Ukishindwa, kufa na shirika lako-Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali imewekeza fedha nyingi katika mashirika ya umma huku ikiwa haioni tija, hivyo Serikali inatarajia kufanya mabadiliko katika mashirika hayo. 
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Agosti 19,2023 jijini Arusha wakati akifungua Kikao Kazi cha siku tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma nchini.

"Ndugu zangu ma-CEO (Maafisa Watendaji Wakuu), Wenyeviti wa Bodi hatutanii, tumeshatoa fedha nyingi sana, zinaingia kwenye drainage, hatuoni tija yake.

"Sasa ni kuwekeana vigezo, ni kuwekeana vipimo vya utekelezaji au utendaji, lakini kuwekea targets za kufanya faida, ukishindwa huna sababu ya maana, kufa na shirika lako."
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amepiga marufuku tabia ya baadhi ya mawaziri na watendaji wa wizara mbalimbali kugeuza mashirika ya umma kama vyanzo vyao vya mapato.

Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa, mpango huo umekuwa ukidhoofisha mashirika kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Amesema, kumekuwa na baadhi ya wizara ambazo zimekuwa zikiomba michango kutoka katika taasisi zilizo chini ya wizara zao kipindi zinapoishiwa bajeti ya matumizi mengineyo.
“Wizara zinaweka mikono katika mapato ya mashirika hii haitakiwi, kama tunataka mashirika yazalishe tusiyaingilie. Mashirika yanapaswa kuchangia gawio.

"Msajili wa Hazina tumekupa jukumu la kuyasimamia mashirika haya ila ninafahamu kuna kujisahau, kwa baadhi ya makatibu wakuu wa wizara kutaka kuingilia utendaji wa kila siku, ikiwemo kuamrisha mashirika kuchangia shughuli za Katibu Mkuu au Waziri kibajeti, hii nimeipiga marufuku na ninadhani mmenisikia."
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameridhia mapendekezo ya kufanya mageuzi makubwa katika mashirika na taasisi za umma ili kuongeza ufanisi na kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.

Amesema, Serikali inatunga sheria kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma huku akibainisha kuwa, amepokea mapendekezo ya kufanya mabadiliko makubwa katika taasisi za umma ambazo kiutendaji zinasimamiwa na ofisi hiyo.“Nimeridhia mapendekezo hayo.Tunataka kupunguza mzigo kwa Serikali."

Aidha, mapendekezo yaliyoidhinishwa na Rais Dkt.Samia ni pamoja na kufuta baadhi ya mashirika, kuunganisha baadhi ya mashirika na kuanzisha mashirika mapya ingawa haijawekwa wazi ni mashirika yapi Serikali inaanza nayo.
Rais Dkt.Samia ameiagiza ofisi hiyo kushirikiana na wizara za kisekta kuanza mchakato wa kisera na kisheria kukamilisha mabadiliko hayo.

Vile vile, Rais Dkt.Samia amesema, mabadiliko hayo yanatokana na kuingiliana na kushabihiana kwa majukumu ya baadhi ya taasisi, hivyo mpango wa kuziunganisha zitaipunguzia serikali gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi na tija kiutendaji.

Rais Samia pia ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha mpango huo unafuata utaratibu na ushirikishwaji wa wadau wanaohusika, kulinda ajira na stahiki za watumishi pamoja na mali za umma kipindi chote cha mpito.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyataka mashirika ya umma kuvuka mipaka na kuwekeza nchi jirani ili faida itakayopatikana itumike kuendesha mashirika hayo hapa nchini.

Mchechu

Awali akizungumza katika mkutano huo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu ametaka uwepo wa maboresho ya utendaji katika uendeshaji wa mashirika ya umma nchini ili kwendana na maelekezo ya Rais Dkt.Samia.

Mchechu amesema, ofisi yake imeandaa mkutano huo ambao utakuwa ukifanyika kila mwaka ili kuboresha utendaji wa taasisi za umma, lakini pia kuja na mabadiliko ambayo yataongeza ufanisi na kufikia malengo ya Serikali.
"Kikao hiki ni nafasi za kuzungumza changamoto zetu na kujadiliana jinsi ya kuzitatua kwa pamoja kwani taasisi zetu zina mahusiano ya karibu,"amesema

Katika hatua nyingine,kampuni 28 za Serikali likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yatakuwa huru karibuni.

