VIFAFIO, Musoma waimarisha ulinzi wa mtoto shuleni

NA FRESHA KINASA

HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara wamezindua Mwongozo wa Taifa wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa Mtoto ndani na nje ya shule katika shule za sekondari mbili na shule za msingi tatu zilizopo katika halmashauri hiyo. 
Shule hizo ni pamoja na Mtiro Sekondari, Nyanja Sekondari, Majita Shule ya Msingi 'A', Nyabaengere Shule ya Msingi na Msanja Shule ya Msingi. 

Uzinduzi huo umefanyika Julai 26, 2023 katika shule hizo kwa kuzingatia muundo wake wakiwemo walimu wawili wa malezi na unasihi upande wa Mtiro Sekondari na Nyanja Sekondari ambao wataratibu na kusimamia dawati hilo na wajumbe ambao ni wanafunzi 11 ambao wamechaguliwa kwa kuzingatia jinsi na mjumbe mmoja kutoka bodi ya shule. 

Huku upande wa shule ya msingi Majita 'A', Nyabaengere na Msanja shule ya Msingi wakichaguliwa wanafunzi 15 kwa kila shule kwa mujibu wa mwongozo huo, walimu walezi wawili na unasihi, wanafunzi wenye ulemavu wawili, pamoja na mwakilishi mmoja kutoka kamati ya shule ya msingi ambao watajumuika kuunda dawati hilo. 
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mratibu wa Shirika la VIFAFIO, Robinson Wangaso amesema kuwa, mwongozo huo ulizinduliwa na Serikali lengo kuu ukiwa ni kuweka mfumo wa ulinzi na usalama wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili shuleni na katika jamii. 

Aidha, Wangaso ameongeza kuwa, kupitia dawati hilo manufaa makubwa yatapatika ambayo yatasaidia kwa kiwango kikubwa kuweza kuimarisha mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia. 
"Tunatekeleza Mradi wa 'Funguka Paza Sauti kupinga vitendo vya ukatili chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society katika Wilaya ya Musoma na Bunda mradi huu pia umeweza kuwa chachu ya kusaidia jamii kuwapa uelewa kusudi washiriki kwa dhati kupinga ukatili, tumekuwa tukitumia matamasha kutoa elimu, kuimarisha mifumo Kama uundwaji wa madawati tukishirikiana na Halmashauri na mikutano ili elimu iwafikie watu wengi,"amesema Wangaso. 
Asteria John ambaye ni Mwalimu wa Malezi wa Dawati hilo katika Shule ya Sekondari Nyanja amelishukuru Shirika la VIFAFIO na Serikali kwa kuleta mwongozo huo ambapo amesema, utakuwa dira na chachu ya kuimarisha mapambano ya vitendo vya ukatili shuleni hapo, ili kuhakikisha wanafunzi wanaondokana na vitendo vya ukatili. 

Erasto Peter ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Nyanja amesema kwamba, kupitia mwongozo huo atajifunza mambo mengi yatakayomsaidia kutoa elimu kwa wenzake juu ya madhara ya vitendo vya ukatili na sehemu sahihi za kuripoti matukio ya ukatili. 
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mfawidhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Abel Gichaine amewataka wajumbe wa dawati la ulinzi na usalama wa watoto ndani ya shule na nje ya shule waliochaguliwa katika shule hizo, kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuhakikisha matukio ya ukatili yanashughulikiwa. 

"Tunataka kutokomeza aina zote za ukatili wa Kijinsia katika Jamii yetu upo ukatili wa Kimwili, wa kingono, kisaikolojia, kiuchumi na mara nyingi wenye uwezo wamekuwa wakiwafanyia ukatili wasio na uwezo hii ni mbaya sana. Na mara nyingi wanaofanyiwa ukatili pia na wao huwa wanakuja kuwa watendaji wakubwa wa ukatili kwa wenzao,"amesema Gichaine.
Pia amewaomba kuibuia matukio ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia kwa kuwasaidia wale ambao pia wanapitia katika vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwa mabalozi kwa wengine katika maeneo yao ikiwemo kutoa taarifa katika ofisi za serikali, kwa walimu, Polisi, dawati la Jinsia na watoto kwa lengo la kutokomeza ukatili. 

Gichaine ameishauri jamii kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, kwani vinarudisha nyuma maendeleo na kwamba ukatili ni kinyume cha sheria na haki za binadamu na una madhara mengi ikiwemo ulemavu na kuathiri afya ya kisaikolojia na magonjwa ya kuambukiza hasa vitendo vya ubakaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news