Endelezeni malezi bora-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameihimiza jamii kuendeleza malezi bora kwa watoto na vijana ili kulinusuru Taifa na mporomoko wa maadili.
Alhajj Dkt.Mwinyi ametoa nasaha hizo kwenye Msikiti wa Polisi Bomani, Mkoa wa Mjini Magharibi, alikojumuika pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.

Amesema, siku hizi maadili yamepotea, jamii zimekithiri vitendo visivyo na maadili mema kwa vijana ikiwemo wizi, watumiaji wa dawa za kulevya, tofauti na zamani, hivyo aliwahimiza wazazi/walezi kuwalea vijana kwa hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu (S.W).

Alieleza, ndani ya jamii kuna mmong’onyoko wa maadili, hivyo aliendelea kuiasa jamii kushirikiana kwenye malezi ya pamoja ili kuwanusuru vijana na janga hilo.

Alieleza wazazi na walezi wana wajibu wa kuhakikisha makosa na mporomoko wa maadili hayafanyiki kwa vijana wao kwa kuendelea kuwa wasimamizi wazuri kwao badala ya kusubiria vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria, hivyo aliwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari mapema.

Katika hatua nyingine, Alhajj Dkt.Mwinyi aliiasa jamii kuendelea kuvumiliana na kuendeleza amani ya nchi licha ya tofauti za kisiasa na imani zilizopo.

Alisema, ndani ya nchi yenye watu wenye mitazamo na fikra tofauti haiwezekani wote wakakubaliana kwa kila jambo, lakini kikubwa katika hayo ni kuvumiliana na kuelewana.

Aidha, Alhajj Dkt.Mwinyi aliwaomba wanasiasa wa vyama mbalimbali kupitia viongozi wa dini na waumini wao, kuendelea kubakia na amani na uvumilivu kwani wakati mwengine kumekua kukijitokeza viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutovumiliana kwenye jamii.

Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwataka waumini wa Dini ya Kiislam kuendelea kumuombea na kumtakia heri Alhajj Dk. Mwinyi kwani tokea ameingia madarakani amekua na ushirikiano mkubwa kwenye jamii kwa kuendeleza utaratibu wake wa kushirikiana na jamii kwenye masuala ya khairati ikiwemo kujumuika nao pamoja katika sala za Ijumaa kupitia misikiti ya maeneo mbalimbali ya nchi.

Akihutubia kwenye sala hiyo, Katibu Sheikh Salum Othman Malolo aliiasa jamii kujiepusha na zinaa ya macho kwa kuangalia na ya ulimi kwa kutamka machafu na kusifia maovu yanayofanyika kwenye jamii. Hivyo aliitaka jamii kutozingatia na kujiepusha kutamani masuala machafu ya zinaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news