Tanzania yavuka malengo mapambano dhidi ya VVU

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema usimamizi makini wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umewezesha Taifa kuvuka malengo ya kupambana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) ya 95-95-95 yaliyopangwa kufikiwa mwaka 2025.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Mdahalo wa Kitaifa wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virus vya Ukimwi (NACOPHA) uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Septemba 7, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Leo hii tayari asilimia 96 ya watu wanaoishi na mambukizi ya VVU wanajua hali zao, asilimia 98 ya wanaojua hali zao wapo kwenye tiba ya ARV na kati yao, asilimia 97 wameweza kufubaza wingi wa virusi kwenye damu. Jukumu kubwa la Taifa tulilonalo ni kulinda na kuyaendeleza mafanikio haya kwa nguvu za pamoja na umoja hadi tufikie malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030.”

Ameyasema hayo Septemba 7, 2023 alipomuwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Mdahalo wa Kitaifa Juu ya Kuimarisha Ubia Baina ya Serikali, Wadau na Jamii kwa Uendelevu wa Mafanikio ya Mwitikio wa UKIMWI nchini uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji na mifumo endelevu ya upatikanaji rasilimali fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za UKIMWI ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund) na mipango mbalimbali katika ngazi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla ili malengo ya kutokomeza ugonjwa huo yaweze kufikiwa.

Akizungumzia kuhusu majumuisho yaliyotokana na mdahalo huo, Waziri Mkuu amewahakikishia wadau na Watanzania wote kuwa Serikali imesikia na kupokea yote yaliyotajwa katika mdahalo huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) na itayafanyia kazi. “Suala la ubia halikwepeki tunatambua umuhimu wa ushirikiano na tutalitekeleza kwa maslahi mapana ya Watanzania.”

“Licha ya hayo, Serikali itazidi kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali waliopo nchini na nje ya nchi hasa katika uwekezaji, kutoa elimu, vifaa tiba, wataalamu, maboresho ya Sera na miongozo mbalimbali ya masuala ya UKIMWI.Tumewasikia wadau na pia tumepata maoni kutoka kwa ndugu zetu WAVIU. Maoni haya yatasaidia kuboresha mikakati ya Serikali katika kuhakikisha tunafikia malengo.”

Amesema licha ya tafiti kuonesha kupungua kwa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya VVU nchini, bado matendo ya unyanyapaa na ubaguzi na ukatili wa kijinsia yanaendelea kuwa kikwazo katika kuzifikia na kuzitumia huduma za VVU hasa kwenye jamii, Shuleni, vyuoni na mahala pa kazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amempongeza Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kupambana na masuala ya UKIMWI nchini. “Mheshimiwa Waziri Mkuu kutokana na juhudi zako, maelekezo na uamuzi wa kuwa Balozi wa kuhamasisha Wanaume kupima maambukizi ya VVU, uelewa kwa Watanzania wanaofahamu hali zao kuhusu VVU umeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2016/2017 hadi kufikia asilimia 97 mwaka 2023.”

Naye, Mwenyekiti wa NACOPHA, Leticia Moris amesema baraza hilo limetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, hivyo ameishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuhakikisha huduma mbalimbali zikiwemo dawa za kufubaza VVU zinaendelea kupatikana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news