Waziri Dkt.Mwigulu:Yajayo mifugo na uvuvi ni makubwa

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ili kuimarisha Sekya ya Mifugo na Uvuvi nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Miradi hiyo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema ni pamoja na ile ya kuimarisha afya za mifugo, huduma za ugani, huduma za tafiti na mafunzo pamoja na masoko ya mazao ya mifugo.

Amesema, mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo hadi Aprili 2023 ni pamoja na kukamilika kwa majosho 97 na kuendelea na ujenzi wa majosho 160 katika mikoa 25, kuanzisha vituo atamizi nane ili kutoa ujuzi wa unenepeshaji wa mifugo kwa vijana na wanawake.

Sambamba na ununuzi wa pikipiki 1,200 na magari 13 kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za ugani. "Katika kuimarisha sekta ya uvuvi, Serikali imeendelea kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania-TAFIRI (Dar es Salaam), kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa, kujenga na kukarabati miundombinu ya ukuzaji viumbe maji.

"Kuendelea na ujenzi wa mialo ya Chifunfu (Sengerema) na Igabiro (Bukoba) na kukamilisha taratibu za ununuzi wa boti za uvuvi 118 ikiwa ni awamu ya kwanza ya ununuzi wa boti 160 kwa ajili ya kukopesha wavuvi.

"Aidha, Serikali imepunguza tozo za kusafirisha mazao ya uvuvi nje ya nchi na kutoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na ushuru wa forodha katika uagizaji wa pembejeo mbalimbali ambapo kampuni 15 za ukuzaji viumbe maji zimenufaika,"amesema.

Pia amesema,Serikali inatambua changamoto wanazopitia wafugaji hapa nchini. "Tatizo la malisho, maji, maeneo ya malisho kutumika kwa shughuli nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, tija ndogo ya shughuli za mazao ya mifugo na mengineyo.

"Mifugo sio laana au umaskini katika nchi yetu, mifugo ni utajiri katika nchi yetu.Mimi (Waziri Dkt.Mwigulu) nimesomeshwa kwa mifugo, bado nakumbuka hata rangi na majina ya ng'ombe waliouzwa.

"Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itafanya tathmini ya kina kwa utaratibu ambao utakuwa shirikishi kwa kuwashirikisha wafugaji nchi nzima kupata namna bora ya kujenga na kuimarisha usimamizi wa maeneo ya ufugaji na miundombinu ya mifugo sambamba na kutekeleza mapendekezo yaliyowasilishwa na wizara ya kisekta kuhusu kuboresha sekta ya mifugo.

"Kuna mabadiliko makubwa yanakuja kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi ili kuziwezesha sekta hizi ziweze kuchangia kwa kasi jitihada za kupunguza umaskini kwa watanzania na kukuza Pato la Taifa,"amesisitiza Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news