Maelfu hawajulikani walipo mjini Derna

TRIPOLI-Wakaazi wa mji ulioharibiwa wa Derna nchini Libya wanaendelea kuwatafuta ndugu na jamaa zao waliopotea huku waokoaji wakiomba usaidizi zaidi. Ni baada ya mafuriko yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kusomba wengi kuelekea baharini.
Wanachama wa Msalaba Mwekundu nchini Libya wakiokoa gari lililozama katika mafuriko.(Handout/Libya Red Crescent via EPA).

Maeneo ya jiji la Mediterania yaliharibiwa na mafuriko ya maji yaliyotokana na dhoruba kali iliyosomba mto ambao kawaida ulikuwa mkavu siku ya Jumapili usiku, na kupasuka kwa mabwawa juu ya jiji hilo. Majengo mengi ya ghorofa yaliporomoka huku familia zikiwa zimelala ndani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Luteni Tarek al-Kharraz siku ya Jumatano aliliambia shirika la habari la AFP kwamba vifo 3,840 vimerekodiwa katika mji huo wa Mediterania kufikia sasa, wakiwemo 3,190 ambao tayari wamezikwa. Miongoni mwao walikuwa angalau 400 wageni, ambapo wanatajwa ni kutoka Sudan na Misri.

Wakati huo huo, Hichem Abu Chkiouat,Waziri wa Usafiri wa Anga katika utawala unaoendesha Mashariki mwa Libya, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa zaidi ya watu 5,300 waliofariki wamehesabiwa kufikia sasa, na kusema idadi hiyo huenda ikaongezeka kwa kiasi kikubwa.

Meya wa Derna, Abdulmenam al-Ghaithi aliiambia televisheni ya Al Arabiya inayomilikiwa na Saudi Arabia kwamba inakadiriwa idadi ya vifo katika mji huo inaweza kufikia kati ya 18,000 hadi 20,000 kulingana na idadi ya wilaya zilizoharibiwa na mafuriko.

Mkazi wa Derna Mahmud Abdulkarim alimwambia mwandishi wa habari Moutaz Ali mjini Tripoli kwamba alipoteza mama yake na kaka yake, baada ya kushindwa kuhama kwa wakati kutoka kwenye ghorofa yao kufuatia kuporomoka kwa bwawa.

"Alikataa kuondoka nyumbani kwake ... hakufikiria kwamba hali ingekuwa mbaya na akamwambia (Abdulkarim) ni mvua za kawaida tu," Ali aliripoti katika hafla iliyoandaliwa kwa jamii ya Derwani ya Tripoli.

Kwa mujibu wa Abdulkarim, mama yake na kaka yake walipoamua hatimaye kuondoka kwenye nyumba yao, walisombwa na mafuriko mara walipofika mitaani kukimbia.

Mabrooka Elmesmary, mwandishi wa habari ambaye alifanikiwa kuondoka Derna siku ya Jumanne, anaelezea jiji hilo kama "janga kwa kiwango kikubwa". "Hakuna maji, hakuna umeme, hakuna petroli," aliiambia Al Jazeera. "Mji umetulia."

Majengo ya ghorofa yenye familia ndani yamesombwa na maji, alisema. "Kuna wimbi la watu kuhama huku watu wakijaribu kutoroka Derna, lakini wengi wamekwama kwa sababu barabara nyingi zimefungwa au hazipo," Elmesmary alisema, akiongeza kuwa baadhi ya familia zimekuwa zikipata hifadhi shuleni.

Aidha, kumekuwa na wito wa kutaka msaada zaidi wa kibinadamu huku waathiriwa wakiwa wamefunikwa na mifuko ya miili na wengine kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja.

Mto wa maji ya mafuriko unaofanana na tsunami ulipiga Derna siku ya Jumapili baada ya bwawa kupasuka wakati wa kimbunga Daniel.

Vikosi vya uokoaji vinachimba vifusi vya majengo yaliyoporomoka kwa matumaini ya kupata manusura, ingawa matumaini yanafifia na idadi ya waliofariki bado inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Maafisa wanasema takribani watu 10,000 hawajulikani walipo, huku watu 30,000 wakikadiriwa kuwa wameyahama makazi yao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) nchini Libya lilisema Jumatano.

Daktari wa Libya Najib Tarhoni, ambaye amekuwa akifanya kazi katika hospitali karibu na Derna, alisema msaada zaidi unahitajika

Wakati huo huo,Serikali mbili zinazohasimiana nchini Libya zinaratibu juhudi za kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko, Umoja wa Mataifa umesema.

Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, Serikali zote mbili za Mashariki na Magharibi zimeomba msaada wa Kimataifa na zinawasiliana. (Mashirika)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news