Wanawake tumieni ujuzi wenu kujiinua kiuchumi-Naibu Meya

NA RAHMA KHAMIS
Maelezo Zanzibar

NAIBU Meya Baraza la Manispaa Mjini, Khadija Ame amewataka wanawake kutumia fursa mbalimbali za mafunzo zinapotokezea zinazolenga kuwainua kiuchumi.
Mkufunzi Asha Abdalla Salim akiwaelekeza washiriki wa mafunzo ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kutengeneza pilipili ili kuweza kujiajiri,huko Skuli ya Mwembe makumbi Zanzibar.

Akizungumza na wanawake hao katika Skuli ya Muembemakumbi wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kujiari amesema, mafunzo hayo yatawasaidia kuwawezesha kujiajiri na kujiletea maendeleo katika jamii.

Pia, amesema kuna baadhi ya wanawake hawajishuhulishi na kitu chochote cha kuwaingizia kipato jambo linalorejesha nyuma jitihada za Serikali katika kupambana ili kuwawezesha kiuchumi.

Aidha, amewaeleza kuwa, iwapo wanawake watajiunga na vikundi mbalimbali vya ujasiriamali wataweza kujiongezea kipato na kjiimarisha.

"Tumieni ujuzi wenu kujiinua kiuchumi, kwani Serikali inatumia nguvu nyingi ikiwemo kuanzisha vikundi na kuwapatia elimu ya ujasiriamali hivyo tuzienzi nguvu hizi ili tujiletee maendeleo "alisisitizia Naibu Meya

Amesema dhamira ya Serikali zote mbili ni kuwainua wanawake kiuchumi hivyo aliwataka wanawake hao kuyafanyia kazi mafunzo wanayopatiwa ili kujikwamua kimaisha.

"Ni jambo zuri la kujivunia tunaona viongozi wetu wanafanya kazi kubwa katika kuleta maendeleo ikiwemo kujenga hospitali,barabara na viwanda,hivyo lazima tusifu mazuri tunayofanyiwa, kwani wao wako mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanaimarika kiuchumi,"alifafanua Naibu Meya huyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Meya amefafanua kuwa, Serikali kupitia Baraza la Manispaa Mjini wametenga kiasi cha shilingi milioni 284 kwa ajili ya wananchi hasa wanawake na vijana ili kuwawezesha kiuchumi hivyo amewataka wanawake kushikamana ili kufikia malengo.

"Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha pesa hizo zinapatikana kwa ajili ya kuwainua wanawake kimaendeleo,"alifahamisha Naibu Meya.

Naye Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mwanzilishi wa Shirika la Wanawake na Uchumi wa Viwanda Tanzania, Halima Saidi Mngite amesema kuwa, lengo la shirika hilo ni kukuza viwanda,kutoa mafunzo na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amefahamisha kuwa wanatarajia kua na viwanda vingi vya wanawake wa Tanzania ikiwemo viwanda vya chumvi, asali na mafuta ili kusaidia Serikali kupunguza tatizo la ajira nchini.

Mkurugenzi ameeleza kuwa, hatua ya kuanzisha shirika hilo linalofanya kazi na Serikali kwa kuwajengea uwezo wa kujitegemea ni baada ya kubaini kua wanawake wengi wamekua tegemezi kwa familia na Taifa kwa ujumla .

Ameongeza kuwa, wanawake wana mchango mkubwa katika jamii hivyo kupitia programu ya Zunguka na Mama Samia itasaidia kuwafikia wanawake wote Tanzania katika kuwapatia elimu ya kujiwawezesha kiuchumi.

Amefahamisha kuwa Serikali ya Muungano wa Tanzania inaaunga mkono juhudi za Shirika kutokana na kuona Shirika hilo linapambana katika kuwainua wanawake kiuchumi.

"Tumuunge mkono mama Samia Suluhu ili tusonge mbele kwani anaona juhudi zetu katika kuwapambania wanawake hivyo tuamke kwani maisha yamebadilika,tutoke katika maisha ya utegemezi,"aliwahimiza wanawake.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema, mafunzo yatawasaidia kujiinua kiuchumi na kuwataka wanawake wenzake kuacha kutegemea wanaume na badala yake kujishughulisha ili kuleta maendeleo.

Shirika la Wanawake na Uchumi wa Viwanda ni Shirika lisilo la Kiserikali limeanzishwa mwaka 2000 na linajishughulisha na kuwawezesha wanawake kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news