Sisi bodi ya TPDC hatutakubali ninyi mtuangushe-Balozi Sefue

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Balozi Ombeni Sefue amewataka wajumbe wa bodi za kampuni tanzu za shirika hilo kwenda kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kupata matokeo chanya.
"Sisi bodi ya TPDC hatutakubali ninyi kampuni tanzu mtuangushe, tuelewane kabisa tangu leo, uwezo mnao mkajitume nashukuru sana Wizara ya Nishati na Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa mstari wa mbele kutekeleza malengo ya TPDC kufikia malengo yanayokusudiwa."

TPDC inamiliki kampuni tanzu mbili ambazo ni Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO) na Kampuni ya Mafuta (TANOIL).

Balozi Sefue ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa bodi hizo leo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam amesema, shirika hilo lina matumaini makubwa na wajumbe hao kutokana na utaalamu ukiwemo uzoefu wa kutosha katika kusimamia sekta hizo.

Aidha, kupitia hafla hiyo, TPDC imetambulisha wajumbe 10 ambapo kati yao wajumbe watano ni wa GASCO na wengine wa TANOIL.

"Niwapongezeni wote mlioteuliwa mmeingia katika historia ya wana bodi waanzilishi, mnawajibu mkubwa kuhakikisha historia hiyo inakuwa ya kutukuka.

"Cha kufanya, mfanye kazi kwa bidii na weledi tunawahakikishieni ushirikiano wa Bodi ya TPDC na sote tunafahamu TPDC inajukumu la kusimamia maslahi ya Serikali katika sekta ya mafuta na gesi asilia.
"Na pia kujiendesha kibiashara ndani na nje ya nchi na kwa sababu hiyo kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC inapenda kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kukubali ombi letu na kupewa uhuru zaidi katika utekelezaji.

"Kuna watu wanafikiri mashirika ya umma hayawezi kujiendesha kibiashara,kupata faida, kushindana, na dhana hiyo haina ukweli.

"Ili tuweze kujiendesha kibiashara na kiushindani ni muhimu tuwe na uhuru wa kuweka mifumo na taratibu zitakazozalisha tuwezeshe kufanya wafanyavyo washindani wetu ndani ya nchi, kikanda na kimataifa."

"Mbali na uhuru unakuja wajibu, mheshimiwa Rais ametuamini ni wajibu wetu kutendea haki wajibu huo na hilo ni jambo la msingi sana kuzingatiwa na kwa hili hatutakuwa na kuoneana muhali. 

"Sekta hii ina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo na ustawi kwa watanzania, Mwenyezi Mungu ametubariki kwa rasilimali za mafuta na gesi ni wajibu wetu kuzitafiti na kila zinapothibitika kuzitumia kwa namna inavyolinda masilahi ya taifa na kuchangia maendeleo kwa kuzingatia masilahi ya wale ambao tunalazimika kushirikiana nao katika kutekeleza na hilo ni jukumu letu.

"Na kwa uhuru tunaopewa tuna jukumu la kuwa wabunifu, wathubutu, wajasiriamali kweli kweli tutakaoshindana nao ni sekta binafsi kitaifa na kimataifa. 
"Lazima tuongeze ubunifu, uwajibakaji, uadilifu kwa kiwango cha juu kama hatuwezi kusema mapema ni busara sana."

Amesema,wajumbe waliochaguliwa hawakuchaguliwa kwa kujuana, kwani kulikuwa na mchakato huru wa kuwapata uliosimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Pia, Balozi Sefue amesema, mchakato wa kuunda bodi hizo za kampuni tanzu ulikuwa moja ya ajenda ya kwanza kabisa ya Bodi ya Mpya ya TPDC katika kikao chake cha kwanza cha Agosti 11,2022.

"Tarehe 10 Oktoba 2022 shirika lilitoa matangazo ya kukaribisha maombi ya Watanzania wenye sifa za kujaza nafasi katika bodi za kampuni tanzu za TPDC na hadi kufikia tarehe 21 bodi ilipokea maombi 289;

"TANOIL yalikuwa maombi 104, GASCO yalikuwa maombi 112 na maombi 73 hayakuonesha yanalenga kampuni ipi katika ya hizo na machache waliomba kujaza nafasi za utendaji ndani ya shirika na hivyo kukosa kufanyiwa mchujo.

"Kufika mwezi Mei, mwaka huu tulifanya usaili ilipofika Julai taratibu zote za kiserikali zilikamilika, ni imani yetu kuwa ninyi mlioteuliwa, hamtatuangusha bali mtaleta ujuzi.
"Maarifa na uzoefu kwa ajili ya ustawi wa shirika kupitia kampuni tanzu na kutuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea kwa maslahi ya taifa kwa wakati na kwa ufanisi.

"Yakiharibika maana yake hamtaki, sote tunajua sifa zenu ama kwa makusudi au kwa uzembe, mnazo sifa na uzoefu, mkafanye kazi nawapongeza pia jopo la usaili kwa kufanikisha vizuri zoezi hili."

Katika hatua nyingine, Balozi Sefue amewataka wajumbe hao kutambua kuwa, utekelezaji wa majukumu unapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Serikali.

Sambamba na ile ya Kimataifa kuhusu utawala bora na usimamizi wa sekta hizi za mafuta na gesi.

"Bodi hizi ninaamini zitafanya kazi kwa weledi, jukumu kubwa la bodi zetu iwe kusimamia menejimenti na sio kufanya kazi za menejimenti.

"Wasimamieni, lakini msifanye kazi za menejimenti, nendeni mkafanye kazi kubwa na nzuri katika kuweka na kusimamia misingi ya utawala bora na mifumo yake

"Mkasimamie mazingira bora ya kazi na watumishi na rasilimali nyingine za kampuni hizi mkasimamie. 

"Najua kuna changamoto mtazikuta, hizo ni fursa za kuonesha kwamba hatukukosea kuwachagua, onesheni uwezo, ukomavu na ubobevu wenu mliotuhakikishia mnao."

Balozi Sefue amesema, hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Hazina imeiondoa TPDC katika taasisi zitakazoendelea kupata ruzuku ya Serikali na hivyo kupata ruzuku ya kujitegemeza.

"Hivyo nashauri bodi za kampuni tanzu zianze kuandaa mipango mkakati wa kila kampuni wenye lengo la kuiwezesha kila kampuni kujitegemea, kuongeza faida na hatimaye gawio kwa Serikali.
"Pili kusimamia mabadiliko ya muundo wa kampuni tanzu na mifumo yake ili kuendana na adhima ya Serikali na hakikisheni mnajiendesha kibiashara na kwa ushindani, muongeze mapato mpunguze gharama na kuongeza kujitegemea."

Wakati huo huo, Balozi Sefue amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini katika sekta ya mafuta na gesi nchini.

"Namshukuru pia tena Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini sisi kuanzisha na kusimamia mageuzi makubwa katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini ili ilete tija na kuchangia maendeleo ya Watanzania, nilimwaahidi Mheshimiwa Rais hatutamwangusha."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news