Waziri Mkuu:Diaspora tunzeni heshima ya Tanzania

*Awataka walitetee Taifa lao, watangaze fursa zilizopo nyumbani

ST.PETERSBURG-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wanadiaspora wa Tanzania wazingatie sheria za nchi wanazoishi ili waendelee kutunza heshima ya nchi yao.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea tuzo maalum ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Latifa Ismail ambaye ni Mhasibu wa Umoja wa Watanzania waishio St. Petersburg nchini Urusi wakati alipozungumza nao kwenye hoteli ya Lotte nchini humo, Julai 29, 2023.Tuzo hiyo ni yakumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa uongozi na utawala bora. Wa pili kushoto ni Katibu wa Umoja huo, Deogratias Kalulu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa wito huo wakati akizungumza na Watanzania waishio St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.

“Baadhi yenu mko hapa mnatafuta fursa, na wengine wengi wako hapa kwa masomo. Zingatieni sheria za nchi hii, tunzeni heshima ya Tanzania. Teteeni Taifa la Tanzania, zungumzieni fursa zilizopo nyumbani,” alisema Waziri Mkuu

Akisisitiza umuhimu wa kukitangaza Kiswahili, Waziri Mkuu alisema: “Kiswahili kiendelee kutangazwa kwa bidii kwani Kiswahili ni fursa na Kiswahili ni ajira. Tukitangaze Kiswahili na tushike nafasi za kutangaza lugha yetu kwa kasi kwa sababu tuna historia ya muda mrefu na Urusi ambao wamekuwa wakitumia lugha hii,” alisema.

Alisema katika baadhi ya vikao vyake na wawekezaji wa Kirusi, hakupata shida ya mkalimani kwa sababu walikuwa na mtu wao ambaye anatafsiri moja kwa moja kutoka Kirusi kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda Kirusi. “Lakini na sisi ubalozini kwetu tuna Afisa Uchumi ambaye alitusaidia kutafsiri Kiswahili kwenda Kirusi kwenye baadhi ya vikao. Tena aliongea kwa ufasaha zaidi. Tusiache fursa hii itupite,” aliwasisitiza.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapa picha halisi ya maendeleo na kiuchumi yanayofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, maji na akawahakikishia kwamba Tanzania iko salama, wao waweke bidii kwenye masomo yao.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk alisema mbali na kazi ya kudumisha mahusiano ya kirafiki na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya Diaspora.

“Hivi sasa, wizara imekamilisha Mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, ambayo inajumuisha masuala ya Diaspora. Ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa takwimu sahihi za idadi ya Diaspora wetu kote ulimwenguni, tarehe 22 Mei, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax alizindua rasmi Mfumo wa Kuwasajili Diaspora Kidigitali. Mfumo huo, uliotengenezwa na Wataalam Wazawa utasaidia kurahisisha usajili wa Diaspora wenye asili ya Tanzania pamoja na wanafunzi.”

“Ni dhahiri kuwa Diaspora waliopo katika eneo zima la uwakilishi wa ubalozi wetu hapa Urusi, sasa hawatalazimika tena kusafiri kwenda ubalozini Moscow ili kujisajili. Napenda kutumia fursa hii kuwahamasisha Diaspora wote wajisajili kwa wingi.”

Alisema ana imani kuwa takwimu zitakazopatikana kupitia mfumo huo, zitaiwezesha Serikali kupanga na kuandaa kwa usahihi mahitaji yanayohitajika ili kuwapatia Diaspora huduma wanazozihitaji, ikiwemo huduma za kibenki, Hati za Kusafiria, Vitambulisho vya Taifa na vitambulisho rasmi vya utambuzi wa diaspora wakati wa utekelezaji wa Hadhi Maalum.

“Hadi sasa, mfumo huu umetuwezesha kufahamu kuwa tunao diaspora wenye asili ya Tanzania katika nchi za Vanuatu, Albania, Antigua na Barbuda, Kazakhstan, Azerbaijan pamoja na America Samoa ambazo nchi yetu haina uwakilishi wa Kibalozi,” alisema.

Akisoma risala yao, Mwenyekiti wa Diaspora katika Shirikisho la Urusi na Nchi huru za Jumuiya ya Madola (CIS), Pascal Gura alisema jumuiya yao (TADRU- CIS), ina wanachama zaidi ya 200 walioko sehemu tofauti za nchi hiyo.

Alisema kwa sasa wanadiaspora hao wanakabiliwa na changamoto ya mifumo ya kifedha kutokana na vikwazo vya kiuchumi. “Changamoto hii inatokana na Shirikisho la Urusi kuondolewa katika mfumo wa uhamishaji fedha (Swift) ambao unatumiwa na mabenki kupitia kadi za ‘‘Visa na Master card’’.

“Kwa sasa kadi pekee zinazokubali katika baadhi ya mabenki katika Shirikisho la Urusi ni kadi zinazotumia mfumo wa Union Pay. Hivyo, tunaomba benki za Kitanzania zipanue wigo kwa kutoa kadi zenye mfumo wa Union Pay kwa kuwa itaimarisha pia fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Urusi,” alisema.

Wanadiaspora hao pia walimkabidhi Waziri Mkuu tuzo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutambua juhudi zake katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news