Hongera kwa kutambuliwa

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye amesema,wizara hiyo imejipanga kimkakati katika mwaka wa Fedha wa 2023/2024 kuleta mabadiliko makubwa ya huduma za habari, mawasiliano na TEHAMA nchini zenye tija kwa watumiaji wote nchini.

Aliyasema hayo jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha viongozi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara yake jijini Arusha.

Mheshimiwa Nape alisema kuwa,katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 wizara itatekeleza mambo kadhaa ambayo yataboresha huduma za mawasiliano nchini na kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma hizo nchini.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na utekelezaji wa Mkakati Mawasiliano wa Taifa kwa Umma,kutekeleza kwa ufanisi Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali,kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma zote zinazotolewa na Serikali na taasisi zake kwa kutumia namba maalumu ya utambulisho atakayopewa kila mwananchi na mengineo.

Aidha, kikao kazi hicho ambacho kilianza Julai 19 hadi Julai 22, 2023 kiliikutanisha wizara na taasisi zake zote wakiwemo viongozi wake.

Kupitia, kikao hicho Mheshimiwa Waziri Nape alimtunuku tuzo na cheti cha pongezi Mjumbe wa Baraza la Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU Council) kwenye mkutano wa ITU 22,Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt.Nkundwe Mwasaga. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande ana neno la muhimu kwa Dokta Mwasaga kwa hatua hiyo. Endelea;


1.Mtu akifanya vema, mpeni pongezi zake,
Kwa nchi atenda mema, akifanya kazi zake,
Tanzania yatajwa vema, zile jitihada zake,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

2.Tumemuona Waziri, akifanya kazi yake,
Kwamba wako umahiri, unatufanya tucheke,
Kupata nafasi njema, tukupe na ushairi,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

3.Serikali yathamani, hawa wazalendo wake,
Ambao wako makini, kwenye majukumu yake,
Ni hapa na duniani, vema wafanya makeke,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

4.Kwamba ulichakarika, bilabila tusitoke,
Pazuri ukaiweka, Tanzania isikike,
Sasa inaeleweka, nafasi tuitamke,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

5.Mambo ya kimataifa, bore Tizedi iwike,
Huko tuzipate sifa, tushiriki tusichoke,
Na tuchote maarifa, Tanzania iinuke,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

6.Mwasaga ni mzalendo, hebu acha utajike,
Unazidi piga mwendo, baraka zote ziteke,
Kwa maneno na vitendo, na sisi tufaidike,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

7.Nchi yetu ni wajumbe, kimataifa tufike,
Mawasiliano kumbe, sisi wajumbe tucheke,
Acha Nkundwe tumuimbe, lakini asibweteke,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

8.Nape Nnauye Waziri, hongera kwako zifike,
Wafanya mambo mazuri, hilo na lieleweke,
Jambo chanya kufikiri, Nkundwe atambulike,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

9.Heri tunakutakia, Ndugu waziri sichoke,
Na Dokta Nkundwe pia, fanya mengi turidhike,
Uzalendo Tanzania, ni muhimu tuinuke,
Dokta Nkundwe Mwasaga, hongera kutambuliwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news