Kisiwa cha Rukuba waishukuru Serikali, Prof.Muhongo

NA FRESHA KINASA

WAKAZI wa Kisiwa cha Rukuba kilichopo katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara kwa kushirikiana na Mbunge wao Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo na Serikali kwa ujumla, wamekamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya kufuatia kupanua zahanati yao ili waweze kupata huduma bora za afya kisiwani hapo. 
Kisiwa cha Rukuba kipo ndani ya Kata ya Etaro yenye vijiji vinne (Busamba, Etaro, Mmahare na Kisiwa cha Rukuba). Ambapo kina shule ya msingi yenye vyumba vya madarasa ya kutosha ikiwemo zaidi ya vyumba viwili, madawati yapo ya kutosha kwa wanafunzi wote na ofisi mbili za walimu zipo.

Aidha, Maktaba ya shule ipo na kila mwalimu amepatiwa makazi mazuri. Wana-Rukuba na Mbunge wao wa Jimbo wameanza ujenzi wa Sekondari hapo Kisiwani.

Kufuatia kukamilika kwa Kituo hicho cha Afya wakazi hao wameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na Wizara ya Afya iwapelekee wafanya kazi na Vifaa Tiba ili kituo hicho kianze kutoa huduma. 

Ambapo, wakazi katika kisiwa hicho wanataka wapunguze sana hali ya kusafirisha wagonjwa mahututi na mama wajawazito kwenye mitumbwi kwenda Musoma Mjini kwa matibabu. 

Hayo yamebainishwa leo Julai 8, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini. 
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Wakazi wa Kisiwa cha Rukuba waliamua kupanua Zahanati yao iwe Kituo cha Afya. Na upanuzi huo ulianza kutekelezwa kwa kutumia michango ya fedha na nguvukazi za wananchi na Mbunge wao, Prof Sospeter Muhongo. Huku serikali iKitoa fedha shilingi milioni 500.

"Wakazi wa Kisiwa cha Rukuba na viongozi wao wanaishukuru sana Serikali kwa kuwapatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya hapo Kisiwani."

"Kituo cha Afya kimekamilika na kipo tayari kutumika. Majengo manne na miundombinu yake yaliyokamilika ni mama na mtoto, maabara,upasuaji na ufuaji. Jengo la OPD litatumika lile la zahanati wakati jengo jipya likiwa linakamilishwa,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa, 

"Wakazi wa Kisiwani Rukuba wanaiomba Serikali kupitia OR-TAMISEMI na Wizara ya Afya iwapelekee wafanyakazi na vifaa tiba ili kituo hicho kianze kutoa huduma za afya kisiwani hapo.
"Wakazi wa hapo Kisiwani wanataka wapunguze sana kusafirisha wagonjwa mahututi na mama wajawazito kwenye mitumbwi kwenda Musoma Mjini kwa matibabu."

Shukrani

"Wananchi wakazi wa Kisiwa cha Rukuba na viongozi wote wa Musoma Vijijini wanaendelea kutoa shukrani zao za dhati kwa Serikali yetu na kwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za afya vijijini mwao."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news