Umakini kila nukta maamuzi yake

NA ADELADIUS MAKWEGA

KUNA wakati fulani aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella (sasa ni Geita) aliagiza Mkoa wa Tanga kujenga stoo kubwa za dawa kila halmashauri, hilo lilikamlishwa katika mkoa mzima wa Tanga. 
Hospitali ya Wilaya ya Lushoto walikwenda kununua vifaa vya tiba na dawa vya kuwekwa katika stoo hiyo ili zitumike katika hospitali yao, vituo vya afya na zahanati zake kama agizo la Mhe.Martine Shigella kuwa.

“Buffer Store hizo ziwe na dawa na vifaa tiba, siyo makazi ya popo na ndege wa angani.” Lushoto waliagiza shehena kubwa ya dawa kutoka MSD na maduka ya dawa mengine ya Tanga Mjini. 

Halmashauri ya Lushoto wakati huo ilikuwa na malori ya zamani ambayo ni ya miaka mingi kama manne, yakafanyiwa ukarabati na moja kwenda kubeba mzigo, kupunguza gharama ya kukodi. Mzigo ukapakiwa na kuanza safari ya kurudi Lushoto milimani.

Lori hilo lilipofika Korogwe likakamatwa maana matairi yake hayakuwa vizuri, Mkurugenzi Mtendaji aliongea na vijana wa Jeshi la Polisi waliolikamata lori hilo na kuzungumza nao, akiwaambia kuwa ni kweli lori letu halina ubora lakini tumeamua kufanya hivyo kukamilisha zoezi la kuleta dawa katika Buffer Store yetu, tunawaomba mzigo ufike tutanunua tairi mpya.

“Mkurugenzi unahatarisha uhai wa binadamu na mali za umma, lakini tunaruhusu leo tu likifika salama nunua tairi mpya, tumeruhusu kwa kuwa dawa hizo ni za kuokoa uhai wa binadamu, hata sisi tunaweza kutibiwa muda wowote ule.” 

Lori likatoka Korogwe na kufika Lushoto salama salimini jioni ya siku hiyo. Msomaji wangu kumbuka Lushoto ni eneo lenye baridi kali, hivyo mzigo ukashushwa na kuingizwa katika jengo jipya la Buffer Store, hapo inapokea dawa kwa mara ya kwanza. 

Kwa bahati mbaya siku hiyo Mfamasia wa Wilaya hakuwepo alikwenda kufunga ndoa hivyo majukumu hayo alimkabidhi Muuguzi Mfawidhi ambaye alitimiza wajibu wake vizuri. 
Wakati zoezi hilo la kuingizwa dawa linafanyika mara kukasikika sauti ya king’ora cha gari la wagonjwa kinalia kwa sauti ya juu, watumishi wa hospitali hiyo wakatoka nje kupokea mgonjwa. 

Kweli gari hiyo ya wagonjwa ilishusha watu kadhaa majeruhi wa ajali huku magari mengine yakibeba wagonjwa pia.

Ajali ilikuwa kubwa, huku wagonjwa wakijaa OPD wakipewa huduma ya kwanza na kuitwa watumishi wengine kwenda kuongeza nguvu katika dharura hiyo. 

Kuna ajali imetokea huko Mlalo ambapo watu walikuwa wakitoka mnadani lori walilopanda lilipata ajali kupinduka watu kadhaa wamefariki.

Wakati wahudumu wa afya wa Hospitali ya Wilaya wanaendelea na kazi hiyo ya kutoa huduma ilibainika kuwa vifaa vingi vilikuwepo isipokuwa kifaa kimoja kinachofahamika kama KANYURA kilikosekana. 

Hivyo aliombwa mtumishi ambaye alikuwa katika Buffer Store ile aliyoagiza Martine Shigella ijengwe na kujazwa dawa ambayo muda huo wa jioni ndiyo wanaingiza mzigo na kuangalia je KANYURA zipo?.

Muuguzi alijibu kuwa KANYURA zimekwisha, lakini mzigo unaoingizwa sasa kutoka Tanga kuna KANYURA za kutosha. Zilichukuliwa KANYURA kadhaa na kupewa wale waliokuwa OPD na kuendelea na kazi ya kuwahudumiwa wagonjwa waliopata ajali hiyo. 

Kwa faida ya msomaji wangu ni vizuri kufahamu KANYURA ni nini? . “Kanyura ni bomba dogo ambalo linawekwa katika mshipa ili linapotundikwa dripu liweze kubebwa kwa urahisi na chochote kilichopo katika dripu kiweze kupitishwa kwa urahisi kama vile dawa, damu na maji. 

Ndani ya Kanyura kuna sindano ambayo inatoboa mshipa, Kanyura inasaidia pale sehemu sahihi palipotobolewa pawe pale pale, pasitobolewe sehemu nyingine hovyo hovyo. Kanyura inakamata penye vein. 

