RC Chalamila asisitiza ufanisi miradi ya maendeleo

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amewataka viongozi wa wilaya na halmashauri mkoani Dar es Salaam kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
RC Chalamila ameyasema hayo Juni 1, 2023 baada ya kukutana na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni na Temeke kwa nyakati tofauti ikiwa ni muendelezo wa kujitambulisha toka apangiwe kuhudumu katika mkoa huo.

Akizungumza na watumishi hao amewataka viongozi wa wilaya na halmashauri kusimamia kwa weledi na kuzingatia thamani ya fedha wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za manunuzi ya umma. 
 
Aidha, RC Chalamila katika kikao hicho ametoa rai kwa waheshimiwa madiwani kuwa mstari wa mbele katika usimamizi wa miradi huku akiwataka kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali. 

Sambamba na hilo Mheshimiwa Chalamila ametoa rai kwa viongozi Idara ya Elimu kuja na mpango mkakati utakaosaidia kuinua elimu ndani ya wilaya hizo huku akilenga kuongeza mapato, kwani uwezekano wa kufanya hivyo upo ikiwa tu wataamua kuwa wabunifu. 
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato, Mheshimiwa Chalamila amesema, kumekuwa na ukusanyaji usioridhisha hasa wa ushuru wa huduma,hivyo ameelekeza watendaji kujipanga vizuri ili kusaidia katika ukusanyaji wa kodi hiyo. 

RC Chalamila akiwa Temeke alipata wasaa wa kukutana na wazee wa wilaya hiyo ambapo walionesha kufurahishwa namna Mheshimiwa Chalamila anavyotekeleza majukumu yake siku chache toka alipohamishiwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassani kuhudumu katika mkoa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news