TanTrade yazidi kusaka fursa za masoko, yatoa onyo kali

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara nchini (TanTrade) imesema imefanya uchambuzi wa takwimu katika Mfumo wa ITC na kutambua mataifa mbalimbali duniani yanayohitaji bidhaa kutoka hapa nchini.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 4, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu amekubali taasisi na mashirika hayo yatoke na kukutana na vyombo vya habari, lengo likiwa ni kuendeleza dhana ya uwazi na uwajibikaji, kwa sababu taasisi hizi ni mali ya umma hivyo lazima wapate taarifa kuhusu namna ambavyo taasisi au mashirika yao yanajiendesha.

Pia, Msajili wa Hazina anataka mashirika na taasisi hizo kuondokana na ile dhana kwamba, taasisi hizo huwa zinasikika wakati wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Leo, TanTrade ni taasisi ya 10 kupitia mwendelezo huo wa kuzikutanisha taasisi, mashirika ya umma na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Bi.Latifa amewaeleza wahariri hao kuwa,miongoni mwa mataifa ambayo yanahitaji bidhaa hizo kutoka Tanzania ni India, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uswisi, Vietnam, China, Pakistani, Japani, Marekani, Oman, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia.

Amezitaja bidhaa zinazohitajika huko kuwa ni dhahabu, korosho, ufuta,mbaazi, kahawa, dengu, almasi, vifungashio vya mifuko na pamba.

Mikakati

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, ili kuwaunganisha Watanzania na masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi, mamlaka hiyo inatekeleza mikakati mbalimbali kwa mwaka 2023/2024.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuendelea kuratibu shughuli za utafutaji masoko na ukuzaji biashara ili kuunganisha wazalishaji.

"Mikakati mingine ni kuendelea na taratibu za uanzishwaji wa Dawati la Waambata wa Kibiashara kwenye Balozi za kimkakati za Tanzania nje ya Nchi.

"Pia, kuendeleza ushirikiano na Balozi nje ya Nchi katika kutangaza fursa za masoko ya bidhaa na mazao yanayozalishwa nchini.

"Kuimarisha upatikanaji wa taarifa za kiintelijensia za biashara na kuimarisha na kukuza biashara za mipakani na kuimarisha Ofisi ya Zanzibar ili kuendeleza na kutafuta masoko ya bidhaa za kipaumbele."

Mbali na hayo amesema, TanTrade imejipanga kuratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2025 Osaka nchini Japani. 

Bi.Latifa amesema,TanTrade imeundwa kwa Sheria Na.4 ya Bunge ya mwaka 2009 yenye jukumu kuu la kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi.

Aidha,amesema dira yao ni kuwa kitovu cha ufanisi wa hadhi ya kimataifa (world class focal point), katika kuendeleza na kukuza uchumi wa Tanzania kupitia biashara.

Huku,dhima ikiwa ni kutafuta fursa za kibiashara kwa kampuni za Kitanzania na kuziunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi.

"Katika kufanya hivyo, mtaona sisi TanTrade tumekuwa kama Maafisa Balozi wataalamu wa Balozi zetu zote za Tanzania tulioko nje sambamba na Balozi zetu katika kuhakikisha tunatekeleza jukumu la kuunganisha masoko, tunaitangaza nchi, bidhaa, huduma kupitia majukumu yetu."

Mapato

Bi.Latifa amesema, katika kipindi cha miaka mitano TanTrade ilipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 52.562 na imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 40,004 sawa na asilimia 76.

Amesema, fedha hizo ni kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya mishahara na miradi ya maendeleo.

Sambamba na vyanzo vya mapato ya ndani ikiwemo ada inayotozwa kwenye uratibu na usimamizi wa maonesho, upangaji wakati usio wa Maonesho pamoja na ushiriki na viingilio vya Maonesho ya DITF.

