Harakisheni na jengeni fikra mpya

ARUSHA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama ameitaka Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali kuharakisha kutengeneza Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama akikabidhi cheti kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa ofisi hiyo,Bi. Sakina Mwinyimkuu wakati Mkutano wa Mazingativu.

Sambamba na kukamilisha na kuzindua haraka Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini ndani ya nchi utakaotumika na Serikali kwa ujumla,wizara,taasisi na maeneo yote ya utendaji kazi ndani ya Serikali.

Ameyasema hayo Agosti 10, 2023 jijini Arusha alipofungua Mkutano wa Mazingativu uliohusisha viongozi, watumishi wa ofisi hiyo pamoja na taasisi zake.

Licha ya kuonesha imani wa Mkurugenzi wa Idara hiyo mpya, Waziri Mhagama aliitaka pia idara hiyo kuwa na ubunifu.
Picha ikionesha baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mazingativu, uliohusisha viongozi, watumishi na taasisi za ofisi hiyo na taasisi zake uliofanyika jijini Arusha tarehe 10 Agosti, 2023.

“Jaribuni kununua mifumo, miundo na taratibu za kufanya ufuatiliaji na tathmini kutoka kwenye mataifa mengine, ili tuweze kulitangaza Taifa letu kwa kazi hiii kuwa tunaweza kufanya vizuri,”amesisitiza Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama alisema anahitaji kupata taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Ofisi yake na Serikali kwa ujumla kwa kila robo mwaka ikiwa ni katika kuboresha eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu Uchapishaji wa Nyaraka za Serikali, Waziri Mhagama alisema katika eneo hilo, katika mwaka huu mpya wa Fedha 2023/2034, Serikali imejiwekea mkakati wa kuongeza maduhuli na mapato ya yake kupitia Mpigachapa Mkuu wa Serikali.

Waziri Mhagama amesema,ujenzi wa Mradi wa Mkakati wa kiwanda kipya cha Mpigachapa Mkuu wa Serikali umefikia asilimia 9 na wameshaanza kufanya manunuzi ya mashine za kisasa, "na tumeshafufua mashine ambazo zilikuwa zimeharibika."

"Nisisitize Chapa muendeshe kiwanda kwa ubunifu, jengeni fikra mpya, boresheni mifumo miundo na namna ya uhifadhi na uchapaji wa nyaraka za Serikali, natarajia kiwanda hiki kinaweza kikajiuza na kinaweza kikapata soko la nchi za Kusini mwa Afrika-SADC na katika na soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Picha ikionesha baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mazingativu, uliohusisha viongozi, watumishi na taasisi za ofisi hiyo na taasisi zake uliofanyika jijini Arusha tarehe 10 Agosti, 2023.

"Pale mnalo jambo na kazi kubwa ya kufanya, na mazingativu haya yawasaidie kujiongoza na kupata picha na fikra ambazo zitatuvusha,"alisisitiza Waziri Mhagama.

Akiongea katika mkutano huo wa mazingativu, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Dkt.Jim Yonazi alisema, kuwepo kwa ofisi hiyo jijini Arusha katika mkutano huo ni kutokana na nia ya ofisi hiyo kuhakikisha kwamba inatenda majukumu yake kwa umakini na kwa utimilifu ikiwa ni pamoja na uratibu wa shughuli za Serikali kwa ujumla na kwenye maeneo mengine.

“Tunaweza kujifunza kutoka hapa ndani ya nchi mambo mengi na tukatumia ubunifu na wataalam wa ndani katika utendaji na hakuna mtu anaweza kuwa mbunifu katika mazingira yenye stress, hivyo tunaweza kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi na kukuza na kuongeza uelewa katika utendaji.”alisema.

Kwa kutekeleza agizo la Mhe.Waziri Mhagama, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Ofisi hiyo, Bi. Sakina Mwinyimkuu alisema, kikosi kazi kitakaa haraka ili kuweza kuandaa mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini.

Pia kuhusiana na kuwa na Mfumo wa Ufuatiiaji na Tathmini, Mkurugenzi alisema kazi hiyo inafanyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Serikali Mtandao (eGa) na maandalizi ya kujengwa kwa mfumo huo yanatarajiwa kuanza.

Kwa upande wake Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Bw.George Lugome alisema, kama idara imejipanga hasa kwa watumishi kuhakikisha wanafanya kazi katika ubora wa hali ya juu na kuhakikisha, watumishi watapata mafunzo ya kuendesha mashine mpya za kisasa, kuongeza idadi ya watumishi wenye sifa na weledi katika eneo hilo la uchapaji.

"Ili kuweza kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ni lazima pia tuchape nyaraka za Serikali kwa kufuata ubora na kuweka alama za usalama kulingana na teknolojia zilizopo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.John Mongela akizungumza na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt.Jim Yonazi, na Naibu Katibu Mkuu Bw.Anderson Mutatembwa wakati wa Mkutano wa Mazingativu uliohusisha viongozi, watumishi na taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu.

"Na tumeshaanza mikakati ya namna gani ya kushirikiana na wenzetu wenye utaalamu wa masuala ya usalama katika nyaraka mbalimbali,”alifafanua.

Mada mbalimbali zinawalishwa katika mkutano huu wa mazingativu huku matarajio ya washiriki wengi yakiwa ni mkutano huo utawasaidia kuboresha utendaji wa kazi, kujifunza, kupata ubunifu katika maeneo yao ya kazi, kuongeza bidii zaidi na hali ya utendaji katika kazi unaoendana na sayansi na teknolojia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news