Msivae jambakoti la uzembe, msivae misurupwete ya uvivu

NA ADELADIUS MAKWEGA

JUMAPILI ya 18 ya mwaka A wa Liturjia ya Kanisa, Agosti 6, 2023 katika Kanisa la Ekaristi Takatifu, Parokia ya Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga kumefanyika adhimisho la misa takatifu ya dominika.

Ni misa iliyoambatana na kutolewa kwa sakramenti mbalimbali za Kanisa Katoliki ikiwemo Ubatizo, Komuniyo ya Kwanza na Kipaimara kwa vijana karibu arobaini huku Wakristo Wakatolki na wa madhehebu mengine wakishiriki.

Akiongoza adhimisho la misa hiyo Padri Richard Masanja alipigia chapuo wajibu wa kila mzazi na mlezi kutimiza majukumu yake ya malezi bila utoro,

“Leo tunawapatia watoto na vijana hawa sakramenti mbalimbali, wazazi msibweteke, mkasema ooooh sasa mimi nimemaliza kazi, ebo haujamaliza kazi baba!.

"Haujamaliza kazi mama, nakwambia sasa kazi ndiyo imeanza. Siku hizi ukipita katika maeneo mbalimbali utasikia’daa walimu wa siku hizi bwana! daa hawa viongozi wa siku hizi bwana.

"Daaa wachungaji wa siku hizi bwana! Daa mapadri wa siku hizi bwana. Jamani msiikwepe lawama. Hao walimu wa siku hizi, hao mapadri wa siku hizi na hao wachungaji wa siku hizi kama wamekengeuka tambueni kuwa wazazi wa siku hizi mmeshindwa kung’arisha sura zao wawe wema, jamani sikilizeni sauti ya Yesu.”

Padri Masanja ambaye anafanya shughuli zake za utume katika Shule ya Rosimini iliyopo Lushoto Mjini akiendelea kuhubiri katika misa hiyo aliwataka wazazi watambue,

“Watoto wanalelewa nyumbani, mzazi unasikia mtoto wako anatoa tusi kubwa alafu unakaa kimya, mwingine anasema mwanangu atakuwa mzungumzaji kweli.Ebo jamani hilo si sahihi, hayo siyo malezi , lazima umkanye mtoto huyo.”

Padri Masanja alilitupa jarife la maadili kwa sauti ya juu kwa kuitaja shida ya ushoga na usagaji, akisema kuwa jamii inaweza kupambana nayo vizuri tu kama wazazi au walezi watatimiza wajibu wao ipasavyo na siyo kutupiana lawama.

“Wazazi au walezi wa leo kila mmoja atambue dunia imebadilika, leo hii kama kaja mgeni nyumbani kwako, usiseme ‘mwanangu leo utalala na mjomba wako, au leo mwanangu utalala na shangazi yako,’ wazazi wa leo msiwaamini hata ndugu zenu.

"Leo tumewapa sakramenti watoto hawa halafu unafanya uzembe wa malezi. Leo wazazi msiruhusu hayo, hawa watoto tumewapa sakramenti wanahitaji malezi yenu.

"Msipotimiza wajibu wenu jamani tutapata mapadri mashoga, tutapata wakuu wilaya mashoga, tutapata walimu wasagaji. Hilo litasababishwa na sisi wenyewe.

"Tuwapatie maadili mema, tuwasaidie ili sura zao zing’ae vizuri. Wazazi au walezi tusivae majambakoti ya uvivu na uzembe katika malezi.

"Wazazi msivae misurupwete ya uvivu na uzembe katika malezi. Jamani kila mzazi ni mwalimu wa kwanza, tuvae vazi la kung’aa, tuwe na sura njema katika malezi ya watoto na vijana wetu ili tupate askari wema, tuapate wanajeshi wema, tuapate wanasheria wema, tupate viongozi wema, tupate mapadri wema, jamani sote tusikie sauti yake yeye.”

Mara baada ya mahubiri hayo Padri Masanja alitoa sakramenti zote tatu na wakati wa matangazo ya misa hiyo ulipowaidia waamini wa kanisa hilo walielezwa kuwa katika adhimisho la misa hiyo wapo viongozi kadhaa kutoa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo walifika kuhudhuria adhimisho la misa hiyo akiwemo Baba Askofu Dkt.Msafiri Mbilu ambaye alialikwa katika marufaa ya Kanisa ya Ekaristi Takatifu na kuwasalimu waamini hao na kutoa ujumbe huu,

“Kuna wakati nilialikwa hapa katika mashindano ya uimbaji, lakini nilikuwa nje ya nchi, siku ya leo nipo hapa, nimeungana nanyi maana kuna kijana wa wanafamilia yetu amepata Komuniyo ya Kwanza.

"Kabla ya kufika hapa niliwasiliana na na Baba Askofu Mteule wa Jimbo Katoliki la Tanga kuwa leo nitashiriki nanyi, leo nipo nanyi.

"Nimeyafuatalia kwa karibu mahubiri ya Padri Masanja juu ya maadili ya vijana wetu.Wazazi au walezi tusivae majambakoti ya uvivu na uzembe katika malezi.

"Wazazi msivae misurupwete ya uvivu na uzembe katika malezi. Jamani kila mzazi ni mwalimu wa kwanza, tuvae vazi la kung’aa, tuwe na sura njema katika malezi ya watoto na vijana wetu na sote ni tuisikie sauti Mungu asanteni sana.”

Baba Askofu Msafiri Mbilu aliambatana na mkewe Dkt.Mary Mbilu na pia akiwa na mama Sarah Jally ambaye ni mke wa Baba Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Baba Askofu Josephy Jally.

Hadi misa hiyo ya iliyoanza saa tatu kamili ya asubuhi inakaamilika hali ya hewa ya Lushoto Mjini na viunga vyake ilikuwa baridi kali, japokuwa jua lilikuwa linawaka, kwa maelezo ya wakazi wa Lushoto wanadai kuwa sasa ni wakati wa baridi kumalizika maana ilianza tangu mwezi wa sita 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news