NHC:Neema kubwa inakuja Kariakoo

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema, uwekezaji ambao unatarajiwa kufanywa na shirika hilo kwa ubia katika maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam utakuwa neema kubwa zaidi kwa Watanzania kuanzia makazi, maeneo ya biashara na ofisi.

Abdallah ameyabainisha hayo Julai 5, 2023 baada ya kufanya ziara katika Banda la NHC lililopo karibu na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Bodi ya Kahawa nchini ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki katika maonesho hayo.

NHC wanashiriki Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba kuanzia Juni 28, 2023 hadi Julai 13, 2023 ndani ya viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (SabaSaba) vilivyopo Barabara ya Kilwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

"Tunakwenda kutengeneza neema kwa Watanzania wengi zaidi, nizungumzie eneo la Kariakoo ambalo tunakwenda kutengeneza makazi, maeneo ya biashara na ofisi zaidi ya 1500, kwa hiyo kutakuwa na ongezeko la kutoka 200 mpaka 1500.

"Hii ni neema kubwa, kuna watu ambao wanapisha hii miradi iweze kufanyika na niwatoe hofu Watanzania, mwanzoni kulikuwa na kelele na tulikuwa tunatarajia baadhi ya kelele kwa mtu ambaye ameweza kukaa kwenye nyumba takribani miaka 30 hadi 40.

"Leo hii ukamwambia hakupishe, atakapopokea ile taarifa itakuja na mtikisiko kidogo. Kwa mujibu wa sheria ya nchi, tunatakiwa tutoe mwezi mmoja kwa mpangaji kuweza kupisha, lakini kwa mujibu wa mikataba ambayo tumekubaliana na hao wapangaji ni miezi mitatu.

"Lakini, bado walikuja wakaomba muda zaidi, tumeweza kuwaongezea, sasa hivi tumetoa jumla ya miezi saba, maana yake mpaka itakapofika mwisho wa mwezi Desemba, mwaka huu.

"Na tumekuwa na vikao mbalimbali na wale wawakilishi kwa sababu si rahisi kukutana na wapangaji wote 200 kwa eneo la Kariakoo, tumekuwa na wawakilishi takribani 20 wa wapangaji na tayari nimeshafanya nao mikutano mitatu.

"Na nimejiwekea utaratibu pamoja na kuwa na ratiba ngumu sana, lakini kila mwezi nitakuwa ninafanya mikutano mitano na wapangaji ambao wanapisha maeneo ambayo tunafanya ubia, moja kuweza kuwafahamisha haki zao.

"Lakini, bahati nzuri haki za wapangaji wetu zipo kwenye mikataba yao ambayo tulisaini nao. Wote wanafahamu na wakaridhia na wakasaini.

"Tunachofanya sasa hivi ni kwenda nje...kwa sasa tunachotumia ni jicho la kibinadamu ambapo Mheshimiwa Rais (Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) vile vile amekuwa anatusihi viongozi mbali na sheria, vile vile viongozi tuwe na jicho la kibinadamu.

"Tunaposhughulikia baadhi ya vitu, kama hiyo kuongeza muda mpaka miezi saba ni jicho la kibinadamu. Jicho la sheria ni mwezi mmoja, lakini vile vile haki ya mpangaji yeye pale ambapo miradi imefanyika watarejea nini?.

"Commitments ambayo nimewapa mimi wale wapangaji wote wazuri na walikuwa wakilipa kodi zao kwa wakati, sisi tunatwaka wapangaji wazuri, kwa nini tuwaache barabarani tungependa kuendelea nao hao wapangaji wazuri, kwa hiyo hilo ndiyo jambo ambalo tunazungumza jinsi gani tunaweza kuwahudumia baada ya miradi kukamilika.

"Kwa hiyo hilo niwatoe hofu, tunaliangalia na tunaliangalia kwa umakini mkubwa sana.Na Watanzania wengi wamekuwa wakiuliza na hii ni kutokana na sheria tuliyo kuwa nayo zamani mfano Sheria ya Ukomo wa Kodi.

"Zamani ile sheria ilikuwa inataka unapofanya ujenzi, moja lazima umtafutie mpangaji makazi mbadala, lakini pili ilikuwa inataka wakati wa notisi yule mpangaji akae bure bahati nzuri au mbaya ile sheria ilifutwa mwaka 2005.

"Ninasema bahati nzuri kwa shirika na waendelezaji wengine wa makazi, lakini bahati mbaya kwa wale ambao ni wapangaji.

"Sheria ilifutwa mwaka 2005, kwa hiyo kwa sasa hivi wakati wa notisi wapangaji wanatakiwa kuendelea kulipa kodi zao kama kawaida na huenda rekodi zao za mwisho zikatupa nguvu zaidi kuwapatia maeneo mbadala baada ya ujenzi kukamilika,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah.

Fursa ya Ubia

"Fursa ya ubia,ipo wazi kwa nchi nzima, bahati nzuri Shirika la Nyumba kwa Tanzania bara tuna viwanja, tuna ardhi maeneo yote ya Tanzania, ukisema Masasi tuna viwanja, ukisema Kigoma tuna viwanja hata pembezoni kabisa mwa nchi tuna viwanja, mpaka Mtukula kule ambako ni mpakani tuna viwanja.

"Na tumetoa fursa ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali, sasa inategemea na mvuto vile vile wa wawekezaji wanataka maeneo gani, lakini maeneo ambayo yameonesha mvuto mkubwa sana ni maeneo ya Kariakoo.

"Lakini, vile vile tumepata wabia Mwanza, maeneo ya Arusha vile vile, na tulitangaza maeneo ya ubia mpaka Shinyanga na mikoa mingine, lakini ambapo tumepata mwitikio wa awali ni mikoa ya Dar es Salaam, tumepata Arusha na tumepata na Mwanza.

"Je? Awamu ya kwanza ndiyo mwisho, hapana. Inawezekana tukawa tunakwenda kwenye phases kwa baadhi ya maeneo mfano sasa hivi maeneo kama Kariakoo miradi 16 kwa kuanzia miaka miwili ya kwanza inatosha, ili sasa iweze kutoa fursa miradi hiyo ifanyike.

"Tunapofanya awamu ya pili, kuwe tayari na maeneo ya kuweza kuwahamishia wale wapangaji ambao wanatumia hayo majengo ambayo tutayabomoa, kwa hiyo wale wa kwanza watakuwa wanatumia, kwa sababu itabidi watafute njia mbadala ya kufanyia biashara.

"Lakini, awamu ya pili kwa sababu tutakuwa, mfano miradi 16 tunaweza kupata maeneo ya biashara takribani 1500 ambayo itakuwa ni fursa kubwa sana, leo hii tunazungumzia tuna maeneo ya biashara takribani 150 na kidogo kwa sababu wapangaji ambao wataathirika kwenye miradi hiyo ni takribani 200.

"Siyo ile 10,000 au 1,000 ambayo watu walikuwa wakizungumza na kuwa kuna mtu mmoja amechukua miradi yote, hapana wamechukua makampuni ya Kitanzania ambayo yamepatiwa miradi.

"Kwa hiyo fursa ya uwekezaji kwa National Housing inaendelea na baadhi ya plots mpaka sasa hivi zipo wazi, kwa watu ambao wanahitaji kwa ajili ya uwekezaji wanatakiwa walete tu maandiko yao, tutayapitia na kama yatakuwa na tija kwa shirika na Taifa, tunaingia mikataba.Kwa hiyo maeneo yapo Tanzania nzima si Dar es Salaam peke yake,"ameongeza Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news