kushoto) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman,Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt.Mwinyi Talib Haji, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Saleh Omar Kabi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe.Dkt. Saada Salum Mkuya na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Dimwa, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo.
Viongozi wa Vyama vya Siasa wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akizungumza baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliyowasilisha na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Dkt.Othman Abbas Ali, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo.
Viongozi wa Serikali na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akizungumza katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar, baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,iliyowasilisha na Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa Serikali Dkt.Othman Abbas Ali, hafla hiyo iliyofanyika leo katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.Baadhi ya Watendaji Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wageni waalikwa wakifuatilia taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakati ikiwasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Zanzibar Dkt. Othman Abbas Ali.(hayupo pichani) hafla hiyo iliyofanyika leo katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar.

Pia aliishauri Serikali kuongeza udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi, ikiwemo kufanya uteketezaji pamoja na kuvipitia vituo vyote vya afya kwa hospital zote za Wilaya, Mikoa hadi Rufaa kwa dawa zilizomo hospitalini pia kufanya vipimo vya kimaabara ili kugundua dawa na vifaa visivyo salama kwa matumizi wa binaadamu kwa kuzichukulia hatua za haraka na kuziondosha kwa kuziteketeza kwa wakati.

Akizungumzia suala la kulipa fidia kwa wananchi wanaotoa maeneo yao kwaajili ya kupisha miradi ya Serikali ya Maendeleo, CAG akiishauri Serikali kuona umuhimu wa kuwalipa kwa wakati ili kuepusha malalamiko, kucheleweshewa kulipwa kwa wakati kunapunguza thamani ya fidia kutokana na kupungua kwa thamani ya fedha.

Jumla ya ripoti saba ikiwemo ya Serikali Kuu (Mawizara na taasisi zote), Mashirika na Taasisi zinazojitegemea, ripoti ya Idara Maalum na taasisi zake, ripoti ya mifumo yote ya Tehema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ripoti ya Mashirika ya Umma, na ripoti ya Ufanisi ya miradi ya Maendeleo iliyofadhiliwa na fedha za Uviko 19 ziliwasilishwa.
Kifungu cha 112 (5) kinamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, awasilishe taarifa yote aliyoikagua na aikabidhi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hatua nyengine. Mei 11 mwaka huu alivyanya hivyo na baadae Rais Dkt. Mwinyi alimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman ambaye naye aliikabihi Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa takwa la kikatiba kwa ajili ya kujadiliwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news