"TanTrade tuna jumla ya watumishi 111 kati ya hao 54 ni wanaume na 56 ni wanawake. Tuna jumla ya vitengo pamoja na idara jumla yake ni 11."

Majukumu

Bi.Latifa amefafanua kuwa, TanTrade ina majukumu mbalimbali ikiwemo kusaidia mazingira rafiki ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ili kuyafikia masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

"Kutambua na kushauri mbinu bora za kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya biashara katika mnyororo wa thamani ili kuongeza thamani, kuhakamaisha uzalishaji wa bidhaa hapa nchini.

"Kushauri na kutoa mafunzo kwa jumuiya za wafanyabiashara juu ya namna bora za kusimamia biashara ndani na nje ya nchi, hili tunafanya kwa kushirikiana na makundi mbalimbali yoyote ambayo tunaona yanafaa katika hili."

Bi.Latifa anasema kuwa, mafunzo haya mara nyingi wanashirikiana na wadau wa kimataifa na wanafanya na taasisi za Kimataifa.

"Na tayari tuna mradi tumeshafanya, huu ni mradi wa bidhaa tano za viungo ikiwemo tangawizi, mdalasini.

"Kwa nini tumeanza na spicies hizo, kwa sababu nchi zetu jirani wananunua bidha hizo, lakini baadae hizo bidhaa wanazi-brand na kuzi export as zimetoka kule. 

"Tumeamua kufanya hivyo kwa ajili ya kupro-tect kwa sababu tuna jukumu la kuprotect.

"Sasa hivi tunaelekea kwenye asali, kama mnavyofahamu Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira mazuri na mazingira yote kwa hiyo tunapaswa kuprotect asali yetu na kuibrand vyema."

"Pia, kujenga na kukuza utamaduni wa kuuza biadhaa nje ya nchi kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kwa njia mbalimbali hii tayari tumeshawajengea uwezo, lakini kuna vitu vya kufanyia kazi."

"Kama nilivyosema jumuiya inavyokua, lakini na sekta na watu wanakua na hali ya ufanyaji biashara inakua."

Changamoto

"Kuna challenge kweli mazingira ya biashara yameingiliwa sana, yameingiliwa sana kwa sababu kuna watu wanatafuta fursa, kuna wafanyabiashara wa kweli ambao wako kwenye sekta na kuna wafanyabiashara ambao wanatumia fursa ya kuona kwamba wana uwezo wa kuuza nje."

"Kwa hiyo haya mazingira yameharibiwa kwa sababu yanaingiliwa na watu ambao sio waadilifu na waaminifu hawana uwezo kwa sababu ya image nchi."

"Sisi kama Watanzania tunapaswa kulinda hili na hasa wanaotumia hii mitandao ya jamii sana naomba hapa tusaidiane sana sana bila ninyi sisi kama Serikali hatuwezi kufanikiwa, sekta imeingiliwa sana na kuna utapeli unafanyika huko utakuta watu wanatangaziwa huko wanatengeneza link zao za bidhaa."

"Kwa mfano wakati wa vita ya Ukraine walijua kuna fursa ya alzeti, kuna watu wametengeneza mtandao alzeti tunauza sijui mafuta, kwa hiyo kuna kazi kubwa kama mamlaka tunapaswa kuifanya kuna watu wameingilia wasio waadilifu na waaminifu ambao ni wadau, lakini sio wadau naomba tusaidiane kwa upeo wenu na utaalamu wenu kwa sababu tuna njia mbalimbali za kuwajua na tukafanya kazi pamoja.

"Katika suala la trade fair, trade mission kama mnavyoshuhudia kwenye mitandao sasa hivi kila mmoja anatangaza, utakuta huyu anafanya maonesho.katika mwezi huu ukiingia mtandaoni utakuta picha za viongozi zinatumika mtu anasema mgeni rasmi hivi na hivi.

"Ni vitu ambavyo vipo na hatuwezi kuviepuka kwa peke yetu kama taasisi, lakini kwa ushirikiano na uzalendo wetu tutaweza."