Msajili wa Hazina,Nehemiah Mchechu amebainisha kuwa, uamuzi huo unalenga kuyafanya mashirika hayo kuwa huru na kuachana na utegemezi kutoka Serikali Kuu.

“Tumefikia muafaka na Wenyeviti na Wakurugenzi wa taasisi hizi. Tunataka kuona makampuni mengi yanafanya kazi kwa uhuru,” alisema.
Mbali na hayo,Ofisi ya Msajili wa Hazina imezitambua taasisi na mashirika yaliyofanya vizuri katika mwaka wa fedha 2022/23. 

Taasisi hizo ni pamoja na Mashirika ya Umma yaliyotoa gawio kubwa zaidi ambapo taasisi hizo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Pia,Ofisi ya Msajili wa Hazina ilizitambua Kampuni za Twiga Cement, Benki ya NMB na Airtel Tanzania kama taasisi binafsi ambazo Serikali inahisa. 

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia pia alitoa tuzo kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Bima la NIC Insurance kama makampuni yaliyofanya mapinduzi kutoka kuwa orodha ya mashirika yaliyokuwa hatarini kufutwa hadi mashirika yanayochangia gawio serikalini.

Taasisi zilizotambuliwa kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Bima ya Taifa (NIC).

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo hizo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu ameipongeza STAMICO na kubainisha kuwa, katika miaka miwili iliyopita ilikuwa inafikiriwa kufutwa kutokana na utegemezi, lakini sasa wameweza kuchangia hadi gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Wachangia mada

Wakati huo huo, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema, kuna umuhimu wa kutungwa upya kwa sera na sheria ya mashirika ya umma ili kuboresha utendaji wa mashirika hayo.
"Lakini pia kampuni ikiundwa tuipeleke kwenye soko la hisa ambapo Watanzania wengi watanunua hisa,"amesema Zitto wakati akitoa mada katika mkutano huo wa watendaji wa taasisi na mashirika ya umma unaoendelea jijini Arusha.

Zitto amesema, sheria mpya ya mashirika ya umma itaweka muongozo wa upatikanaji wakurugenzi wa bodi, watendaji wa bodi, hisa na uendeshaji.

"Mapendekezo yangu mimi ni kuwa Rais akiteua Mwenyekiti wa Bodi, basi bodi ndio ipewe jukumu la kuajiri Mtendaji Mkuu wa shirika ili aweze kuwajibika kwa bodi.

"Bodi ikiajiri Mtendaji Mkuu, ina uwezo wa kumuondoa kama atashindwa kutekeleza majukumu yake na kuajiri mtendaji mwingine," amesema Zitto.

Naye aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amependekeza namna bora ya upatikanaji wa wajumbe, bodi za mashirika ya umma nchini huku akitaka waombe na wafanyiwe usaili.

Akitoa mada katika undeshaji wa mashirika hayo na tafakuri kuhusu Tanzania,Profesa Assad amesema, upatikanaji wa wajumbe wa bodi ni tatizo.

Profesa Assad amesema, ili bodi za mashirika hayo ziweze kufanya kazi kwa ufanisi, lazima wajumbe wanaopatikana wawe na uwezo wa kusaidia taasisi hizo.

Amesema, pia matatizo mengine yaliyosababisha mengi ya mashirika hayo ama kufa, au kufanya kazi chini ni kiwango, ni matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za taasisi, ikiwemo ununuzi wa magari ya kifahari.

"Kuna haja gani kuwanunuliwa watendaji watano katika taasisi moja, magari matano ya kisasa V8 ambapo inabidi kuajiri madereva, lazima maeneo ya kuegesha magari.
Picha zote na Ikulu.

"Lakini pia kuna hili nimeona, tunakuja Arusha kwenye mkutano, watendaji wanakuja na ndege na magari yanawafuata Arusha, ili waje kutembelea nadhani hii pia ni matumizi mabaya ya rasilimali za mashirika.

"Kwa mfano tunanunua ndege Dreamliner ambazo tunajua kabisa matumizi yake hatuwezi, kwani ndege ambazo zinahitajika sana ni za kufanya safari za ndani matokeo yake shirika kupata hasara,"amesema Profesa Assad.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news