Vijana wa Kitanzania wang'ara mafunzo kilimo cha kisasa Israel

NA MWANDISHI WETU

VIJANA 99 kati ya vijana 100 waliokuwa wanapatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa njia ya vitendo katika Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Kilimo cha Arava kilichopo Kusini mwa Israel, wamehitimu mafunzo na kutunukiwa vyeti katika mahafali yaliyofanyika tarehe 12 Juni 2023 (The Arava International Center for Agriculture Training - AICAT).
Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wakiwa wameshikilia mfano wa hundi ya Dola za Marekani 6000 kufuatia ushindi walioupata kwenye shindano la Andiko Mradi.

Kundi hili la watu 99 ambaye mmoja alirejeshwa nchini kutokana na changamoto za kiafya ni la kwanza kuhitimu katika kituo hicho tangu Tanzania ilipojiunga kwa mara ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023.
Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua akimtunuku cheti mmoja wa mhitimu wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo nchini Israel. 

Katika hotuba yake, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua aliwapongeza wahitimu wote na kuwaasa kuwa chachu ya mabadiliko wanaporejea nchini kwao kwa kufanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata nchini Israel. 
Mhitimu wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo nchini Israel baada ya kutunukiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua.

Katika mahafali hayo, mradi mmoja kutoka kwa vijana wa Tanzania ulishinda tuzo ya Dolaza Marekani 6,000.00 kutoka kwa The Dean Family Fellowship Grant, kufuatia shindano la kuandika na kuwasilisha mradi ambao vijana husika watafanya na kuleta mabadiliko chanya kwao na kwa jamii inayowazunguka, mara baada ya kurejea nyumbani. 

Tuzo hii itawawezesha vijana walioshinda kuanzisha mradi husika na hivyo kujikwamua kiuchumi. Shindano lilihusisha nchi 12 ambazo zinashiriki mafunzo hayo na tuzo ilitolewa kwa nchi 7 ikiwemo Tanzania. 
Usawa wa kijinsia umezingatiwa, Mhitimu wa Kike wa Mafunzo ya kilimo kwa vitendo nchini Israel akitunukiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua.

Aidha, vijana 5 kutoka Tanzania walipata tuzo ya wanafunzi bora na kijana mmoja ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la Tanzania amepewa ofa ya kuendelea na mafunzo kwa mwaka ujao wa masomo kutokana na nidhamu na uongozi uliotukuka. 

Kwa mwaka wa masomo 2022/2023, Tanzania ilipewa nafasi za masomo 250 ambapo vijana 100 walipelekwa kwenye kituo cha AICAT na 150 walipelekwa kituo cha mafunzo cha Agrostudies ambacho kimekuwa kikitoa mafunzo hayo kwa vijana wa Tanzania tangu programu hii ilivyoanza. Vijana wengine 150 wanatarajiwa kuhitimu mafunzo yao mwezi Agosti 2023. 
Wahitimu wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo wakiwa na vyetu vyao baada ya kutunukiwa wakati wa mahafali yaliyofanyika nchini Israel tarehe 12 Juni 2023.

Kwa mwaka wa masomo 2023/2024, Tanzania imepewa nafasi 260 ambapo vijana 150 watapelekwa Agrostudies na vijana 110 watapelekwa AICAT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news