Awadhi Hamza Mohamed jela miaka 30 kwa kusafirisha bangi

MOROGORO-Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro imemhukumu, Awadhi Hamza Mohamed adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 34.65.
Katika hukumu iliyotolewa Agosti 31 2023 na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama hiyo, Livini Lykinana imeeleza kuwa, adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa sheria na pia ili iwe fundisho kwa wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Upande wa Jamhuri katika shauri hilo uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Elias Masini ambapo jumla ya mashahidi watano wa upande wa Jamhuri waitoa ushahidi ambao umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alisafirisha dawa hizo huku upande wa utetezi, mtuhumiwa alijitetea mwenyewe.

Hata hivyo, mtuhumiwa baada ya kusomewa adhabu hiyo aliomba Mahakama impunguziwe adhabu akidai kuwa hilo ni kosa lake la kwanza kutenda pia ana familia ambayo inamtegemea yeye na ana matatizo ya uti wa mgongo.

Mtuhumiwa alikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Desemba 22, 2022 katika Kijiji cha Chogoali Sokoni huko Kata ya Iyongwe Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro akiwa na kilo 34.64 za dawa za kulevya aina ya bangi.

Mohamed alikuwa ameficha na kuhifadhi bangi hiyo katika mifuko ya sandarusi. Aidha, Mahakama imeamuru kiasi hicho cha bangi kuteketezwa.

Bangi ni nini?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Cannabis Sativa”.

Huu ni mmea ambao hustawi na hutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote. Bangi huathiri ubongo na kubadili jinsi tunavyotafsiri uhalisia wa vitu.

Majani na maua ya mmea huo hukaushwa na hutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa zingine. Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi.

Aidha, watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia dawa nyingine hapo baadae kama heroin na cocaine. Hivyo, bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Majina mengine ya bangi yanayotumika mitaani ni kama msuba, dope, nyasi, majani, mche, kitu, blanti, mboga, sigara kubwa, ndumu, msokoto, ganja na mengineo.

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni kosa la jinai.

Kwa hiyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata, nk) ni kosa la jina na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news