NEC yatangaza uchaguzi mdogo wa Mbarali na kata sita

DODOMA-Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023.
Akisoma taarifa kwa umma jijini Dodoma leo tarehe 05 Agosti, 2023, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima amesema wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.

Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi mdogo kuwa ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” amesema Bw. Kailima.

Aliongeza kuwa, Tume imetoa taarifa hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiitaarifu Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya. Nafasi hiyo wazi inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Francis Mtega. Spika ametoa taarifa hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

“Tume imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye Dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara. Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,” amesema Bw. Kailima.

Ameongeza, “Tume kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Mbarali na Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news