DC Shaka aweka mambo wazi

IRINGA-Mkuu wa Wilaya Kilosa mkoani Morogoro Shaka Hamdu Shaka, amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaongeza kasi ya maendeleo na kuihakikishia nchi kupaa kiuchumi.
Amesema ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kiuchumi zikiwemo barabara, Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na ununuzi wa ndege kubwa ni miongoni mwa hatua za uhakika katika kuleta maendeleo endelevu.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa kongamano la uwekezaji lilofanyika ukumbi wa Royal Palm mkoani Iringa Shaka aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema pia mkakati wa usambazaji umeme unaotekelezwa na Serikali utafanikisha vijiji vyote nchini kupata umeme ifikapo Juni 2024.

Amesema nishati ya umeme ni muhimu kwa maendeleo hususan katika kuvutia uwekezaji mkubwa na kwamba kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kufanikisha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja wetu.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 za Afrika zinazokua kwa kasi kiuchumi. Kwa miaka 10 iliyopita uchumi wa nchi ulikua kwa wastani wa asilimia saba. Julai mwaka 2020, Benki ya Dunia (WB) iliipaisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha mwanzo cha kati.

“Mafanikio haya yanachagizwa na amani, utulivu wa kisiasa na kiuchumi pamoja na sera nzuri zinazotabirika. Kwa sasa uchumi wetu unakua kwa asilimia 5.2 ukiwa unainuka kutoka katika athari za Uviko-19 ni dhahiri kuwa tunakwenda vyema,” amesema Shaka.

Ameongeza Tanzania imeendelea kutoa fursa nyingi katika sekta zote na kwamba serikali inaweka kipaumbele zaidi katika maeneo muhimu kikiwemo kilimo, madini, utalii, ufugaji, uvuvi, gesi asilia, viwanda na Teknolojia ya Hbari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Serikali imedhamiria na kujitoa kuifungua nchi katika uchumi wa dunia kutokana na maboresho kwa sekta ya biashara na uwekezaji kupitia uendelezaji wa miundombinu mikubwa.

“Hatua hizo zinalenga kuharakisha mtiririko mzuri wa wawekezaji wa moja kwa moja wa nje (Foreign Direct Investments - FDI) na uwekezaji wa moja kwa moja wa ndani (Direct Domestic Investments - DDI) kwa ustawi wa jamii na uchumi wa Watanzania,” amesema.

Akieleza zaidi amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa ya kisheria, kikanuni, kikodi na kiforodha, mifumo na taasisi, utendaji kazi na matumizi ya TEHAMA pamoja na kuondoa vikwazo vinavyozuia ukuaji wa biashara."Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji Afrika."

Akizungumzia ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere lenye thamani ya dola za Marekani bilioni tatu litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,115, amesema litakuwa msaada mkubwa na kutoa msukumo katika ukuaji wa uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news