Mwinjilisti Temba aibua hoja Bandari Kavu ya Kwala

PWANI-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ameiomba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuelekeza Bandari Kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani ianze kutoa huduma ili wananchi na Taifa liweze kunufaika kiuchumi.

Hii ni sehemu ya Barabara ya Kwala ambayo vinyesi vya ng'ombe vimeichafua kutokana na wafugaji kuitumia barabara hiyo mpya iliyotumia gharama nyingi kwa ajili ya Bandari Kavu ya Kwala kupitisha mifugo kwenda malishoni na Mnada wa Kwala aambao huwa unafanyika kila Jumamosi.

Mwinjilisti Temba ambaye ni mdau mkubwa wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli za maendeleo nchini ameyabainisha hayo leo Agosti 16,2023 baada ya kufika bandarini hapo na kubaini kuwa, kuna changamoto kadhaa ambazo zinajitokeza huku mifugo ikianza kuharibu miundombinu ambayo imejengwa kwa gharama kubwa.

"Kuanzishwa rasmi kwa Bandari Kavu ya Kwala iliyoko Ruvu Kwala kumekuwa ni changamoto, kumekuwa na kauli mbalimbali za Serikali tangu mwaka 2017 za uanzishwaji wa haraka wa banadari kavu na kila mwaka Serikali imekuwa ikisema mwaka huu itakuwa ndiyo mwaka wa uanzishwaji wa banadari kavu.

"Lakini, kumekuwa na vikwazo mbele ya safari, hata baada ya eneo kubwa la Bandari Kavu ya Kwala kukamilika, bado vikwazo ilikuwa ni changamoto ya barabara kutoka Vigwaza mpaka Kwala kilomita 15 ambayo ilikuwa haijajengwa.

"Kwa sasa, barabara hiyo imejengwa na imekamilika, lakini pia kuna barabara ya reli, maofisi yamejengwa na viongozi mbalimbali wa Uchukuzi (Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi) huko nyuma, walitembelea na treni maalumu wakionesha kwamba baada ya miezi michache, Bandari Kavu ya Kwala itaanza.

"Mheshimiwa Kamwele (Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe ) aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi alifanya safarai za mara kwa mara za kuonesha kwamba, baada ya miezi michache Bandari Kavu ya Kwala itaanza.

Fikra za Watanzania

"Lakini, cha ajabu mpaka sasa hivi Bandari Kavu ya Kwala haijaanza, wako Watanzania wanaoamini kwamba, bandari hii inaweza isianze leo au kesho na inaweza kuchukua miaka mingi, kwa sababu ya baadhi ya Watanzania wanaomiliki mayadi yaliyoko katika Jiji la Dar es Salaam.

"Wamiliki ambao ni wanufaika wakubwa sana wa mayadi hayo kwa sababu ya ukaribu na bandari kabisa na wamekuwa wakitengeneza fedha nyingi.

"Baadhi ya maeneo mbalimbali utafiti uliofanywa ambayo Watanzania wanakodisha maeneo yao kama yadi au sehemu mbalimbali za kuwekea mizigo kumekuwa na gharama za kulipia kwa mwezi kuanzia dola 3000 na kuendelea.

"Hivyo, inawezekana kabisa ikaonekana kuna nguvu isiyojulikana ikiendelea kuchelewesha uanzishwaji wa makusudi wa Bandari Kavu ya Kwala.

"Baadhi ya wafanyabiashara Tanzania huko nyuma kwa awamu zilizopita walikuwa wakiendelea kulaumiwa kwamba, waliweza kuihujumu Serikali ili kunufaisha maisha yao na biashara zao.

"Kwa mfano, reli ilikuwa ikifanya kazi kubwa huko nyuma kubeba mizigo tulikuwa tukishuhudia kipindi cha Bandari Kavu ya Isaka ilivyokuwa ikifanya kazi huko Shinyanga mizigo mingi ilikuwa ikibebwa kwa reli, na wakati huo reli ilikuwa ina nguvu sana.

