CRDB yaanza kuuza Hatifungani ya Kijani

DAR ES SALAAM-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha zama mpya za uwekezaji endelevu nchini.
Ambapo imekuja na Hatifungani ya Kijani (Green Bond) ambayo ni ya kwanza nchini na kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara huku uuzaji wake ukianza leo.

Uzinduzi huo wa kihistoria ambapo Prof.Mkumbo alikuwa mgeni rasmi umefanyika leo Agosti 31, 2023 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, mbele ya wageni waalikwa pamoja na viongozi mbalimbali.

Katika hotuba yake Mhe. Prof. Mkumbo alitambua jukumu la Benki ya CRDB katika kuzipatia taasisi za ndani njia ya kutumia uwezo wa kubadilisha hatifungani za kijani kwa ustawi bora. 

Alisisitiza nafasi ya Serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuimarisha sera, sheria na kanuni zilizopo.

"Benki ya CRDB tayari imekuwa mfano wa kuigwa,"amesema. Kutolewa kwa Hatifungani ya Kijani,kunaashiria hatua kubwa ya kufikia Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Tanzania 2020/21-2029/30, mwongozo wa kimkakati wa kuwezesha sekta ya umma na binafsi kwa ajili ya ustawi mkubwa wa watu."

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo,Abdulmajid Nsekela kwenye mkutano huo wa kuanza wa kuuza hatifungani hiyo amesema kuwa, Agosti 18, 2023 ilikuwa siku moja ya siku za furaha sana kwa Benki ya CRDB;

Baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwapa idhini ya kuuza hatifungani ya kwanza ya kijani Tanzania na kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akikabidhi Kitabu kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kuanza kutoa hatifungani ya kijani "green bond" yenye jumla ya thamani ya dola za kimarekani milioni 300 sawa na Shilingi bilioni 780 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni ya kwanza kutolewa Tanzania na ya kwanza kwa ukubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara, katika hafla iliyofanyika leo kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (watatu kushoto), Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Robert Mshiu (wapili kushoto) pamoja na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mary Mniwasa.

"Lakini naweza kusema leo tupo katika kilele cha furaha kwa kuwa sasa tunakwenda kuaza kuunza hatifungani yetu ya kijani au “Green Bond” ambayo inalenga kukusanya fedha zitakazofanikisha miradi yenye mrengo wa kuhifadhi mazingira.

"Hivyo kuifanya Tanzania iendane na mikakati ya Dunia ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi."

Mkurugenzi Mtendaji huyo amefafanua kuwa, kukamilika kwa mchakato huo ulioanza mapema mwaka jana ni mafanikio makubwa kwao, kwani wataalamu wao wa ndani na nje ya benki hiyo walilazimika kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha taratibu za kikanuni na kisheria. 

"Lakini jitihada hizi zisingefaa kitu kama si ushirikiano ambao tulipata kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ambao hawakuchoka kutupa miongozo mpaka leo hii tunaanza kuiuza hatifungani yetu.

"Kufanikiwa kuanza kuuza hatifungani hii kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni heshima kwa nchi yetu kwa kuwa Benki ya CRDB ni benki ya kizalendo inayomilikwa na Mtanzania mmoja mmoja, 

"Serikali pamoja na taasisi zake. Na hili linaendelea kudhihirisha kuwa taasisi zetu zina uwezo wa kufanya mambo makubwa katika ulingo wa kimataifa."

Nsekela amesema kuwa, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini ikiwemo Benki ya CRDB katika uwezeshaji wa miradi inayojali mazingira, bado jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinaendelea.

Pia amesema,mahitaji ya uwezeshaji wa miradi yenye mrengo huo ni makubwa, kwani miradi mipya inabuniwa kila siku kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

"Kwa kutambua umuhimu na mahitaji yaliyopo, Benki ya CRDB iliona ni muhimu kutafuta vyanzo vipya vya fedha ili kuwezesha miradi hii ndipo lilipopatikana wazo la hatifungani ya kijani. 

"Hatifungani hii ambayo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetupa idhini ya kuiuza ina thamani ya dola milioni 300 za Marekani sawa na takribani shilingi bilioni 780 za Tanzania ambayo kama nilivyosema awali hii ni kubwa zaidi kuwahi kutolewa katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara." 
Amesema, hatifungani hiyo itakayoorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Soko la Hisa London yaani London Stock Exchange (LSE), wanatarajia kuiuza kwa awamu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema,katika awamu hii ya kwanza mauzo yanaanza leo Agosti 31, 2023 na yatadumu kwa siku 37 ambapo wanatarajia kukusanya shilingi Bilioni 55. 

"Hivyo kufanikiwa kuuzwa kwa hatifungani kwa hii kutakwenda kuiongezea uwezo mkubwa benki yetu kuwezesha wawekezaji ambao miradi yao katika namna moja au nyingine inasaidia katika utunzaji wa mazingira. 

"Na hili ni eneo ambalo tumeshuhudia mataifa mengi duniani yanawekeza huko ambapo hapa Afrika tayari nchi kama Afrika Kusini, Ghana, Nigeria na Kenya tayari wamepiga hatua kubwa."

Nsekela amefafanua kuwa,licha ya heshima iliyoipa nchi yetu na faida zake kwa mazingira ya nchi yetu na dunia kwa ujumla, hatifungani ya kijani ambayo inakwenda kuuzwa na Benki ya CRDB ni uwekezaji ambao iwe mtu binafsi, 

Kampuni, shirika au taasisi inaweza kuwekeza kwa kianzio cha shilingi 500,000 tu. 

"Hivyo, tofauti na wengi wanavyodhani huu ni uwekezaji ambao hata Mtanzania wa kawaida anaweza kuwekeza na kunufaika nao."

Sambamba na hilo, Nsekela amesema kuwa, hatifungani hiyo ya kijani ni uwekezaji ambao una uhakika wa kukulipa au kwa lugha ya kigeni wanasema “risk free investment”. 

"Kupitia uwekezaji wa hatifungani ya kijani ya Benki ya CRDB, muwekezaji atakua na uhakika wa kupata riba ya asilimia 10.25 ambayo ni biashara chache sana ambazo unaweza kuzifanya na ukawa na uhakika wa kupata kiasi hiki tena bila kujali mazingira ya biashara yatakuaje."

Wakati huo huo, Nsekela ametoa shukrani kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa ushirikiano mkubwa waliowapatia hadi kufikia hatua hii ya leo. 
Lakini pia amewashukuru washirika wao Benki ya Stanbic Tanzania ambayo ni mshauri elekezi mkuu katika mchakato mzima, Kampuni ya Orbit Securities Company Limited ambayo ni wakala wao katika uuzajiwa hatifungani hiyo.

Pia, Kampuni ya Dentons EALC East African Law Chambers, washauri wao wa masuala yote ya kisheria, kampuni ya KPMG Tanzania ambao wawaongoza katika masuala yote ya kihasibu na Kampuni ya FSD Afrika ambao waliratibu muundo wa hatifungani hiyo kabla ya kufanyiwa mapitio na Kampuni ya Sustainalytics. 

"Lakini nitakua mchoyo wa fadhila endapo sitotoa shukrani zangu kwa Idara yetu ya Hazina ya Benki ya CRDB pamoja na Kitengo cha Uwezeshaji wa Miradi Endelevu na Rafiki wa Mazingira kwa kazi nzuri ambayo wamefanya kusimamia mchakato huu wote kwa kushirikiana na wadau ambao nimetangulia kuwataja."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news