Taasisi za kidini nchini zakalia kuti kavu

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amesema kuna baadhi ya taasisi za dini zinajiendesha kinyume na tamaduni za Tanzania, hivyo zitachukuliwa hatua kali.

Waziri Masauni amesema hayo Julai 4, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao chake na viongozi wa mashirikisho na mabaraza ya kidini, ambapo alisema taasisi ambazo zinakwenda kinyume.

Alisema taasisi inaposajiliwa inapata udhamini kutoka kwa mdhamini wao, hivyo ni muhimu kujiridhisha wanapowachukulia dhamana ili wafuate yake yanayotakiwa.

Mhandisi Masauni alisema, serikali haiwezi kukubali na wamekuwa wakichukua hatua wale wote wanaokwenda kinyume cha sheria ya nchi, kimaadili, mila na desturi za nchi.

“Jeshi la Polisi lipo mtu akiiba anakamatwa na taasisi za dini na viongozi wa dini au unatumia dini...mtu yoyote atachukuliwa hatua simzungumzii huyo mtu mmoja na wengine wanaokiuka taratibu hatua zitachukuliwa kwa yoyote anayevunja sheria za nchi,”alisema Masauni.

Alisema, changamoto iliyopo kwa sasa ni kuanzishwa kwa taasisi za kidini pasipo kufuata sheria jambo hilo haliwezi kukubalika watawachukulia sheria.

“Zipo taasisi nyingi katika jamii yetu ambazo zinajiendesha pasipo kusajiliwa na hata uendeshwaji wake ni wa kutia mashaka. Nitoe wito tusaidiane katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kusajili jumuiya na vikundi,”alisema Masauni.

Alisema inapobainika kuna Jumuiya ama vikundi vya kidini ambavyo uendeshwaji wake ni wa mashaka ni vyema wakatoa taarifa kwa Ofisi ya Msajili katika kuzibaini ili kuweka jamii katika hali ya usalama na amani.

“Hivi karibuni nchi yetu imekubwa na viashiria vya uvunjifu wa maadili ya kijamii. Kwa niaba ya Wizara, napenda kuwashukuru na kuwapongeza viongozi ambao mlijitokeza na kukemea kwa uwazi vitendo ambavyo si utamaduni wetu na vinatweza utu wetu,” alisema Masauni.

Alisema vita dhidi ya uvunjifu wa maadili ni ya watu wote inatakiwa kupingwa pasipo kuoneana.

Masauni alisema serikali na taasisi za kidini kila upande ukitimiza wajibu wake anaamini jamii itakuwa salama.

“Nichukue fursa hii kuwasihi viongozi wetu wa kiroho kutoleta taaharuki katika jamii kutokana na mafundisho mnayoyatoa kwani yanaweza kutugawa katika kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili,”alisema Masauni na kuongeza kuwa;

“Sitaki kuonekana kama mwalimu au mtafasiri wa sheria, lakini sisi sote tunatambua kuwa serikali yetu haina dini isipokuwa watu wake wana dini na wanaamini katika Imani tofauti tofauti. Katiba yetu inatoa haki kwa Watanzania kuamini katika imanu waitakayo bila kuingiliwa ili mradi katika kutekeleza haki hiyo hawavunji sheria,”.

Aidha, alisema ili kuweka utaratibu mzuri kwa taasisi za kidini katika kujiendesha bunge limetunga sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya jumuiya sura ya 337.

“Sheria hii inahusika na kusajili na kusimamia jumuiya zote kwa ujumla wake ikiwemo na taasisi za kidini,”alisema Masauni.

Masauni alisema ni wajibu wao viongozi kuhakikisha jumuiya wanazoziongoza zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria kwa kutekeleza masharti ya usajili wa jumuiya wanazoziongoza.

Alisema masharti hayo ni kuwasilisha taarifa mbalimbali kila mwaka kama ilivyoelekezwa katika sheria na kulipa ada kwa wakati.

Masauni aliwataka kuzingatia masharti ya usajili na sheria zingine za nchi katika kuendesha shughuli za jumuiya wanazoziongoza.

Aidha, alisema hivi karibuni kumekuwa na migogoro mingi inayozikumba jumuiya za kidini na kutumia muda na rasilimali nyingi katika kushughulika na utatuzi wa migogoro badala ya rasilimali hizo na muda kutumika kuwahudumia waumini wao.

Alisema uchambuzi uliofanywa na Ofisi ya Msajili wa Jumuiya umebaini kuwa migogoro mengi inatokana na katiba ambazo ni za muda mrefu ambazo kwa mazingira ya sasa zinahitaji kufanyiwa marekebisho.

“Jambo jingine kutokuwa na uwazi katika mapato na matumizi ya taasisi, kugombea madaraka na viongozi na wafuasi au waumini kutokuwa na uelewa wa katiba yao na sheria zinazosimamia uendeshaji wa jumuiya,”alisema Masauni.

Alisema katika eneo la migogoro viongozi wa dini wanatakiwa kufanya mapitio ya katiba zao na kujiridhisha kama zinakidhi haja kwa wakati uliopo.

Masauni alisema kuna haja ya kujengeana uwezo wa kuzieleza katiba zao na miongozo iliyopo na kuendesha taasisi kwa kuzingatia katiba itasaidia kuepusha migogoro isiyokuwa na sababu.

“Pia katika kusimamia rasilimali za taasisi ni vizuri kuwa na uwazi ambao utawasaidia waumini au wanachama kujua jinsi mapato na matumizi ya taasisi yanavyotumika,”alisema Masauni.

Aidha, Masauni alisema kikao hicho kitasaidia kuibua changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ili serikali izifahamu na kushauriana kwa pamoja katika kuziondoa.

“Kikao hiki sio cha upande mmoja kwa maana nyie tutawasikiliza tutajadiliana kwa lengo la kujengana na kuimarisha. Naomba mjisikie kuwa huru katika mjadala tutakuwa na kikao kizuri ambacho si cha kunyosheana kidole bali kitakuwa ni kikao cha kujenga,” alisema Masauni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news