Wakulima mambo mazuri yanakuja Mpwapwa

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 27.9 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Msagali litakalotumika kwa shughuli za kilimo biashara katika Kata ya Ng’ambi na Chunyu, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati wa siku ya pili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndugu Daniel Chongolo katika Mkoa wa Dodoma.

Senyemule amesema kukamilika kwa bwawa hilo kutasaidia Wilaya ya Mpwapwa na maeneo ya jirani kujishughulisha na kilimo mwaka mzima. 

"Ndugu zangu Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwakomboa wana Mpwapwa kwa kuleta mradi huu mkubwa ambao utakuwa ni mkombozi kiuchumi na kijamii, rai yangu tuhamikishe mradi huu unatunza ili uweze kutunufaisha sote,"amesisitiza Mhe.Senyamule. 

Senyamule amesema kwa Wilaya ya Mpwapwa Serikali imeendea kuleta miradi ya Afya, Elimu na ujenzi wa miundombinu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Barabara na skimu za umwagiliaji. 
Senyamule amewataka wakazi wa Kingiti kuendea kutunza na kuhifadhi mazingira kwakuwa uhai wa kila kiumbe unategemea mazingira endelevu. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Bw. Daniel Chongolo amekemea vikali uharibu wa mazingira unaofanywa na wakazi wa Kingiti katika Milima ya Guru na Lugundalule na kumwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua kali za kisheria kwa waharibifu wote wa mazingira. 

“Hakuna maisha bila kutunza na kuhifadhi mazingira, maisha yetu sote yanategemea hifadhi endelevu ya vyanzo maji, maji ni uhai hivyo tukiharibu vyanzo hivi tunahatarisha uhai wetu wenyewe. Hatuwezi kucheza na maisha ya watu kwa kuruhusi hali ya uharibifu iendelee,” Chongolo amekemea. 

Bwawa hilo lenye ukubwa wa hekta 1428 sawa na kilometa za mraba 14 litakuwa na ukubwa wa mita za ujazo 92.2 sawa na lita bilioni 92.2. Ujenzi wa bwawa unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 27.9 na kazi ya ujenzi inafanywa na kampuni ya wazawa ya GNMS Contactors Co. Ltd kutoka Iringa na ujenzi unatarajia kukamilika mwezi Novemba 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news