TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-31:UVIKO, KATUONGOZA DKT.SAMIA KUPATA CHANJO

NA LWAGA MWAMBANDE

JANUARI 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa ugonjwa mpya wa virusi vya Corona katika Mkoa wa Hubei nchini China kuwa suala la hali ya hatari ya afya ya umma Kimataifa kwa sababu ya uwezekano mkubwa wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona vya mwaka 2019 (UVIKO-19) kuenea duniani kote.

Virusi hivyo, vilisambaa kwa kasi duniani kote huku vikisababisha maumivu na vifo vya watu wengi, ingawa jitihada mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa ziliendelea ili kutafuta suluhu ya kukabiliana na ugonjwa huo hatari.

UVIKO-19 haikuathiri tu sekta ya afya, bali iliathiri uchumi kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na biashara na utalii, ambazo ndio nguzo kuu za maisha katika mataifa mbalimbali ikiwemo Ukanda wa Afrika Mashariki.

Kirusi ambacho husababisha Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) ni cha aina mpya ambacho hakikuwa kimewahi kutokea kwa binadamu hadi ugonjwa huo ulipozuka mwaka 2019.

Aidha, wataalamu walibainisha kuwa, UVIKO-19 ni kundi kubwa la virusi ambavyo kwa kawaida hupatikana kwa wanyama na husababisha maradhi hatari yanyohusiana na upumuaji kama vile dalili za upumuaji za Middle East (Middle East Respiratory Syndrome (MERS-CoV) na dalili kali na hatari za upumuaji (Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS- CoV).

Baada ya jitihada mbalimbali za kukabiliana na janga hilo ikiwemo hamasa ya chanjo, hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza rasmi ukomo wa hali ya dharura ya kimataifa ya UVIKO-19 ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu baada ya tamko lake la awali juu ya hatari ya ugonjwa huo Januari, 2020.

“Kwa matumaini makubwa tunatangaza mwisho wa UVIKO-19 kama dharura ya afya ya umma ulimwenguni, haimaanishi ugonjwa huo sio tishio tena ulimwenguni,” ilifafanua sehemu ya taarifa iliyotolewa hivi karibuni na WHO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan akipokea chanjo dhidi ya UVIKO-19 baada ya uzinduzi uliofanyika Julai, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na UVIKO-19 nchini zimeleta matokeo chanya mijini na vijijini. Endelea;

1.Wale walifikiria,
Kuna kupwaya Samia,
Vinywa wazi wasalia,
Na mikono mashavuni.

2.Kubwa aliloanzia,
Nchi kuifungulia,
Ni gonjwa lilovamia,
Hapa kwetu duniani.

3.Ilikuwa Tanzania,
Ni kisiwa cha dunia,
UVIKO lipoingia,
Lielekea kusini.

4.Japo tulishangilia,
Tulivyojifukizia,
Maswali yalisalia,
Hivi tuko duniani?

5.Hakuna alobishia,
Kiongozi Tanzania,
Mikia ilisalia,
Imenyong’onyea chini.

6.Japo ilisaidia,
Imani kutuingia,
Tena tulishangilia,
Athari zikuwa duni.

7.Ila ukiangalia,
Watu wengi liishia,
Tukabaki kusalia,
Tunalilia chooni.

8.Samia lipoingia,
Mwanamke Tanzania,
Msimamo kaingia,
Mijini na vijijini.

9.Mama litutamkia,
Mwanamke kaingia,
Mpini kashikilia,
Asibezwe aslani.

10.Sera litutangazia,
Pale atapoanzia,
Yakaanza tuingia,
Kumbe tupo duniani.

11.UVIKO akapania,
Nyuma hatutasalia,
Vile atafwatilia,
Nasi tuwe duniani.

12.Sasa hivi Tanzania,
Ni sehemu ya dunia,
Yale tunajifanyia,
Yafanyika duniani.

13.Chanjo tulizosagia,
Sasa tunajipatia,
Katuongoza Samia,
Naye kachanjwa begani.

14.Hii mpya Tanzania,
Mambo tunajifanyia,
Msimu tumeingia,
Sio ule wa zamani.

15.Mengi meshatufanyia,
Yale tunafurahia,
Heri tunamtakia,
Akiwapo kileleni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news