Mlima Kilimanjaro, Simba inaunga'arisha

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo ni sehemu ya baraka iliyokirimiwa na Mungu kuanzia bara hadi visiwani.

Vivutio hivyo, licha ya kuchochea pato la Taifa, pia vimekuwa sehemu kubwa ya kufungua fursa za ajira za kudumu na za muda kulingana na maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa vivutio hivyo, ambavyo popote utakaposimama duniani na kuvitaja kila mtu lazima atamke hiyo ni Tanzania ni pamoja na Mlima Kilimanjaro.

Huu ni mlima ambao umezungukwa na uoto wa asili wa misitu huku ukipambwa na wanyama mbalimnbali wa kuvutia.

Mlima Kilimanjaro ndio mlima mrefu zaidi barani Afrika wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,340).Aidha, pamoja na safu zake tatu za volkeno za Kibo, Mawenzi na Shira ndio mlima mrefu kuliko yote duniani uliosimama peke yake na unaojitegemea.

Huu mlima unaweza kufikika kupitia njia za Rombo, Hai na Moshi ambapo kilele cha Kibo kina urefu wa futi 19,340 (mita 5,895) ambacho ndio killele kirefu katika mlima huo.

Ikumbukwe, Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), ilianzishwa mwaka 1973 pia mlima Kilimanjaro uliteuliwa kuwa eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO mwaka 1987.

Historia inaonesha kuwa, mtu wa kwanza wa kufika katika kilele cha mlima huo alikuwa, Johannes Kinyala Lauwo kutoka Marangu aliyewaongoza Wajerumani, Hans Meyer na Ludwig Purtscheller mnamo Oktoba 6, 1889 wakati wa ukoloni wa Ujerumani.

Safari ya kupanda mlima huo humpitisha mpandaji katika kanda za hali ya hewa tofauti kuanzia ile ya nchi za Tropiti hadi Aktiki.

Mshairi wa kisasa, Lwanga Mwambande anasisitiza kuwa, heshima walioitoa Klabu ya Simba kuutangaza Mlima Kilimanjaro kupitia 'kibegi cha Simba' inapaswa kuigwa na wengine kwa manufaa mema ya kukuza utalii wa taifa letu. Endelea.


1.Hiki kibegi cha Simba, nchi kimeshaiteka,
Ajenda hasa ni Simba, kileleni wakifika,
Mlima unaotamba, bara letu Afrika,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

2.Kibegi umaarufu, mengi kimeyafunika,
Wengi ambao twasifu, kwa ubunifu hakika,
Wengine kinawakifu, wabaki waweweseka,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

3.Tayari historia, Simba imeshaandika,
Watu watakumbukia, mipango ya kutukuka,
Ambayo twafurahia, utalii wainuka,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

4.Tena tunafurahia, internet imefika,
Hivyo tunaangalia, pote pale wanafika,
Jezi tukisubiria, zikiisha tambulika,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

5.Hongera timu ya Simba, maarufu Afrika,
Kati ya nane miamba, Super Cup Afrika,
Tanzania inatamba, watalii watafika,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

6.Miaka nyuma mitano, juujuu yasikika,
Kwenye makundi ni wino, huko ulishamwagika,
Sasa mbele liko neno, kwamba izidi inuka,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

7.Usajili mwaka huu, ule wa kuaminika,
Wa hapa na wa majuu, wote wanaeleweka,
Yale malengo makuu, yapate kutimilika,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

8.Hongera kwa viongozi, rekodi mnayoweka,
Mmeyafanyia kazi, haya yanayosikika,
Siyo siri yako wazi, hata kwa wasowataka,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

9.Heri tunawatakia, kileleni mkifika,
Kazi mkitufanyia, kwa salama mweze shuka,
Tuwaweze kufurahia, msimu mpya kufika,
Mlima Kilimanjaro, Simba inaung’arisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news