Kiswahili Afrika Mashariki:Hebu kujeni na Sera

NA LWAGA MWAMBANDE

MEKACHA (2000:126) anafafanua kuwa, Sera ya Lugha ni jumla ya mawazo, matamko, sheria na taratibu zenye kuelezea taratibu za utekelezaji wa mabadiliko ya nafasi na matumizi ya lugha katika jamii.

Aidha, dhana hii ya sera ya lugha ina uhusiano wa karibu sana na dhana ya mpango lugha, dhana ambayo kwa mujibu wa Rubin na Jernudd (1971), ina maana ya jumla ya matukio, shughuli, au hatua mbalimbali za wazi na zisizo za wazi zinazochukuliwa hasa na dola kwa makusudi.

Lengo likiwa ni kuleta mabadiliko au kusitisha mabadiliko katika jamii kuhusiana na taratibu za matumizi ya lugha.

Wataalamu wa lugha wamefikia hatua kutaka kuona ndani ya Taifa letu na Jumuiya ya Afrika Mashariki tunakuwa na sera toshelevu ya lugha ya Kiswahili ambayo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wana Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ili lengo la kukifanya Kiswahili kuendelea kuenea na kusambaa kwa kasi zaidi ndani na nje ya Tanzania, ndani ya Afrika Mashariki kuna umuhimu wa kuja na sera. Endelea;


1:Jumuiya yetu hii, hebu kujeni na sera,
Ili kwamba lugha hii, itumike kwa ubora,
Kwa sababu hali hii, kwa sehemu inakera,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

2:Imesemwa jana hii, lugha inakosa sera,
Ambayo tungeitii, kienee pwani bara,
Hakiki hatutulii, hadi tuipate sera,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

3:Duniani lugha hii, imeonekana bora,
Hata siku twaitii, iliyopigiwa kura,
Vipi jumuiya hii, iko hasarahasara?
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

4:Lugha yapendeza hii, kutamkwa ni ishara,
Wenyeji na watalii, kusema yatia for a,
Ila hatushangilii, kwa kukosekana sera,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

5:Kama jumuiya hii, ikaiandaa sera,
Itafanya lugha hii, itumike kwa ubora,
Nchi zote kanda hii, wawe na mipango bora,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

6:Changamoto kanda hii, lugha nyingi ni taswira,
Kuirasimisha hii, kwingine kama ukora,
Kwa sababu kanda hii, imekosekana sera,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

7:Shime inakuja hii, kwa wote watunga sera,
Hii changamoto hii, isizidi kutukera,
Wito huo tuutii, hebu itungeni sera,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

8:Twajua dunia hii, Kiswahili lugha bora,
Kwanini hatukamii, kizidi kuuza sura?
Malengo hatufikii, tunakwamisha ajira,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

9:Kwa lugha hatukawii, kupatana si kufura,
Tangamano kanda hii, utazidi kuwa bora,
Na elimu yetu hii, itakuwa barabara,
Afrika Mashariki, kitumike Kiswahili.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news