"Kuna njia ambazo tunazifanya sasa hivi tunawazuia wengi, kuna taratibu ambazo tunazifanya, lakini ninaamini solution wakati mwingie si ambao wameajiriwa bali solution wakati mwingine wapo wengine walioko nyumbani na ninyi niwataalamu naomba tusaidiane."

"Kwa hapa ninaamini kuna wahariri, wataalamu mtaweza kutusaidia katika hili ninaamini mkitoka hapa mtakuwa msaada mkubwa sana."

"Katika jukumu jingine kukuza na kuwezesha uanzishaji wa miundombinu ya maonesho nchini katika hili, ndio ninalolisema utakuta kwenye maneo mengi tu kwenye mitandao tumepiga unthorized hizo ni miundombinu ambayo tuna ikataa sasa tuweze kui-control."

"Utakuta kuna watu wanasema tunafanya maonesho kila mtu, maonesho zamani ilikuwa sehemu ya kufanya promotion na inakuwa na lengo maalumu, lakini kwa sasa imekuwa income, mtu amekaa tu nyumbani anataka kiongozi achangie, anaandika barua anatafuta hela anapeleka kwenye mabenki anaita wadau anafanya shughuli kwa hilo hatulishangai tumeshika hatamu kwenye sheria yetu tunawakamata."

"Kuna kipindi hata mimi niliandikwa sana kwa sababu nilizuia watu ambao ninaamini wako nyuma wanajiamini, lakini na mimi nilijiamini kwa sababu sheria naisimamia namba 4 ya mwaka 2009 na nitaendelea kufanya hivyo kwa kila ambaye atakuwa hajapata kibali tutaendelea kuwazuia."

"Majukumu mengine ni kuratibu maonesho ya biashara na misafara na mikutano ya kimataifa hilo ni jukumu ambalo kwa sasa limeingiliwa sana.

"Kuna watu wengi sana wanafanya misafara bila vibali maalumu,kwa nini tunawazuia sisi kama taasisi huwezi kufanya trade mission unaiita hivyo kumbe ni tour wakati kuna watu ambao wana leseni, wanafanya hiyo biashara na wanalipia kodi zote za serikali kwa nini unaenda kwenye biashara za watu?.

"Kwa hiyo hicho ndio tunawazuia, kama wewe ni tour mwache mwenye tour wewe umejiandikisha kama NGO ya wajasirimali endelea na hiyo NGO na usifanye kazi ambayo hukupewa kibali wala hujajisajili unataka kufanya hivyo fuata sheria."

"Na wale wenzetu wanapata faida kwa sababu unakuta mtu mmoja ana-mcharge kichwa dola 2500, ukipiga hesabu ana watu 50 yeye ameingiza income anapiga kelele kwa nini tume-mcharge sisi kama TanTrade lazima tumcharge.

"Kwani iko kisheria na sidhani Kama hawa watu walioanzisha hii sheria ya TanTrade kuweka ile charge ile wameiweka kwa sababu waliona hii environment ilikuwa imechafuliwa, kwa hiyo baada ya environment kuchafuliwa kikaanzishwa hicho kipengele cha kuratibu hiyo misafara kwa sababu kuna heshima ya nchi pia."

"Kuna wanaokwenda kule wanaondoka hapa kama trade mission kutoka Tanzania, lakini vitu wanavyokwenda kuvifanya kule sio vizuri kwa heshima ya nchi. 

"Kwa hiyo lazima tuprotect kwa sababu sisi ni taasisi ya serikali na wale wengine wasije wakaharibu image za wafanyabiashara ambao ni waaminifu na tabia mbaya ya mtu mmoja isiharibu tabia ya watu wengine ambao ni wema."

Bi.Latifa amesema,TanTrade inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuwa kitovu cha biashara kwa kuendeleza, kukuza na kutangaza bidhaa na huduma ndani na nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news