Simba SC yaandika historia Makumbusho ya Taifa

DAR ES SALAAM-Simba SC imekuwa klabu ya kwanza Tanzania kuweka taarifa na kumbukumbu zao kwenye Makumbusho ya Taifa.
Lengo ni kuwezesha vizazi vya sasa na vijavyo kupata nafasi ya kutembelea na kufahamu walipotoka, walipo na wanapoelekea.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, CPA Issa Masoud amezindua eneo maalum ndani ya Makumbusho ya Taifa ambapo kumbukumbu zote za klabu yao zimewekwa rasmi.

Baada ya kuzindua eneo hilo ambalo kuna eneo maalum taarifa zote za klabu tangu ilivyoanzishwa mwaka 1936, CPA Masoud alitembezwa maeneo mbalimbali na Mkurugenzi wa Wanachama, Mzee Khamis Kisiwa.

CPA Masoud amesema, wameamua kuiweka historia ya klabu yao ili kutunzwa ndani ya Makumbusho ya Taifa ambapo wanaamini itakuwa salama.

“Kuanzia sasa historia ya Simba inapatikana ndani ya Makumbusho ya Taifa, yoyote ambaye anataka kuijua vizuri Simba anapaswa kuja hapa na kujifunza,” amesema CPA Masoud.

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Dkt.Gwakisa Kamatula aliwakaribisha Wanasimba na Watanzania kwa ujumla kutembelea ili kujua historia ya Simba tangu ilivyoanzishwa na mabadiliko mbalimbali iliyopitia hadi kufika sasa.

“Tunawaalika Wanasimba na Watanzania wote kuja kuifahamu timu hii kubwa Afrika. Kama kuna mtu ana picha au kipande cha gazeti, jezi ya miaka ya nyuma au viatu avilete hapa ili tuvihifadhi kwa kumbukumbu za sasa na baadae,”amesema Dkt.Gwakisa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news