Rais Dkt.Samia awaapisha Waziri na Naibu Waziri wa Nishati

NA VERONICA SIMBA-REA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 1, 2023 amewaapisha viongozi aliowateua Agosti 30, 2023 kushika nyadhifa mbalimbali.

Miongoni mwao ni Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa nafasi ya Naibu Waziri Mkuu (Uratibu wa Shughuli za Serikali) na Waziri wa Nishati pamoja na Mhe. Judith Kapinga kwa nafasi ya Naibu Waziri wa Nishati. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimuapisha Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu (Uratibu wa Shughuli za Serikali) na Waziri wa Nishati katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar tarehe 01 Septemba, 2023. 

Hafla hiyo fupi ya uapisho imefanyika Ikulu Ndogo Tunguu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya Siasa. 

Akitoa hotuba baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia amewataka kila mmoja kwenda kukiishi kiapo alichoapa kwa kusimama katika nafasi zao zinazowataka kuwatumikia wananchi na kujenga mahusiano mema nao. 

“Kiapo mlichoapa hata Mungu anakisikia hivyo naomba mkafanye hivyo mlivyoapa,” amesisitiza na kuongeza kuwa sifa ya upole kwa kiongozi siyo ujinga bali ni maarifa. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimuapisha Mhe. Judith Salvio Kapinga kuwa Naibu Waziri wa Nishati katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar tarehe 01 Septemba,2023.

Aidha, Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa mabadiliko aliyoyafanya katika uteuzi wa viongozi hao siyo adhabu bali ni ya kawaida yanayolenga kuimarisha utendaji kazi Serikalini. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wamewapongeza viongozi walioteuliwa na kuwataka kwenda kutimiza wajibu wao ipasavyo. 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto) akimpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko baada ya kuapishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Ndogo Tunguu Zanzibar Septemba 1, 2023.

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Janet Mbene na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, wametoa pongezi kwa Viongozi wapya wa Wizara ya Nishati walioapishwa na kuwaahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao hususan katika sekta ya nishati vijijini. 

Kabla ya uteuzi, Mhe. Dkt. Biteko alikuwa Waziri wa Madini na Mhe. Kapinga ni Mbunge wa Viti Maalum (Ruvuma).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news