Mwenyekiti wa TEF aishirikisha jambo TTCL

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatius Balile ametoa rai kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wake wote huku msisitizo ukiwa ni ubunifu.

Sambamba na kufanya kazi kwa bidii ili shirika hilo liweze kuwa kivutio cha huduma kwa watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi, hivyo kutengeneza faida kubwa.

Balile ametoa wito huo leo Agosti 24, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kinachoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo leo ilikuwa ni zamu ya TTCL kuelezea walipotoka, walipo na wanapokwenda.

Amesema, "Transformation zote hizi ambazo mnazifanya zitafanikiwa zaidi ikiwa pia wafanyakazi wako utawalipa vizuri, kwa hiyo wafanyakazi wako wawezeshe kiasi kwamba, mfanyakazi hana wasiwasi anapotoka nyumbani kuja ofisini kufanya kazi.

"Wafanyakazi wengi wa taasisi zinazofanya vizuri, hakuna anayekopa Januari, kwa ajili ya ada au kodi ya pango imeisha. Kwa hiyo, wawezeshe wafanyakazi wa TTCL wawe wameridhika kwanza, akitamani kununua gari alinunue, ikiwa wana uwezo wa kuzalisha fedha nyingi, basi wawezeshwe vizuri.

"Ukifanikiwa hilo la kuwapa motisha wafanyakazi, kwa kuwaongeza mishahara hata kuwahi watawahi ofisini, wenyewe ndiyo watakwambia tufanye ubunifu wa namna hii, lakini mkiendelea kuwambia fungeni mkanda kama wakati ule wa vita, hii mipango yote unayoizungumza haitafanikiwa vizuri, kwa hiyo wewe acha alama vizuri."

Mbali na hayo amebainisha kuwa, kuna umuhimu wa kufanya maboresho kwa baadhi ya sheria ambazo zimekuwa zikiyafanya mashirika ya umma kushindwa kutekeleza miradi kwa wakati kutokana na sheria husika kuchukua muda mrefu huku wengine wakiendelea kuboresha huduma zao.

"Hii Sheria ya Ununuzi wa Umma, watu ambao hawajaitumia, watu ambao hawafanyi biashara, hawajui ugumu wa hii sheria.

"Kwa mfano, TTCL ikatokea wanataka kujenga mnara, ukianza mchakato wa ununuzi serikalini-procurement, ni siku 180, miezi sita.

"Lakini, Vodacom, Airtel, Tigo akitaka kujenga mnara, yeye anaamka asubuhi, anapiga simu Dubai anaambiwa mnara unauzwa kiasi fulani, anasema ninawatumia advance nyingine nitamalizia taratibu.

"Hela za TTCL zisipopita kwenye bajeti bungeni hawezi kuzitumia, kwa hiyo pamoja na kwamba TTCL anaweza kupata maono mwezi wa saba, baada ya bajeti kusomwa bungeni mwezi wa sita, ina maana hilo jambo litasubiri mwaka mmoja.

"Sasa, kama tunataka kujenga taasisi ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, lakini pia zikaenda kama tunavyoona TTCL inaziwezesha nchi zote zinazotuzunguka, tumeona mitandao ya simu Kenya, Zambia hapa kwa wenzetu Burundi, sehemu nyingi tunaona connection ile kwamba wanawezeshwa na Mkongo wa TTCL."

"Hapa kwa mfano nilioutoa TTCL leo mwezi wa nane,wakipata wazo ambalo wanadhani ni la kimaendeleo kwa kutumia utaratibu wa uamuzi wa kiserikali,inabidi ili wazo waliweke kwenye mipango yao ili liwekewe bajeti mwakani mwezi wa sita.

"Sasa, kama kwa mfano mtu alikuw ana teknolojia ya 3G mwezi wa tatu mwaka jana, ikafikia mwezi wa nane ikaenda 4G, sasa hivi wanazidua 5G wewe unasubiria mwaka mmoja ndipo na wewe ushiriki uzinduzi, kwa hiyo wakati unazindua wenzako wanaanua matanga wewe ndiyo unatangaza msiba.

"Kumbe marehemu hata alishaoza, kwa hiyo katika hali hiyo ni lazima tufike mahali kwamba hizi taasisi za umma, ziwe na uwezo wa kufanya uamuzi, uamuzi wa kibiashara na zisijifungie ndani kama alivyosema Mheshimiwa Rais."

Aidha, ili kuondokana na changamoto hiyo, Balile ameshauri kuna umuhimu wa kujifunza kwa wenzetu na hata ifike mahali kufanya uamuzi sahihi kwa ustawi bora wa taasisi na mashirika mbalimbali nchini.

Balile amesema, China ina mfano mzuri ambapo mwaka 1976 waliunda kampuni 11 ambazo zinaendesha uchumi wake na hizo kampuni zikawa zinafanya uamuzi wa kibiashara bila kuingiliwa ambapo matokeo bora yalipatikana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news