"Lakini, inasemekana wafanyabiashara ndiyo walioiua reli na kusababisha kifo cha Bandari kavu ya Isaka, hivyo, Watanzania wengi wamekata tamaa Bandari Kavu ya Kwala imekuwa kila mara inatangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

"Tumekuwa tukiwaona viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakienda, tumewaona marais wa nje wakienda mfano Rais wa Jamhuri ya Burundi, tumewaona wajumbe wa kutoka Rwanda,Congo na wengineo kwa nyakati tofauti wakipelekwa na kukabidhiniwa, kuoneshwa maeneo ya Bandari Kavu ya Kwala.

"Lakini, pia tumeona baadhi ya maeneo ya Bandari Kavu kule Kwala yakiwekwa misingi na utambulisho wa miradi mbalimbali.

"Hata sasa hivi tumeona kwamba kuna viwanda karibu 200 vinajengwa na barabara ya lami imeongezwa kutoka pale Bandari Kavu ya Kwala na maeneo ya karakana, mwendokasi, yanayojengwa zaidi ya kilomita tatu.

"Lakini, bado mazingira na watu ambao wanaishi maeneo ya Kwala wanasema wazi kwamba masuala ya uanzishwaji wa Bandari Kavu Kwala ni kizungumkuti.

Mifugo barabarani

"Barabara iliyojengwa kwa gharama kubwa, ya Vigwaza kwenda Kwala sasa hivi inaonekana kabisa kuharibika kwa vinyesi vya ng'ombe kwa sababu inaonekana kuwa ni njia kuu sasa ya kwenda kwenye Mnada wa Kwala.

"Mnada unaofanyika kila Jumamosi ambao upo karibu kabisa na Bandari Kavu ya Kwala, kitendo cha ng'ombe kutumika kuswagwa kupita katika barabara hiyo ya zege yenye gharama kubwa ambayo kimsingi zimekuwa zikizuiwa sana kupita kwenye barabara za lami na barabara za zege.

"Zimesababisha barabara hiyo kuendelea kuchafuka na kuendelea kuwa katika mazingira mabaya baada tu ya kumaliza kujengwa na hata kabla ya matumizi.

"Watu wengi wanashangaa namna ambavyo Serikali inakaa kimya,na uchafuzi huu ambao unasababishwa katika barabara iliyoigharimu Serikali fedha nyingi.

"Ni ujenzi uliotumia mabilioni ya fedha ambazo ni fedha za walipa kodi Watanzania, Serikali ije wazi iseme ni lini bandari kavu itaanza.

"Kwa sababu pia Watanzania ambao wapo pembezoni mwa bandari kavu ya Kwala ambao watanufaika kiuchumi, lakini pia bandari inakwenda sambamba na wadau ambao nao husababisha eneo la bandari kavu nalo liweze kuwa imara.

"Kwa mfano mahoteli yangetakiwa yawepo sasa hivi, ilibidi yaanze kujengwa, magereji yalitakiwa yaanze kuwepo ili yaweze kutoa huduma, maeneo ya yadi, maeneo ya kuegeshea yangetakiwa kujengwa na yawepo kwa sababu eneo kubwa kule ni mfinyanzi.

"Hivyo, ilitakiwa liweze kutengenezwa kwa kiwango cha zege ili kuweza kuruhusi magari makubwa yakipaki yasiweze kuzama.

"Kitendo cha Serikali kuwa kimya na kutotangaza ni lini bandari kavu ya Kwala itafunguliwa kumeendelea kuwatia wasiwasi Watanzania na kuwa na mashaka makubwa, hivyo kuonesha ni kwa namna gani Serikali wakati mwingine yapo mambo ambayo yanatumia gharama kubwa, lakini wakati mwingine yanaendeshwa kisiasa.

"Wananchi, pia walitaka, ipo njia ambayo itatengenezwa kupita Kwala kwenda Mpriamumbi, kwenda Ngwala mpaka Chaua Chalinze, njia hiyo ambayo itakuwa rahisi na fupi ukitokea Chalinze ni barabara ambayo itasaidia malori ambayo yanarudi tupu au na mizigo kutoka Zambia ama Congo kuzunguka wakati wa kurudi.

"Badala ya kuja moja kwa moja mpaka Vigwaza na baadaye kukatisha tena kwenda Kwala ambapo njia hiyo inaweza kuwa na msongamano mkubwa wa malori na kusababisha foleni kubwa katika eneo hilo la Vigwaza mpaka Kwala.

