Funguka paza sauti yako yashika kasi Musoma

NA FRESHA KINASA

HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara kwa kushirikiana na Shirika la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) wameendelea kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya mialo kupitia mradi wa 'Funguka Paza Sauti kutokomeza ukatili wa Kijinsia'.
Ni mradi unaofadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society katika Kata ya Bwasi Kijiji cha Kome Wilaya ya Musoma mkoani Mara. 

Mradi huo wa 'Funguka Paza Sauti kutokomeza ukatili wa Kijinsia' ulianza kutekelezwa kuanzia mwaka jana mwezi Septemba katika Wilaya ya Musoma na Bunda na ulimalizika mwezi Aprili, 2023 ukiwa na thamani ya shilingi milioni 37 awamu ya kwanza

Ambapo pia umepata mwendelezo kuanzia mwezi Juni, 2023 na utamalizika mwezi Oktoba 2023 kwa awamu ya pili ukiwa na thamani ya shilingi milioni 22 chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society. 

Lengo ni kuimarisha ushiriki wa wananchi na jamii kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikifanyika bila kuripotiwa na pasipo kujali kwamba vinakiuka haki za binadamu pamoja na sheria za nchi. 
Elimu hiyo imetolewa kwa wananchi hao Julai 25, 2023 ambapo imeenda sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzuia kuzama maji duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Julai 25 ambapo wavuvi kutoka Kata ya Bwasi na Bukumi pamoja na viongozi wa serikali wameshiriki kwa pamoja na wananchi pia. 

Meneja wa Shirika la VIFAFIO, Majura Maingu amesema, nguvu ya pamoja inahitajika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya mialo kwa wananchi kushiriki kwa dhati katika mapambano ya vitendo hivyo bila kuvifumbia macho, kwani vinarudisha nyuma maendeleo na ustawi bora. 

Maingu ameongeza kuwa, shirika hilo litaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na Serikali kuona jamii inakuwa salama kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi na hivyo ameomba kila mmoja kuwa na ushiriki wa dhati katika kuhakikisha vitendo vya ukatili vinatokomezwa. 

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Musoma,Abel Gichaine amesema, ukatili mwingi umekuwa ukijitokeza kwenye maeneo mawili mgawanyo wa rasilimali usio sawa na uwezo. 

"Matumizi mabaya ya uwezo alionao mtu wakati mwingine ni chanzo cha ukatili katika jamii. Na suala la ukatili huwa lina muendelezo, mtu anapokuwa na uwezo asiwatendee wengine wasio na uwezo vitendo vya ukatili. 
"Maana unayemtendea ukatili leo kwa baadae atakuwa na uwezo wa kuwafanyia wengine tena kwa kiwango kikubwa sana.

"Kuna ukatili wa kimwili,kingono, kisaikolojia, na kiuchumi hizi zote ni aina za ukatili ambazo zipo kwenye jamii yetu. 

"Ukatili wa kisaikolojia umekuwa ukifanywa sana kwa njia ya lugha chafu mfano mama kumtolea lugha chafu mwanaye au baba kumtolea lugha chafu mkewe athari zake hujirudia rudia katika fikra ya kuathiri afya ya akili,"amesema Ginchaine na kuongeza kuwa.

"Ukatili wa kiuchumi mara nyingi hufanywa na kina baba, mama anaweza kumwezesha baba kufanya uzalishaji vizuri, lakini anapopata mafanikio humuacha mama na watoto na kutumia rasilimali aliyopata yeye binafsi wakati kabla ya mafanikio mama aliwajibika. 

"Na ukatili wa kimwili huambatana na kutoa vipigo kwa kwa mama na madhara yake ni mabaya huweza kuleta ulemavu na madhara mengine." 

Sambamba na hilo, amesema kuwa, kuna ukatili wa kingono huhusisha vitendo vya ubakaji, ulawiti. Na hivyo amewataka wananchi hao kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na viongozi wachukue hatua za kisheria kwa wote wanaofanya ukatili na kutelekeza watoto. 

Pia amewataka wananchi wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoa taarifa polisi, dawati la jinsia na watoto, ofisi za watendaji wa kata, Serikali za mitaa na kuachana na mila na desturi, mfumo dume, na sababu mbalimbali zinazochangia ukatili kuendelea kufanyika.
Diwani wa Kata ya Bwasi, Maregesi Mbogora amelishukuru Shirika la VIFAFIO kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi ambayo imewapa uelewa wa jinsi ya kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

"Nafurahi nimefahamu kumbe kutoa lugha isiyofaa pia ni ukatili, sikuweza kufahamu, lakini kupitia elimu hi nimefahamu na hivyo nitasaidia kuelimisha wengine. Kwa sababu ukatili kweli upo lazima tuunge mkono juhudi za shirika hili na Serikali kutokomeza,"amesema Neema Bwire. 

Naye Rhoda Paul amesema kuwa, kutolewa kwa elimu hiyo kutasaidia jamii kuwa salama na kuwa na ari ya kuwafichua wanaofanya vitendo vya ukatili bila woga, kwani watakuwa na ujasiri wa kutoa taarifa hizo katika vyombo vya dola.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news