Kuna kitu kingine kinachofanya kazi kama Kanyura kinaitwa Skafu Vein vipo kama kipepeo, hivi vinafanya kazi kama KANYURA hiyo hiyo, kenyewe kembamba sana, Kanyura ni plastiki imara sana, mgonjwa anaweza kukaa nayo hata wiki, inasadia mgonjwa asitobolewe tobolewe kila mara.” 

Kwa faida ya msomaji wangu katika zoezi la matumzi ya KANYURA inawezakana mgonjwa mmoja akatumia hata Kanyura 10 kutokana dharura hiyo maana zoezi la kutafuta mishipa ya damu muda mwingine linakuwa gumu.

Kumbuka majeruhi wanatibiwa wodini na huyu muuguzi mfawidhi aliyetoa KANYURA akaingia kazini kuokoa uhai wa watu hao majeruhi wa ajali ya Mlola. Muuguzi mfawidhi ameshatoa KANYURA na zinafanya kazi ya kupitisha dawa, damu na maji kwa wagonjwa waliopata ajali kutoka gulioni. 

Mwanakwetu anakuomba msomaji wake kama upo halmashauri yoyote ile nchini Tanzania usikae kiasara hasara, tumia muda wako wote kuwepo hapo kujifunza mambo yanavyofanyika, kuna mambo mengi ya kujifunza kuliko eneo lolote na habari zake hazifahamiki kabisa na watu wengi kama hii simulizi ya KANYURA YA DHARURA.
Siku iliyofuata wale walifariki maiti zoa zilichukuliwa na kwenda kuzikwa haraka sana, maana wakazi wa Mlola Lushoto huwa wanazika mapema mno, nao majeruhi waliopata nafuu waliruhusiwa wengine wakipewa rufaa kwenda Bombo na KCMC. 

Siku hiyo hiyo, kamati ya ukaguzi ilifika kuupokea mzigo huo ulioingia jioni nakubaini kuwa sehemu ya mzigo huo umetumika kwa wagonjwa waliopata ajali. 
 
Sasa hoja ya KANYURA likawa hoja na kuleta maneno na malalamiko mengi kutoka kwa wajumbe wa kamati ya mapokezi na baadaye mkaguzi wa ndani wakigombea kupokea mzigo huo. 

Hoja hiyo ilipoibuka, huyu Muuguzi Mfaawidhi alipata msukosuko mkubwa huku na kule, hapo ilibidi Mkurugenzi Mtendaji kuingilia kati katika shauri hilo baada ya kushirikishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt.Charles Mkombachepa. 

“Jamani tuweni wakweli, dawa na vifaa tiba hivyo Mkuu wa Mkoa aliagiza vije kukaa stoo? Nia ni kuwahudumia wananchi ambao ni mimi na wewe, hivyo hizo KANYURA zimetumika kuwahudumia wananchi, ajali hiyo ingeweza kuwakuta hata hao wajumbe kamati ya ukaguzi na mkaguzi wa ndani, leo wasingekuwepo kufanya ukaguzi huo, hesabuni KANYURA zilizopo na zilizotumika fungeni hesabu, hiyo ilikuwa dharura tu hakuna wizi wowote ule.” 
Mwanakwetu hoja hiyo ilifungwa hapo hapo na kila mmoja kwenda na njia yake. Mkurugenzi Mtendaji akisema kama maneno yangezidi basi hoja hiyo angeelezwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati huo Martine Shigella.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini? 

Ebu fikiria msomaji wangu kama Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati huo, Martine Shigella asingeweka msisitizo wa kununuliwa dawa, je wale watu majeruhi ajali ya lori la Mlalo wangepata wapi KANYURA?.
 
Hata Mwanakwetu asingeongea vizuri na vijana wa Jeshi la Polisi waliokamata Lori, nakuapia msomaji wangu vifo vingeongezeka siku hiyo. 

Mwanakwetu anakuomba msomaji wake popote ulipo uwe makini kama alivyokuwa Mheshimiwa Martine Shigella katika maaamuzi yake, kila nukta yako na kila maamuzi yako yanaweza kuokoa uhai wa mtu au kupoteza uhai wa binadamu mwenzako, kuwa makini. 
Mkoa wa Geita jaribuni sana mtumieni huyu ndugu vizuri, atawasaidia sana. Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndugu zangu, huyu jamaa mtumieni kwa nafasi kubwa za chama hiki anaweza kuongoza vizuri sana katika mazingira yoyote yale. 
 
Mwanakwetu anaamini kuwa Shigella anaweza kukisaidia chama chetu kwa nafasi kubwa ndani ya CCM, nawaambieni ukweli. 

Mwanakwetu upo? Nakutakia siku njema. 
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news