"Mpaka sasa hivi kumekuwa na taarifa kwamba, njia hiyo inatakiwa ijengwe ni bora na ni muhimu sana na hata hivyo, njia hiyo ilitakiwa itengenezwe ambapo inaweza kuanza Vigwaza kwa Zoka baada ya kuvuka reli ambapo njia hiyo itapiga Kivungwi, Vishezi na kisha itaingia kwenye shamba la kilimo la Serikali lililoko Kwala na kutokezea kwenye bandari Kavu ya Kwala.

"Mambo haya pia yalitakiwa yakionekana sambamba Serikali ikiyafanyia kazi, kwa sababu kuna magari zaidi ya 20,000 ambayo yatakuwa yanakwenda Kwala kuchukua mizigo.

"Hivyo basi kitendo cha Serikali kuendelea kukaa kimya wakati ikijulikana wazi magari 20,000 mpaka 10,000 ni magari mengi sana ambayo yanahitaji barabara nyingi ili kupunguza msongamano wa malori.

"Kwenda eneo hili, ikijulikana kwamba barabara ya Morogoro kuanzia Mlandizi mpaka Chalinze bado imekuwa na ufinyu mkubwa sana na hivyo ingepaswa kupanuliwa na kuongezwa.

"Kama kweli Serikali ina nia ya dhati ya kuwekeza katika bandari kavu, kwa sababu malori haya ni mengi sana kupunguza foleni, pale bandari kavu itakapoanza.

"Wananchi wanatamani sana kuona uchumi wao ukibadilika na Serikali imeleta mpango kazi wa kusababisha mji wa Kwala kuwa mji wa kibiashara wa kisasa, lakini hatuoni juhudi zozote za haraka.

"Zinazoonesha upanuzi wa barabara katika maeneo hayo na kujenga na kufunguliwa barabara mpya zaidi ya iliyojengwa,lakini pia kumekuwa na kizungumkuti juu ya ufunguzi wa bandari kavu hivyo kuonesha jambo hili ni la kisiasa zaidi ya kiuchumi, kwa sababu haieleweki na hakuna anayejua ni lini bandari kavu ya Kwala itaanza.

"Wakati zaidi ya asilimia 90 imekwisha kamilika na tuliambiwa kwamba malori yangeweza kuanza hata pale ambapo shughuli zote hazijakamilika kwa asilimia 100, ilikuwa pia ni sehemu ya kuangalia changamoto mbalimbali na tuliambiwa pia mabehewa yalikiwisha wasili na njia ya reli tayari ilikuwa imeshaungwa.

"Lakini,bado inaonekana kuna mkono wa baadhi ya wafanyabiashara ama la sivyo, kwa sababu hakuna taarifa zozote za Serikali au TPA (Mamlaka ya Bandari Tanzania) za kuhamasisha wananchi waanze kutengeneza miundombinu ya kuweza kwenda sambamba na bandari kavu.

"Bandari kavu ni jambo kubwa sana,ni suala ambalo Watanzania mbalimbali wanatarajia kupata fursa zaidi ya milioni moja zitakuwa kwa ajira zisizokuwa rasmi ambazo zitasaidia uchumi wa Tanzania ambao watu wengi hawana ajira, lakini kwa nini Serikali imekuwa kimya.

"Kuliona hilo, limekuwa ni jambo lingine la kushangaza, kwa sababu Serikali imekuwa ikiendelea kupambana na kuwahakikishia Watanzania kuwa imekuwa ikiimarisha miundombinu ili kufungua fursa za ajira.

"Hivyo, Serikali inatakiwa kujua kwamba, suala hili la bandari kavu limekuwa kichwani mwa watu, na umeshakuwa ni muyda mrefu sasa kumekuwa na kauli za kwamba, kila bada ya miezi mitatu, miezi sita bandari kavu inaanza.

"Lakini, mpaka sasa hivi hakuna dalili zozote za kuanza, wananchi wengine wamekwishajitoa hususani wafanyabiashara walioko maeneo ya Tabata Dampo ambapo katika eneo la Vigwaza Kambini wamenunua zaidi ya hekari 100 ambazo wameshazipima na wametengeneza maeneo yao kwa ajili ya kufanya mambo mbalimbali ya kiuchumi.

"Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na mayadi, maeneo ya vifaa, gereji na kadhalika, lakini bado Serikali Kuu kupitia TPA imekaa kimya, tunaiomba TPA ije sasa iwaambie Watanzania kama Bandari Kavu Kwala ipo na itaanza lini.

"Ikumbukwe kwamba fedha nyingi zimekwishatumika na zinatakiwa zirudi, hivyo ni wakati wa Serikali sasa kuamua moja juu ya uanzishwaji wa Bandari Kavu ya Kwala, kwa sababu Watanzania wengi wamekuwa wakisiia huzuni kwa sababu taarifa za kuanza kwa bandari hiyo zimekuwa kama za kisiasa bada ya kiuchumi.

"Tunaiomba Serikali na ninaiomba Serikali, ifanye haraka mwaka huu usiishe ili banadari kavu ianze kwa sababu watu zaidi ya milioni moja ambao wangeweza kupata kazi na ajira, rasmi na zisizo rasmi.

"Sambamba na hayo, kanda ya Pwani ambayo imeathirika sana kwa biasahara ya ukataji wa mikaa na vijana wengi wamekuwa na tabia mbaya mbaya ikiwemo kudokoa na kudandia malori kushusha mizigo na kadhalika.

"Ujio huu wa bandari kavu ulikuwa unasaidia zaidi ya asilimia 70 kupunguza kasi ya ukataji miti na uchomaji mikaa pamoja na vijana mbalimbali ambao wamekuwa wakijishughulisha na vitendo vya uhalifu kufikia kikomo.

"Serikali ije sasa iseme wazi ni lini sasa ama Mheshimiwa Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wataifungua rasmi bandari hiyo ili ianze kutoa huduma.

"Ama wataanza kabla ya kufunguliwa rasmi ili Watanzania waweze kujipanga, zaidi ya hapo, eneo la Mnindi ambalo ni karibu kilomita saba kutoka Vigwaza kwenda Kwala Bandari Kavu limevamiwa na Watanzania mbalimbali, wameuziwa na wameanza ujenzi, Serikali ifanye juhudi kuja kuonesha au kuja kuzuia watu ambao wameingia kwenye eneo la Serikali.

"Katika shamba la Kilimo na NARCO pembezoni mwa bandari kavu ya Kwala ambapo kila kukicha Watanzania wanauziwa wasiojua kwamba eneo hilo mwisho wake ni wapi, kwa sababu zipo nyumba mbalimbali ambazo zimejengwa katika maeneo ambayo si ya wananchi.

"Na zinahaminisha watu wengine kwamba maeneo hayo ni sahihi,kitendo cha Serikali kuendelea kukaa kimya kuhusu maeneo hayo ambayo yamevamiwa na yanaendelea kujengwa huku Watanzania wakiendelea kuuziwa kitaendelea kuumiza Watanzania wengi ambao wanatumia nguvu kazi zao za fedha kwa ajili ya ujenzi na kisha baadaye kuja kubomolea.

"Ninatoa wito kwa Serikali kuhakikisha kwamba,inaruhusu ama inazuia uvamiaji wa maeneo ya Serikali kwa sababu watu wengi wanaonunua hawajui, na mwisho kabisa wananchi wamekata tamaa.

"Wa Kwala, Mpiramumbi, Gwata, Chaua Chalinze ni lini uanzishwaji wa bandari kavu ya Kwala itaanza kufanya kazi, ninamuomba Mheshimiwa Rais atoe kauli juu ya uanzishwaji wa bandari kavu kwa sababu, wananchi wanajipanga kuleta maendeleo hususani kupitia uanzishwaji wa bandari kavu hiyo.

"Suala hilo linahitaji fedha za ujenzi, fedha za matumizi, wanashindwa kuamua sasa kwa sababu hawajui ni lini wasije wakawekeza fedha nyingi katika ujenzi mbalimbali kisha bandari kavu isianze leo au kesho au ikahairishwa, Serikali iseme ni lini Bandari Kavu ya Kwala itaanza.

"Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, atoke hadharani awaambie Watanzania ni lini Bandari Kavu ya Kwala itaanza,"amefafanua kwa kina Mhubiri a Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news